
Nafanya hivyo kwa sababu maswali yanayoulizwa ni mengi sana, ambayo si rahisi kuyajibu kwa njia ya SMS, lakini pia naamini kupitia majibu ya maswali haya, hata ambao hawajatuma wanaweza kupata darasa kupitia maswali na majibu haya. Hebu tuone.
NIMEMUACHA LAKINI BADO NAMPENDA
Shikamoo kaka Shaluwa, mimi ni binti mwenye miaka 22, nilikuwa na mpenzi wangu, lakini kwasasa nimeachana naye. Tatizo lake yeye alikuwa mtu wa hasira sana. Kitu kidogo anakasirika, yaani hata ukimtania tu kidogo anakasirika na anaweza kukununia hata wiki nzima.
Lakini cha ajabu, ukimpigia simu anazungumza vizuri tu, kiasi kwamba mkiagana mna-kiss, lakini baada ya hapo anakuwa kimya. Mbaya zaidi huwa hapendi kabisa kuwasiliana. Yaani mpaka mimi nimpigie, nisipompigia na yeye atakuwa kimya moja kwa moja.
Mambo yote hayo yalinikera nikaamua kuachana naye, lakini moyoni mwangu bado nampenda. Nifanyeje?
Naima, Arusha.
MAJIBU YA SHALUWA: Kila mtu ameumbwa akiwa na kasoro zake, tabia pia tunatofautiana. Ukiyajua hayo ni rahisi kumsoma mtu na kujua namna ya kuishi naye. Ni kweli mawasiliano ni ngao ya mapenzi ya kweli, lakini kuna watu ambao hawana ‘hobi’ kabisa ya kupiga simu na kuandikiana SMS.
Hukutakiwa kufanya maamuzi ya haraka kiasi hicho hasa kutokana na ukweli kwamba, umesema mwenyewe kuwa bado unampenda. Kwa hali hiyo, kama wewe ndiye uliyemuacha na moyoni mwako bado kuna chembechembe za mapenzi, una uwezo wa kukutana naye na kumweleza hisia zako, huku ukiweka wazi mambo unayopenda akufanyie.
NINA MIMBA YA MIEZI SABA, MPENZI WANGU ANATAKA NIKATOE...
Hi, kaka Jose. Naitwa Asha, nina mpenzi wangu ambaye nimekuwa naye katika mapenzi kwa kipindi cha mwaka mmoja na sasa nina mimba ya miezi sita inaendelea saba.
Hivi juzi, nimegundua kwamba kumbe huyu bwana alikuwa na mkewe ila walikuwa wameachana lakini bila talaka, sasa jamaa ameamua kurudiana na mkewe, lakini mbaya zaidi anasema eti nitoe hii mimba kwakuwa hana mahali pa kuniweka kwani hata huyo mkewe naye ana mimba.
Hapa nilipo, nipo njia panda. Naomba msaada wako, nizae au nitoe hii mimba? Ushauri wako ni muhimu sana kaka Shaluwa.
MAJIBU YA SHALUWA: Nimekuwa nikisisitiza sana kuhusu kuchunguzana kabla ya kuanzisha uhusiano.
Huyo mwanaume umemkurupukia sana, maana kama mna mwaka mmoja na tayari una mimba ya miezi saba, maana yake hapo ni kwamba ulianza kukutana naye kimwili ndani ya miezi mitatu baada ya kukutana, tena bila kinga, hiyo ni hatari sana.
Nikirudi katika hoja ya msingi ni kwamba, hutakiwi kutoa mimba (hata kama ingekuwa na wiki moja), kwanza kufanya hivyo ni kosa la kisheria lakini kubwa zaidi ni kwamba hakuna imani yoyote inayokubaliana na utoaji mimba.
Anza kufanya mchakato wa namna atakavyowajibika kumlea mwanaye, hata kama amesharudiana na mkewe. Wakati mwingine uwe makini, wanaume wa siku hizi ni matapeli sana na wanaweza kukuharibia maisha yako.
NILIVYOCHOKA ALINITOSA, SASA MAMBO SAFI ANATAKA TURUDIANE, NIFANYEJE?
Mambo bro Shaluwa? Kaka mimi ni msomaji wa hadithi zako pamoja na makala zako magazetini, kiukweli zimenibadilisha na kunipa mwanga wa maisha yangu.
