ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 2, 2010

Marando ataja sababu ya kung’oka NCCR

Mabere Marando
Na Elvan Stambuli
KADA wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mabere Marando ametoa sababu ya kung’oka na kukikimbia Chama Cha NCCR Mageuzi na kujiunga anachokipigia debe sasa.

Akihutubia mwishoni mwa wiki iliyopita katika mkutano wa kampeni wa kumnadi mgombea wa Ubunge wa Chadema katika Jimbo la Kawe jijini Dar es Salaam Halima Mdee, Marando aliwaasa wakazi wa Kawe kutochagua wagombea wa CCM na NCCR Mageuzi kwa kuwa hawatakuwa na msaada wa kimaendeleo kwenye jimbo hilo.
Kuhusu Mgombea Ubunge kupitia NCCR Magezuzi James Mbatia, Marando alisema ndiye aliyesababisha yeye kukihama chama hicho.

“Mimi ni mkazi wa jimbo hilo, maendeleo ya jimbo hili yananihusu, nilimwambia Mbatia kama atagombea Ubunge katika jimbo nitakihama chama hicho kwa kuwa yeye hana uwezo wa kuongoza na amekiua chama hicho,” alisema Marando.

Alisema amekihama sababu anajua mgombea huyo kupitia NCCR Mageuzi hana uwezo wa kuongoza kutokana na kushindwa hata kufuatilia matatizo makubwa ya ardhi yaliyowakumba wakazi wa eneo hilo huku akiwa kama mwenyekiti wa chama hicho na mkazi wa jimbo hilo.
Marando alirudia kauli hiyo aliyoitoa katika Viwanja vya Jangwani kwa kusema kuwa bado anaamini kuwa mafisadi wa kweli hawajafikishwa mahakamani.
Katika mkutano huo, Marando alisisitiza kuwa watu waliofikishwa mahakamani si mafisadi, bali ni matawi ya ufisadi. 

Huku akishangiliwa na umati wa watu Marando alisema; “ Nilipozunguzia hili wakati wa kufungua kampeni TBC (Shirika la Utangazaji la Tanzania ) walikata mitambo yao,sasa leo narudia tena na hapa hukuna mitambo sijui watakata nini,”alisema Marandu na kucheka.

“Niliwaambia kumfunga Liyumba, kumshitaki Maranda na wengine ambao kesi zao ziko mahakamani kwa sasa siyo suluhisho la ufisadi hapa nchini, nasema hivyo sababu wale waliofikishwa mahakamani ni matawi tu na mafisadi ni mti mkubwa ambao unatakiwa kung’olewa.

Mafisadi halali ni wale waliotajwa na Dk.Slaa waziwazi katika Viwanja vya Mwembe Yanga, alitaja majina yote na kuonyesha Watanzania wote kuwa kumbe wizi uko hata (Bot) mahali ambapo Watanznaia hata siku moja hamukuamini kama kuna wizi unafanyika,” alisema Marando.

Akifafanua maana ya ufisadi alisema; “Mafisadi maana yake ni viongozi wanaotumia nafasi zao kuchota fedha za umma zilizotengewa kwa ajili ya ujenzi wa huduma za kijamii kama shule, zahanati, barabara n.k na kuzitumia wao binafsi na marafiki zao.”

No comments: