
Hii ina maana kuwa hata katika maisha ya mapenzi kuna watu wema, wastaarabu wanaoheshimika na jamii huweza kuangukia katika mikono ya wapenzi wabaya ambao hawakuwatarajia kabisa, si kwa sababu walikuwa wavivu kuchagua bali walipata ajali za kimapenzi.
Unaposoma mada hii unaweza kuwa mmoja kati ya watu wapole, wanaojiheshimu lakini mumeo akawa ni mtu wa kukutia aibu kwa kulewa mpaka kuvua nguo. Kitu kibaya kabisa katika maisha ya namna hii ni pale wahusika wanapojenga mbinu za kuwafanya wanaowaonea kujiona kuwa hawana chaguo zaidi ya kubaki katika hali hiyo.
“Wanawake wengi husema “...nitafanyaje nd’o nimeshaolewa” Husema hivyo wakiwa wameaminishwa kupitia mahubiri ya wanaume wabaya kwamba hakuna maisha mengine nje ya uhusiano wao huo, nje ya mapenzi ya mume huyo au wakati mwingine huvumilia aibu kwa vitisho. “Ukiondoka nitakuua”
Tatizo la wanawake kuishi maisha ya kuonewa limezidi kuwa kubwa nyakati hizi na familia nyingi zimekuwa maskini kutokana na kulelewa katika familia za mfumo dume ambao wakati mwingine huvuka mipaka na kuathiri watoto.
“Tulikimbia nyumbani kwa sababu baba alikuwa anatutesa…alikuwa akirudi anatupiga sisi na mama …tukaamua kutoroka …tukaja kwa rafiki yetu …akawa anatuletea wanaume…kwa sababu ya dhiki tukawa tunakubali kufanya nao mapenzi.” Hizi ni kauli za watoto wanaolelewa na wanawake ambao wameangukia kwenye mikono ya wanaume wabaya.
Katika uchunguzi wangu si wanawake walioolewa tu ndiyo wanaoathirika na mapenzi ya wanaume wenye tabia mbaya, bali hata wapenzi wa kawaida tu wamekuwa wakiteswa na tatizo hili.
Utakuta msichana mrembo atanyanyaswa na mwanaume kwa kupigwa, kuporwa mshahara wake lakini hachukui hatua za kujitambua na kuachana na mwanaume asiyekuwa na mtazamo mpana wa maisha, badala yake ataendelea kuishi naye miaka nenda rudi bila mafanikio na cha kufanya ni kuteswa, haya si maisha kuna hatua za kuchukua ili kuondokana na hali hii.
Kwanza: Ni kutokuwa tayari mapema kutoka moyoni kuishi na mwanaume asiyekuwa na tabia njema. Tatizo la wanawake wengi hujidanganya kuishi na wanaume wenye matatizo kwa kisingizio kuwa wataweza kuwabadilisha tabia.
Kibaya zaidi wakati wanafanya hivyo huchukua uvumilivu mkubwa ambao hauhitajiki katika kutatua tatizo na kumfanya mhusika kuweka misingi imara ya maisha yake kama mwanadamu. Usikubali kuwa na mpenzi mwenye tabia mbaya na ikitokea umeangukia mikononi mwake usimvumilie sana!
Pili : Kuwa na msimamao. Wanawake wengi wanakasoro za kusimamia maamuzi yao, wengi wao ni waoga hata kwenye maumivu, hawako tayari kuweka wazi kasoro za waume zao kwa hofu kwamba watawapoteza, ni hodari kupamba ubaya wa wapenzi wao na kukubali malipo ya mateso, jambo ambalo huwapa kiburi wanaume cha kuona hakuna umuhimu wa kubadili tabia kwa vile wanaoishi nao wanawatawala. Msimamo ni jambo la lazima.
Tatu: Ni kulinda familia: Kwa wanawake walioolewa wasikubali tabia za baba ziathiri malezi ya watoto kwa vile katika ustawi wa familia, watoto ni wa kuwaangalia zaidi kuliko kitu kingine. Mwanamke ambaye anaishi na mwanaume mwenye tabia mbaya lazima ahakikishe kuwa mifarakano na uovu haurithishwi kwa watoto.
Nne: Kuchukua hatua. Pale madhara ya tabia mbaya za mwanaume au mpenzi yanapokuwa makubwa, hakuna njia mbadala zaidi ya kuchukua maamuzi magumu ya kuachana na mwanaume huyo haraka na kuanza maisha mapya. Kinachosikitisha ni kwamba wanawake wengi ni wagumu kwenye kuchukua hatua kwa kisingizio cha kupenda.
Lakini wanashindwa kuelewa kuwa mapenzi si kitu kinachoendana na karaha au mateso. Siku zote mapenzi ya kweli ni yale yanayojengwa katika misingi inayouridhisha moyo kwa kiwango cha juu.
Hebu jiulize ni lini utaachana na huyo mchumba feki au mpaka uzeeke, utamvumilia mpaka lini mwanaume mkorofi? Unajidanganya sana chukua hatua mapema, duniani kuna vitu vingi vya kupenda zaidi ya huyo uliyenaye.
Tano: Katika kila unalofanya washirikishe wengine ili wakushauri, unapokuwa katika hali ya kuonewa na mwanaume mbaya uliyeangukia mikononi mwake washirikishe rafiki zako, ili wakushauri njia sahihi za kuchukua na hasa wale ambao waliwahi kupata mikasa kama yako.
Somo hili linawafaa pia wanaume waliopata ajali ya kuwa na wanawake wenye tabia mbaya. Najua unapenda kujua zaidi elimu hii ya mapenzi, kaa tayari kitabu cha TITANIC N0 3 kitakata kiu yako.
Kwani kimesheheni meseji,makala za mapenzi pamoja na chombezo mbili, Vuvuzela Kitandani na Mshauri wa Mapenzi.
No comments:
Post a Comment