ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 21, 2010

Hata ningekuwa mimi ningemfukuza Tido

Tido Mhando.
Maadamu Dustan Tido Mhando niliyempa Ukurugenzi wa kuongoza Shirika la Utangazaji la Taifa ‘TBC’ linalotajwa kuwa mali ya umma ingawa ni langu kwa mantiki hai, amediriki kwenda kinyume na mapenzi yangu, hata mimi ningemuondoa kwenye nafasi yake.


Utangulizi wangu hapo juu utafsiriwe kuwa nasema kwa niaba ya serikali inayodaiwa kumuona Tido kama msaliti aliyekwenda kinyume na  macho ya wakubwa yaliyotazama safari nzima ya chombo hicho cha habari kwenye uchaguzi mkuu uliomalizika hivi karibuni.

Tido anazo kasoro ambazo serikali imeziona na kwa msingi huo imejiridhisha kuwa hafai kuendelea kuongoza, sina shaka hata ningekuwa mimi nisingekubali kuishi na mtu asiyenifurahisha. Katika hili sina neno zaidi ya kusema serikali imefanya vema kutetea matakwa yake.

Nasema hivyo kwa sababu najivika u-serikali na kuona ningemvumiliaje mkurugenzi huyo wa TBC kama kweli nilimuagiza asiwape nafasi wapinzani ‘kuuza sura’ zao kwenye runinga na kamwe sauti zao za kuikosoa serikali zisiwafikie akina Karumanzira huko shamba halafu yeye kwa ujeuri wake akaamua kufanya niliyomkataza?

Hata ningekuwa mimi ningemfukuza Tido, ila kwa haki ya Mungu ‘nisingemuua’ wakati akipiga kilele na kuwafanya wananchi wajitokeze kumuonea huruma, kama hali inavyojitokeza hivi sasa.

Tangu afukuzwe ‘kinyama’ Tido analia sambamba na wapambe wake akidai kuonewa, hoja ambayo inakuza simanzi ambayo ‘wauaji wake’ walikuwa na njia ya kuikwepa.

Naamini hakuna mwenye ujasiri wa kupita kando ya njia na kumwelezea Tido kama mtu aliyeshindwa na asiyestahili heshima kwa kazi aliyoifanya ndani ya TBC. Hii ina maana kwamba mema yake yanajulikana kwa jamii, isipokuwa ameshindwa tu kutii mambo ya wakubwa, hilo ni kosa la mkono wa kushoto linalomgharimu.

Binafsi sina sababu ya kumtetea mkurugenzi huyo juu ya makosa yake kwa vile najua kumtumikia mfalme kunahitaji roho ya unyenyekevu la sivyo ni rahisi kuandikiwa hati ya kifo na adhabu yake ikakufika hata usiku wa manane.

Nikisherehesha hili nataka Tido mwenyewe ajue toka ndani ya moyo wake kwamba ‘kiburi’ hakikustahili kwenye nyumba ya mfalme. Nikisema ujeuri simaanishi alichokifanya kilikuwa na makosa ya jumla, lakini alipaswa kujua waliomuweka walitaka awatumikie hivyo, alipoacha utumishi alipoteza sifa za kuishi kwa mfalme.

Binafsi ninapoyatazama ya Tido na serikali hayanitii ganzi, ila busara iliyotumika kumuondoa mkurugenzi huyo ndiyo iliyotibua akili yangu kiasi cha kujiuliza kulikuwa na sababu gani ya kumtimua ndani ya saa 48 wakati kanuni za kazi zinaelekeza muajiri kumtaarifu muajiriwa nia ya kusitisha mkataba miezi sita kabla?

Hivi ni kweli serikali kupitia watendaji wake walijiridhisha kabisa kwamba utaratibu huo waliotumia ulifaa kumuondoa mtu kama huyo kwenye nafasi yake?  Ikiwa waliona inafaa mbona hawajibu hoja zake, matokeo yake wanakuza ‘umbeya’ kwenye jamii kiasi watu kuamini kwamba Tido ameonewa.

Tuko karne ya ishirini na moja sasa, tujiulize ni sahihi uonevu kufanywa wazi wazi namna hii, tena kwenye chombo cha serikali kinachoongozwa kwa sheria?

Najiuliza kulikuwa na ugumu gani wa kumtathmini mkurugenzi huyo na kufikia maamuzi ya kiungwana ambayo yangeweza kutambua mchango wake hata kama ni mdogo alioutoa kufanikisha TBC kuwa walau na sura ya kisasa tofauti na zamani ambapo watu walikuwa wamejitenga nayo kwa kuita ni chombo cha habari cha wazee.

Inawezekana Tido alifanya makosa ndani ya miezi mitatu ya mwisho hivyo isingekuwa rahisi kumpa notisi ya miezi sita, lakini kwa nini asiongezewe mkataba hata wa miezi sita au mwaka mmoja ili tu utaratibu ufuatwe na yeye mwenyewe asijisikie vibaya.

Binafsi naamini hilo lingefanyika lisingezua mjadala uliopo mitaani hivi sasa na serikali ingebaki bila taka. Lakini kwa sababu ya upofu wa kusoma alama za nyakati, mzimu wa Dustas Tido Mhando anayedaiwa kuombwa na rais kuja kulifufua shirika hilo, utaishi milele na makovu yake yatabaki akisubiri kijiti tu kuumua majeraha mapya.

Nimeandika haya bila kuzingatia  tuhuma zisizothibitishwa dhidi ya  Tido, kwa sababu nataka kujiridhisha kwanza kama kweli amefanya ufisadi kupitia mradi wa Star Media,  amekiuka ushauri wa ajira kwa wafanyakazi wake pamoja na mambo yake binafsi yanayotajwa kuwa yalikuwa yanaivuruga ofisi huku lile la kipindi cha Mchakato Majimboni nikilitumia kujenga hoja. Leo nachochea tu!
CHANZO:GLOBAL PUBLISHERS

No comments: