ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 20, 2010

Lipumba atumia dawa bila vipimo

Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akizungumza na wananchi waliohudhuria moja ya mikutano yake.
Na Mwandishi Wetu
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Haruna Lipumba ameanza kutumia dawa za malaria bila kupimwa.

Habari zinasema kuwa Lipumba akiwa kwenye ziara zake za kampeni Kanda ya Ziwa, alibanwa na homa, hivyo kwenda Hospitali ya Wilaya ya Kwimba, Mwanza Ijumaa iliyopita lakini madaktari hawakuwepo.

Vyanzo vyetu vinasema kuwa baada ya kukutana na hali hiyo, ilimbidi Lipumba kurudi hoteli aliyofikia lakini baadaye alinunua dawa za malaria na kuanza kujitibu kutokana na uzoefu wake kwa kuangalia dalili za maradhi yanayomsumbua.

Watoa habari wetu waliendelea kuweka kweupe kwamba Jumamosi iliyopita, Lipumba aliitumia kupumzika na kufanya mkutano mmoja wa kampeni Kata ya Ngudu, Kwimba badala ya 11 iliyokuwepo kwenye ratiba.

“Hivi sasa (juzi) anaendelea vizuri na ni matarajio yetu atazidi kuimarika ili kuendelea vema na mikutano yake ya kampeni,” kilisema chanzo chetu cha habari ambacho kimeomba hifadhi ya jina lake kwa sababu hakihusiki na usemaji wa afya ya kiongozi huyo.

Katika hatua nyingine, Lipumba aliye Mwenyekiti Taifa wa CUF, ‘alitisha’ Ngudu kutokana na staili yake ya kuhutubia kwa kuchambua ilani ya CCM ya mwaka 2005, huku akiwafafanulia wananchi ambavyo haikutekelezwa.

Lipumba, aliwataka wananchi kuwa makini na uchaguzi wa mwaka huu kwa kuhakikisha wanakipumzisha CCM ili maendeleo ya kweli yaweze kuja na kuondokana na hali ngumu ya maisha inayowakabili.
                                                      CHANZO GPL

No comments: