
Wiki iliyopita mtakumbuka kuwa nilijaribu kujibu baadhi ya maswali ambayo ninyi wasomaji wangu mmekuwa mkiniuliza mara kwa mara. Ni utaratibu niliojiwekea wa kujibu maswali yenu mara moja kwa mwezi hivyo, kama una jambo linalokutatiza kuhusu mpenzi wako na maisha yako kwa ujumla usisite kunitumia kwa njia ya meseji kupitia namba za simu zilizopo hapo chini.
Ndugu zangu, huu ni mwezi mtukufu na kutokana na hivyo mtaona mada ambazo naziandika zinagusa sana maisha yetu ya kimapenzi ndani ya mwezi huu. Mnaonaje wapendwa? Au mnadhani nitakuwa sahihi kama nitaanza kuzungumzia mada za namna ya kudatishana faragha? Itakuwa siyo freshi jamani au siyo! Naamini hata haya ninayoyaandika yatakuwa na faida kwenu pia, siyo kwa Waislamu tu bali hata Wakristo.
Wiki hii nataka kuzungumzia suala la mavazi kwa wapenzi hasa kwa kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa ndugu zetu Waislamu. Suala la mavazi limekuwa likileta mkanganyiko kwa walio wengi. Wapo wanawake wanaolazimika kuvaa mavazi yasiyo ya kistaarabu eti kwa sababu tu wapenzi wao wanataka hivyo.
Lakini pia, wapo wanaume wanaokerwa na staili ya uvaaji ya wapenzi wao lakini wasichana hao wakivaa hivyo wanadai eti wanakwenda na wakati na lengo ni kupendeza. Ndipo pale unaweza kujiuliza, kupendeza kwa msichana ni lazima avae nguo za kubana zinazoacha wazi baadhi ya sehemu zake nyeti?
Yawezekana tukawa tunatofautiana katika hili lakini kiukweli kabisa suala la kupendeza halina uhusiano na kuvaa nguo ambazo si za kiheshima. Upo ulimbukeni uliopo kwa baadhi ya wasichana kwamba, wakivaa nguo za aina flani wanapendeza na wanawadatisha wanaume bila kujua kuwa, wakati mwingine yawezekana ikawa ni sababu ya kutoheshimika katika jamii.
Kwa mwanamke makini suala la avaeje halimhusishi mpenzi wake tu. Msichana wa sampuli hii anapofungua kabati na kuangalia nguo ya kuvaa, lazima atajiuliza maswali ya kwamba; ‘Nguo hii nikiiva nitapendeza na mpenzi wangu atafurahi lakini je, jamii itanichukuliaje? Hivyo ndivyo inavyotakiwa kuwa kwa kila mmoja wetu.
Nasema hivyo kwa sababu, suala la uvaaji limewashushia wengi heshima mbele ya jamii na hii ni kwa wale wasiojali. Hawa ni wale wanaoishia kusema; kwani wakiona matiti yangu tu wanayachukua? Hivi jamani kuvaa nguo zinazoacha wazi sehemu nyeti za mwili wako au zinazobana ndiyo kupendeza? Kama ni hivyo basi neno kupendeza naweza kusema maana yake inapotoshwa.
Nasema inapotoshwa kwakuwa, kila mmoja anavaa nguo ili apendeze sasa kutembea uchi kwa msichana nako ni sehemu ya kupendeza au ni kutafuta soko la wanaume? Sisemi kwamba kuvaa mavazi yanayobana na mengine ya namna hiyo ni umalaya au kutojiheshimu, la hasha! Cha kujiuliza ni kwamba, una nia gani kuvaa hivyo? Watu wajue jinsi ulivyoumbika?
Wakishajua sasa unataka wafanye nini? Sawa labda wewe huna mtu na lengo lako ni kutamanisha wanaume kisha wakutongoze (Licha ya kwamba sio njia sahihi ya kutafuta mpenzi) lakini je, wewe uliye na mpenzi au mume kuvaa mavazi hayo unatafuta nini? Hudhani unajitafutia usumbufu kutoka kwa wanaume wakware bila sababu za msingi?
Mimi naona kuna kila sababu ya kuwa makini katika hili. Vaa kiheshima kwa kuzingatia huo huo uhuru wa kuamua avae nini, wapi na wakati gani.
Kumbuka tu kwamba kuvaa nusu uchi, nguo zinazobana unajenga picha flani kwa watu licha ya kwamba hivyo wanavyoweza kufikiria vinaweza kukosa ukweli ndani yake.
Angali ndani ya mwezi huu wa Ramadhani, watu wengi sana wamekuwa wakivaa nguo zinazositiri miili yao na wanapendeza kuliko hata wanapovaa nguzo za kubana na kimitego. Lakini mwezi ukiisha wanarudi kule kule. Mwezi huu iwe sababu ya kutubadilisha kabisa.
Nimalizie kwa kusema kwamba, usivae nguo kwa kumfurahisha mpenzi wako kwani tambua wanaume wengine akili zao hazijatulia. Nasema hivyo kwa sababu, msichana anapovaa nguo inayosababisha chupi yake kuonekana au mapaja na matiti kuwa wazi kisha mwanaume wake akajiona fahari na hata kuwa tayari kutembea naye, huko ni kujichoresha.
Kwa wiki hii nimejaaliwa kuwafikishia hilo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine kali zaidi.
No comments:
Post a Comment