ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 27, 2010

Kisa na Mkasa na salim Kikeke

Wachimbaji na namba 33

Katika tukio la kunasa na kuokolewa kwa wachimbaji nchini Chile, kuna mambo ambayo yameoneakana na kuhusishwa na sakata zima. Kulikuwa na wachimbaji thelathini na watatu walionasa, ilichukua siku thelathini na tatu kuchimba na kuwafikia.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, watu wengine wanasema imetokea tu, lakini wengine wanasema, hata kuna kitu hapa. "Kazi ya kuchimba ilichukua siku thelathini na tatu, siku moja ya kila mmoja" amesema Mikhail Proestakis, meneja wa kampuni iliyochimba shimo la kuwaokoa. Shimo hilo lilikuwana upana wa diamita sitini na sita, ambayo ni thelathini na tatu mara mbili.
" Ninaamini masuala ya namba, lazima ina maana" amesema Mikhail.
Shughuli ya kuwaokoa wachimbaji hao ilianza Oktoba kumi na tatu, ambapo tarehe hiyo ikiandikwa kwa namba inasomeka kama kumi na tatu, kumi, kumi -- yaani tarehe kumi na tatu, mwezi wa kumi mwaka elfu mbili na kumi. Ukijumlisha kumi na tatu, na kumi na kumi, jawabu ni thelathini na tatu.
Jambo hilo alilisema hata rais wa Chile Sebastian Pinera. "Hii namba thelathini na tatu inatokea kila mahala, yaani ni miujiza" amesema Maria Segovia, dada wa mmoja wa wachimbaji walionasa. Aidha waumini kadhaa wa Kikatoliki walisema Yesu alikuwa na umri wa miaka thelathini na tatu wakati alipotundikwa msalabani.
Na wengine wamesema ujumbe wa kwanza wa maandishi uliotumwa na wachimbaji hao kuonesha kuwa bado wako hai ulikuwa na herufi thelathini na tatu. Ujumbe huo ulisomeka hivi "estamos bien en el refugio los 33".

No comments: