ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 21, 2010

Bei ya umeme juu mwakani


Mkurugenzi wa Ewura, Haruna Masebu
Nora Damian na Pilly Hashimu  
MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), imeruhusu Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 18.5 kuanzia Januari Mosi mwakani.  

Mkurugenzi wa Ewura, Haruna Masebu, aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa ongezeko hilo la bei ni chini ya mapendekezo ya Tanesco kwa asilimia 16.1.  Kwa mujibu wa Masebu, Tanesco ilipendekeza umeme upande bei kwa asilimia 34.6, lakini, baada ya uchambuzi wa kina, mamlaka imekubali kuruhusu nyongeza ya asilimia 18.5 kwenye nishati hiyo. 
"Shirika hilo liliomba kupandisha bei ya umeme kwa miaka mitatu mfulululizo na kwa viwango tofauti kuanzia 2011 hadi 2013, lakini, tumeona kuwa kuna hoja za msingi ambazo haziwezi kutufanya tukubali ombi hilo," alisema.

Masebu alibainisha kuwa Tanesco iliomba kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 34.6 mwaka 2011, asilimia 13.8 mwaka 2012 na asilimia 13.9 ifikapo mwaka 2013.  “Najua kwa uamuzi huu tutakuwa tumewaumiza watumiaji umeme na hatutakuwa tumewaridhisha Tanesco, lakini tumefanya hivyo kwa vigezo ili kufanya sekta iwe endelevu,”alisema Masebu.
  Mkurugenzi huyo wa Ewura alisema kuwa ili shirika hilo liweze kujiendesha, linahitaji zaidi ya Sh 691bilioni na uchambuzi walioufanya umeonyesha kuwa ongezeko hilo jipya la bei ya umeme, linaweza kukidhi hitaji hilo.  
Alisema  pia wameondoa mfumo wa shirika hilo uliokuwa unawapa nafuu wafanyakazi wake kulipia garama za umeme na kuanzia sasa wafanyakazi hao watalipa gharama hizo kama watumiaji wengine.  “Si sahihi wao kulipa pungufu, lazima walipe kama  watumiaji wengine na wasipolipa hata kwenye mahesabu itaonekana,”alisema.  Hata hivyo, alisema watumiaji wadogo wa umeme wasiozidisha kilowati 50 kwa mwezi, wataendelea kusaidiwa na watumiaji umeme mkubwa. 
Kwa mujibu wa Ewura, bei ya zamani kwa watumiaji hao wa umeme, ilikuwa Sh 49, lakini bei mpya itakuwa Sh60.  Kwa upande wa watumiaji umeme mkubwa zaidi bei ya zamani ilikuwa Sh 2,303 na Tanesco waliomba ipandishwe hadi Sh 3,109, lakini bei iliyokubaliwa ni Sh 2,738 kwa kilowati moja.

"Tumeamua kuruhusu ongezeko hilo na kama Tanesco wanadhani gharama zao za uendeshaji zinapanda kwa sababu ya ongezeko la gharama za mafuta ya kuzalishia umeme, wanaweza kujenga hoja na tukabadilisha bei ya mafuta pia," alisema Masebu.  Alisema ili kuhakikisha kwamba fedha zitakazopatikana hazitatumika vibaya, wameiagiza Tanesco kufungua akaunti maalumu kwa ajili ya kuboresha huduma ya umeme.

"Akaunti hizo zitakuwa zikikaguliwa na Ewura kila baada ya miezi mitatu na fedha zitakazokusanywa zitasaidia pia kununulia umeme mkubwa kwa wazalishaji wengine wa umeme," alisema Masebu na kuongeza:  “Tumewaagiza baada ya mwaka mmoja watueleze mabadiliko haya ya bei yameleta mafanikio gani katika kupunguza hasara.”  Masebu alisema pia kuwa wameiagiza Tanesco ndani ya siku 30 tangu kuanza kwa mabadiliko hayo ya bei, kuwapelekea mkataba ili kujiridhisha kama hautakuwa na madhara kwa watumiaji wa nishati hiyo.

Mkurugenzi wa umeme katika mamlaka hiyo, Pius Mbawala aliitaka Tanesco kuangalia mifumo ya manunuzi ya vifaa ili kupunguza garama za kuunganisha umeme kwani garama kubwa ni kikwazo mojawapo cha watu kuunganisha umeme.  Alisema pia wameliagiza shirika hilo hadi kufikia mwaka 2011 wawe wameunganisha wateja wapya zaidi ya 100,000, kuwa na idadi ya wafanyakazi inayotosheleza na kuhakikisha umeme unarudishwa mapema baada ya kukatika.

                                                                         CHANZO:MWANANCHI

No comments: