
KUFUATIA kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa wenyeji Afrika Kusini, kocha wa timu ya taifa ya wanawake Twiga Stars, Charles Mkwasa amemlaumu mwamuzi aliyechezesha mpambano huo kwa madai ya kutow
atendea haki katika maamuzi yake ikiwemo kutoa penati isiyo halali na kuwanyima penati.
Twiga Stars na Afrika Kusini 'Banyana Banyana' zilimenyana katika pambano la ufunguzi la Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake lililofanyika jana kwenye dimba la uwanja wa Sinaba kwenye mji wa Daveyton nchini Afrika Kusini.
Katika mpambano huo wenyeji walitangulia kupata bao dakika ya 35 lililofungwa na Mamphasha Popela kabla ya winga wa kimataifa wa Tanzania Maimuna Saidi kusawazisha dakika nane baadaye na kufanya timu hizo ziende mapumziko zikiwa zimefungana bao 1-1.
Hali ilikuwa tofauti kipindi cha pili ambapo wenyeji waliuanza mchezo kwa kasi na kupeleka mashambulizi mfululizo katika lango la Twiga Stars na kumfanya mlinda mlango Fatuma Omari afanye kazi ya ziada ya kuokoa michomo ya washambuliaji wa Banyana Banyana.
Hata hivyo licha ya juhudi za ngome ya Twiga iliyokuwa chini ya nahodha Sophia Mwasikili kuhakikisha hakuna bao linalogusa nyavu zao tena ziligonga mwamba pale Makhabane Mamemello alipofunga bao la pili kwa njia ya mkwaju wa penati zikiwa zimebakia dakika 4 mpira kumalizika na kufanya hadi mwisho wenyeji watoke kifua mbele kwa ushindi wa magoli 2-1.
Akizungumza na kituo cha Televisheni cha Super Sport mara baada ya mchezo huo kumalizika, Mkwasa alisema kuwa mwamuzi huyo aliwanyima penati badala yake alimpa kadi nyekundu Mwanahamisi Shurua lakini pia hata ile aliyoitoa kwa wapinzani wao dakika ya 94 haikuwa sahihi.
Mkwasa aliongeza kuwa kitendo cha kutolewa nje kwa kadi nyekundu mchezaji wake Mwanahamisi Shurua hakikuwa sahihi kwa sababu yeye ndiye aliyechezewa rafu.
Hata hivyo Mkwasa alisema kuwa matokeo hayo hayamkatishi tamaa na sasa anajipanga kuhakikisha mechi zijazo ambazo ni dhidi ya Mali itakayochezwa Alhamisi na Nigeria itakayochezwa Jumapili anapata ushindi utakaomwezesha kusonga mbele.
Katika hatua nyingine kocha Mkwasa alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuijenga vema safu yake ya ulinzi hususani katika suala la kuweka mtego wa kuotea kwani vijana wake waliweza kufanya hivyo mara tisa dhidi ya mara mbili ya wapinzani wao.
Nchi nane za Afrika zinakwaana katika fainali hizo zinazochezwa kwa mara ya saba tangu kuanzishwa kwake ambapo zinatarajiwa kumalizika Novemba 14 na timu mbili zitakazofanya vizuri zitashiriki katika fainali za kombe la dunia zitakazofanyika nchini Ujerumani kuanzia Juni 26 mpaka Julai 17,2011.
Leo mashindano hayo yanaendelea, ambapo kutakuwa na mechi moja itakayowakutanisha mabingwa mara tano Nigeria watakaocheza na Mali, na hapo kesho mabingwa watetezi Guinea ya Ikweta watacheza dhidi ya Cameroon.
Wakati huo huo waandaaji wa mashindano hayo wamewaruhusu watu kuingia bure kushuhudia mechi, ingawa wanatakiwa kuchukua tiketi mapema kwa ajili ya utaratibu na usalama.
No comments:
Post a Comment