Nilikuwa katika uhusiano wa kimapenzi na msichana mmoja hivi tangu nikiwa nasoma, baada ya kuhitimu masomo yangu mwaka 2008, bahati mbaya baba yangu mzazi ambaye alikuwa tegemeo langu kwa kila kitu, alifariki dunia.
Hapo hali ya maisha yangu ikabadilika na kuwa mbaya sana. Tangia hapo mpenzi wangu akabadilika na kuanza kuwa na tabia mbaya. Nilipofanya uchunguzi nikagundua kwamba yawezekana ni kwa sababu maisha yangu yameyumba, nikaamua kuachana naye.
Baada ya kuhangaika kwa muda, sasa hivi nimepata kazi ambayo ni msaada mkubwa sana kwangu. Maisha yangu yanaenda vizuri, sasa cha ajabu yule msichana anarudi anaomba msamaha na kutaka nirudiane naye, akidai kwamba ni shetani tu ndiye aliyekuwa akimtawala kwa kipindi kile.
Je, kuna mapenzi ya dhati hapo? Ni kweli amebadilika? Naomba msaada wako kaka Shaluwa.
Abasi, Masasi.
MAJIBU YA SHALUWA: Siri ya penzi la dhati ni pomoja na kuvumiliana, anayekosa uvumilivu hana mapenzi ya kweli. Kupima penzi la kweli, mara nyingi ni hasa unapokuwa katika matatizo. Maelezo yako yanaonesha moja kwa moja, huyo msichana hana mapenzi ya kweli, anaangalia ‘pochi’ lako.
Usijidanganye kwa kumpenda kwako, ukamkaribisha tena, unaweza kuja kulia sana. Akili kichwani mwako.
NINA BIKRA, LAKINI MZUKA UNANIPANDA SANA!
Pole na kazi kaka’ngu. Naitwa Hellen, nina miaka 23, tangu kuzaliwa kwangu sijawaji kukutana kimwili na mwanaume (bikra), lakini siku za hivi karibuni kila nikimuona mwanaume nachanganyikiwa!
Hamu ya kufanya mapenzi inapanda sana mpaka nachanganyikiwa.
Tatizo ni nini na nifanyeje ili hii hali iniondoke?
MAJIBU YA SHALUWA: Kwanza hongera sana kwa kujitunza mdogo wangu. Kwa umri wako kuwa na bikra ni heshima kubwa sana kwako na hata kwa wazazi/walezi wako. Endelea kujitunza mpaka siku ya ndoa yako.
Cha kufanya kwasasa ni kufanya mazoezi, achana na ‘kampani’ ambazo stori zake zinahusisha ngono, punguza vyakula vya protini na mafuta, soma sana vitabu (lakini si vinavyohamasisha ngono) na kubwa zaidi unalotakiwa kufanya ni kuzingatia zaidi mafundisho ya imani ya dini unayoiamini.
ANANITAKA KWA NGUVU, NAOMBA MSAADA
Pole na kazi kaka Joseph. Mimi ni binti ambaye ninaye mpenzi wangu na tunapendana sana, sasa kuna kaka mmoja anaonekana kunitaka kwa nguvu kiasi kwamba ananitishia. Naomba msaada wako maana sina amani kabisa.
MAJIBU YA SHALUWA: Hakuna mapenzi ya kulazimishana siku hizi dada yangu. Kwanza muonye kwa msisitizo ukimaanisha kwamba humtaki kabisa kwakuwa una mpenzi wako. Akiwa haelewi, mweleze mpenzi wako ili afahamu maana mwisho anaweza kuharibu uhusiano wa wewe na mpenzi wako.
2 comments:
Pole snaaa
Me nilikuwa na mpenzi wangu Sasa hapo kipindi Cha nyuma alikuwa ananipenda kweli ila gafra nashaanga hataki hata kuja geto tena wakati zamani alikuwa yeye ndo wa kwanza kuniambia kuwa leo nataka nije geto harafu hata nikwambie Siku hizi natamani tuonane sababu zinaanza kuwa nyingi me sina mda wa kuja huko hivi kaka tatizo linaweza kuwa ni Nini?
Post a Comment