ANGALIA LIVE NEWS
Wednesday, December 15, 2010
Buriani Dk. remmy ongala
Na Mwandishi Wetu
Gwiji wa muziki wa dansi nchini, hayati Ramazani Mtoro Ongala ‘Dk. Remmy’ (pichani) aliyefariki dunia juzi (Jumatatu) aliteseka kwa zaidi ya miaka minane.
The 5star Paper, Risasi Mchanganyiko linafunua historia ya ugonjwa wa Dk. Remmy ambaye afya yake ilianza kuleta utata tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Katika kipindi hicho, Dk. Remmy alishambuliwa na ugonjwa wa kisukari pamoja na shinikizo la damu, maradhi ambayo yalimsababishia kiharusi.
Uchunguzi wa Risasi Mchanganyiko umebaini kuwa tangu wakati huo, afya ya Dk. Remmy haikurejea katika hali yake ya kawaida.
Muda mfupi baada ya kupata nafuu alipokuwa amepooza viungo, midomo, mguu na mkono, staa huyo wa nyimbo za Kifo Hakina Huruma, Siku ya Kufa na Kilio cha Samaki alikata shauri la kuokoka.
Gazeti hili linazo data za kutosha kwamba wakati akijiuguza, alitumia mamilioni ya shilingi kabla ya mauti kumfika Desemba 13, 2010.
Vyanzo vyetu makini vilipasha kuwa, Dk. Remmy kwa zaidi ya miaka minane alikuwa anatumia dawa ambazo dozi yake kwa siku moja iligharimu wastani wa shilingi 40,000 au hata zaidi.
Vilisema kuwa kutokana na hesabu hiyo, kwa mwezi Dk. Remmy aliweza kutumia zaidi ya shilingi 1,200,000 kwa dawa peke yake, kiasi ambacho kinaleta jumla ya shilingi milioni 14.4 kwa mwaka.
Dk. Remmy, alizaliwa mwaka 1947, mkoani Kivu, Kongo ya Kinshasa ambayo sasa inaitwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Akiwa na umri wa miaka 17, alikuwa muimbaji na mpiga ngoma katika Bendi ya Vijana ya Bantu Success. Miaka miwili baadaye alijiunga na vikundi mbalimbali vya bendi za muziki akiwa mpiga gita.
Baadhi ya bendi alizofanyia kazi ni pamoja na Micky Jazz ya DRC (Zamani Zaire), Grand Mike Jazz ya Uganda.
Mwaka 1978 alihamia Tanzania na kujiunga na bendi ya mjomba wake, Orchestra Makassy ya jijini Dar es Salaam.
Mwaka 1981 alijiunga na Bendi ya Matimila, ikiwa na wanamuziki 18 na ikimilikiwa na mfanyabiashara mmoja. Baadaye alianzisha bendi yake ya Super Matimila na kuendeleza mtindo wa kutumia magita matatu, besi, ngoma na tarumbeta aina ya saksafoni.
Remmy Ongala alipiga muziki wake kwa mtindo wa Soukous, akitumia vionjo asili vya Kitanzania kabla ya kugeukia muziki wa Injili.
Katika moja ya nyimbo zake, Kifo Hakina Huruma, marehemu aliwahi kuimba kama utabiri kwamba atakwenda kufia Muhimbili. Japo kuwa hilo halikutimia lakini maiti yake ilipelekwa katika hospitali hiyo ya taifa.
Mpaka tunakwenda mitamboni Jumatatu, mipango ya mazishi ilikuwa ikisubiri watoto wake walio nje ya nchi na msiba ulikuwa nyumbani kwa marehemu, Sinza Kwaremi, jijini Dar es Salaam.
Mungu ailaze pema peponi roho ya marehemu. Amina.
CHANZO:GLOBAL PUBLISHERS
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
1 comment:
MUNGU amuweke mahali pema peponi na hawape familia yake nguvu baada ya kuondokewa na baba yao.
Post a Comment