
Kwa mara nyingine XXLOVE imetukutanisha kwa uwezo wa Mungu. Tutoe shukurani kwake muweza wa yote, kwani bila dhati yake, si mimi, wewe wala kiumbe chochote kingepata fursa ya kuona mwangaza wa dunia.
Kipengele cha mwisho wiki iliyopita, nilikutaka uheshimu joto na harufu yake ya asili. Kuna watu wengi hawajui hili kwamba uasili wa mtu, huchangia kuongeza mvuto wake. Kwamba akiwa na wewe, kesho akiwa na yule aone tofauti.
Hapa kuna pointi muhimu zaidi kisaikolojia. Kuna watu ni hodari kwa kuondoa uhalisia wa kitu. Hawataki harufu yao ya asili isikike. Asubuhi manukato, mchana hivyo hivyo mpaka usiku kabla ya kupanda kitandani atahakikisha anajipulizia au anajipaka uturi.
Je, anafanya hayo yote kuogopa nini? Uasili wa mtu ni nyenzo muhimu mno. Harufu asilia ya mtu na joto lake, ni jawabu la utulivu wa moyo kwa mtu ambaye ametosheka navyo. Mapenzi ya kweli hayahitaji nakshi nyingi za bandia.
Unaweza kuchangamsha chumba chako kwa hewa nzuri (air refresher) na udi kama unapenda lakini suala la kuunukisha mwili wako uzuri, itokee kwa vipindi maalum. Siyo kila siku, utamfanya mwenzako ashindwe kuakisi joto na harufu asilia kutoka kwako.
Harufu yako ni kielelezo cha kukupa upekee ulionao. Lazima mwenzi wako hata ikitokea bahati mbaya akaenda kutenda dhambi pembeni, aone tofauti kati yako na huyo. Muhimu kwako ni usafi. Hicho ni kitu cha kusimamia popote.
KUNA WANAOJIMWAGIA MANUKATO KABLA YA KUINGIA FARAGHA
Wanafanya kosa, ingawa katika baadhi ya vipindi hupatia. Kuna mambo mengi ya msingi ya kuzingatia lakini uturi wa kila mara hauna maana. Utakufanya kila siku uwe wa bandia na zaidi ya yote hutomvuta mwenzi wako moyoni.
Utamvutia juu juu kwa harufu ya ‘kufoji’, lakini fahamu kwamba akienda pembeni akikutana na mtu anayejimiminia uturi kama wako, ataona sawa. Si ajabu akajiona ni mwenye huba kama ambavyo hujisikia akiwa na wewe.
Hiyo ni hatari mno katika kuliweka penzi lako kuwa la kipekee. Kwa mantiki hiyo, kataa kufananishwa na mwingine, usikubali alinganishe raha zako na za mwingine. Baki na uasili wako, ila ukiona haja ya kuchombeza harufu basi iwe katika vipindi maalum.
USAFI IWE KILA KITU
Ni vizuri kila mtu afanyie kazi hili kwamba kuna wakati mwili unakuwa unahitaji zaidi. Hapo hamasa yake huwa ni kubwa. Hapo sishauri kukimbilia kwanza bafuni kwa sababu maji hupoteza ‘stimu’ za mwanzo.
Hata hivyo, ni vizuri kuhakikisha mwili wako unakuwa safi muda wote. Muhimu zaidi ni kuhakikisha yale maeneo yenye jasho la mafuta yanadhibitiwa kwa nguvu zote. Harufu za ajabu hazitakiwi kwa sababu zitayeyusha mguso wa moyoni.
Unapaswa kudhibiti harufu ya kwapa, halafu weka mkazo kwenye maeneo nyeti. Nimekuwa nikielekeza kwamba si busara kwenda haja ndogo halafu akili yako ikawa kuwahi kutoka ili uendelee na shughuli nyingine.
Usiwe mvivu, jisafishe ndugu yangu. Tumia maji ya kutosha. Achana na tissue. Mkono wako ukupe jibu pale unapopitisha vidole na kuhakikisha viashiria vya utelezi havipo. Ukiweza hilo, hutakumbana na aibu ya kutoa harufu mbaya.
Mwanaume au mwanamke anaweza kujua kama anatoa harufu au kinyume chake kwa kutumia tu mkono wake. Peleka kidole au vidole kwenye eneo husika, halafu ondoa kisha nusa. Majibu utayapata mwenyewe, hivyo chukua hatua kabla hujaaibika.
Mwili wako uwe safi kila eneo. Hakikisha mdomo hautoi harufu ya kuudhi, kwapa na mwili wote kwa jumla. Badili nguo, ni kosa kubwa kurudia nguo ya ndani siku mbili mfululizo. Wengine mpaka zinabadilika rangi, aibu iliyoje?
Hivyo basi, mwili ukiwa safi bila harufu mbaya wala manukato ya nyongeza, itafanya mwenzi wako aweze kukupata wewe kama wewe. Tamu yako hataweza kuvuna sehemu nyingine yoyote, atakuona wa kipekee na mtadumu.
Epuka leo yupo na wewe, halafu kesho akidondoka kwa mwingine moja kwa moja anakutoa thamani. Anakuona si lolote. Aibu ya aina hiyo isikufike. Anaweza asikwambie kwa kukuonea aibu lakini wewe uwe wa kwanza kujishtukia na kuchukua hatua zinazofaa.
HISIA ZAKO BAADA YA TENDO
Mwili ulikuongoza kufanya kile ambacho umetenda naye, umemamaliza haja zako, vipi hisia zako kwake? Unahisi faraja? Umejisikia vibaya? Jibu A au B litakupa picha ikiwa huyo uliyenaye yupo moyoni au ilikuwa fahari ya macho.
Anayependa, hata baada ya tendo na kuridhika bado atahisi faraja kuwa na mtu aliyetoka naye ulingoni. Asiyependa, anapomaliza haja zake huanza majuto na kujilaumu kwa kile ambacho alikitekeleza.
Baada ya tendo aligoma hata kukukumbatia? Anaweza kusingizia joto hata kama kiyoyozi kinacharaza chumbani au mvua yenye upepo mkali inavuma nje. Mtu wa hivyo usijiulize sana, haupo moyoni mwake ndiyo maana hakutaki tena kwa maana ameshatimiza haja zake.
Kwa mantiki hiyo, hata kama wewe unahisi hali ya kujilaumu au kutomhitaji tena baada ya kutimiza haja zako, ujue huyo si wa moyoni mwako. Yule wa kweli, utahitaji kumng’ang’ania hata usiku mzima kwa maana ndiye faraja yako. Zingatia!
No comments:
Post a Comment