ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 15, 2010

Tibaijuka awasha moto waliojenga ufukweni

Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka
Waandishi Wetu
SERIKALI imewatoa siku 30 kwa wananchi waliojenga nyumba kwenye maeneo ya fukwe ya Bahari ya Hindi kuzibomoa kabla ya kuanza kuchukua hatua, Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alisema jana.
Akizungumza katika ziara ya kukagua hali ya makazi na mipango miji  katika jijini la Dar es Salaam jana, Waziri Tibaijuka alisema viwanja vya serikali vilivyokuwa wazi haviruhusiwi kuwa makazi watu kwa kuwa viwanja hivyo ni kwa ajili ya michezo na bustani za kupumzika wananchi wa maeneo husika.

“Nasikitika kusikia kuwa wananchi wanaoishi hapa wamenunua maeneo haya. Hivi viwanja si vya watu ni vya serikali na kila aliyenunua anapaswa kubomoa na kurudisha kiwanja kwa wahusika,”
alisema Profesa Tibaijuka.
Alisema miongoni mwa viwanja hivyo ni eneo la wazi lililopo Ocean Road ambalo lilikuwa linamilikiwa na Shree Hindu Mandal, kiwanja namba 59 kitalu 1 kilichokuwa kinatumika kuchomea maiti mwaka 1952 mpaka 1967 na kuhamishiwa Kijitonyama na kutaka eneo hilo lilirudi mikononi mwa serikali.

Alisema katika hali ya udanganyifu Shree Hindu Mandal waliibuka na kudai mabadiliko ya matumizi ya kiwanja hicho na baadaye kupewa kibali na rais cha kutaka matumizi ya awali yafutwe na msajili alikifuta kwa nyaraka namba 131942 ya Septemba 2 mwaka huu kisha kuagiza manispaa ya Ilala ivunje ukuta uliopo.

Katika eneo jingine lililopo Palm Beach kiwanja namba 1006 ambalo lilikuwa la matumizi ya wazi mwaka 1975 kabla ya kubatilishwa kuwa eneo la mtu binafsi mwaka 2002 na mpaka sasa kinamilikiwa na mtu huyo.
“Mtu hawezi akajenga kwenye eneo la serikali kubwa kama hili wakati wananchi wanaoishi katika maeneo haya hawana sehemu ya kupumzikia wala sehemu ya watoto kucheza. Hii ni hujuma na wahusika wanapaswa kuchukuliwa hatua,” alisema Tibaijuka.
Alisema kiwanja namba 1072 kilichopo eneo la Upanga ambacho ni cha nyongeza, kilibuniwa pasipo kufuata utaratibu. Alisema kiwanja hicho kiko eneo la mikoko na hakijawai kupimwa rasmi.

“Kiwanja hiki hakikuwahi kupimwa kwa kuwa hakina sifa ya kuwa kiwanja kutokana na kutokuwa na barabara ya moja kwa moja, lakini mtu kanunua hapa na kuanza kujenga sehemu ambayo hamna kiwanja,” alisema Tibaijuka.

Tibaijuka alisema viwanja namba 1272,1273,1274 na 1275 vilivyo Kaole na ambavyo vimemilikishwa kwa kampuni ya Kahama Mining (1272 na 1273) na kampuni ya ujenzi ijulikanayo kama Tanzania Builiding Works (viwanja namba 1274 na 1275), vina kesi mahakamani kwa sababu vilitolewa katika eneo la wazi kinyume na taratibu ya mipango miji namba 8 ya mwaka 2007.
Katika kiwanja namba 615 eneo la Msasani Village ambacho kilikuwa na jengo la Afisa Mtendaji wa kata ya Msasani, ambalo lilishawahi kutangazwa katika gazeti la serikali, limevamiwa na mtu ambaye anadai ni kiwanja chake na ana barua.
Maeneo yaliyopo ufukwe wa Oysterbay kati ya Barabara za Sekou Toure na Ocean Road, Kinondoni Hananasif, Bonde la Msimbazi na la mpunga lililo Msasani yamepangwa kufanyiwa uboreshaji ikiwemo kujenga sehemu za mapumziko kwa ufukwe Oysterbay na uboreshaji wa nyumba zilizo maeneo yaliyobaki.

Mbunge wa Jimbo la Kawe, Halima Mdehe alisema anashukuru kwa utekelezaji wa urekebishaji wa viwanja hivyo vya wazi na kuwataka wananchi wawe makini wakati wa kununua viwanja ili kuepuka utapeli.
Hivi karibuni, Tibaijuka alisema vita yake ya kupambana na wavamizi wa viwanja itaanzia kwa wajanja waliojenga hoteli zisizofikia hadhi ya nyota tano na nyumba za makazi kwenye fukwe.

Tibaijuka, ambaye alikuwa mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi, ameshatangaza vita kali dhidi ya ufisadi kwenye viwanja na juzi alisisitiza nia hiyo wakati akifungua semina elekezi kwa vijana kutoka nchi za Afrika na Arabuni kuhusu namna ya kujenga nyumba bora kwa kutumia Mfuko wa Jumuiya ya Vijana wa Mijini.
Profesa Tibaijuka alisema kuwa mkakati huo umeshaanza kwa kuzitambua hoteli hizo na nyumba za vigogo zilizojengwa maeneo hayo.
Profesa Tibaijuka alisema mchakato wa kuvunja hoteli hizo utaendeshwa kulingana na vigezo vya kimataifa vya makazi na kwamba majengo yatakayosalimika ni yale yanayotoa huduma kwa umma na yanayolingana na thamani ya ardhi hiyo.
“Suala la kuyatwaa maeneo ya serikali yaliyokuwa yametengwa kwa ajili ya matumizi maalumu na baadaye kuporwa na wajanja halina mjadala, lililobaki ni kujipanga tu,” alisema Profesa Tibaijuka.

Alisema katika tasnia ya makazi, hakuna msamiati wa  maeneo ya wazi badala yake maeneo yote yametengewa shughuli na msamiati huo umebuniwa na wajanja kwa ajili ya kujichukuliwa maeneo kiholela.

Kwa Dar es salaam pekee, tume iliyoundwa mapema mwaka huu na mkuu wa zamani wa mkoa wa Dar es salaam, William Lukuvi ilibaini kuwa asilimia 80 ya maeneo ya wazi jijini Dar es salaam imevamiwa na wajanja.
Ripoti ya tume hiyo ilichunguza viwanja 154 na ilibaini kuwa maeneo 110 yaliyovamiwa yamo wilayani Kinondoni ambako kuna sehemu kubwa ya fukwe za mkoa wa Dar es salaam.
Wilaya ya Kinondoni ndio ina hoteli na nyumba nyingi zilizo kwenye fukwe ya Bahari ya Hindi na imekuwa ikiongoza kwa tuhuma za ufisadi.

Imeandikwa na Fredy Azzah, Salim Said, Aziza Masoud na Mwanaidi Abasi wa gazeti la Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

Hongera saaana Mama,sisi wananchi wanyonge tuna kuunga mkono kwenye vita hivi.Ufuko wa bahari ni kwa Watanzania woooote,Mwenyezi Mungu hakuwaumbia Mafisadi tu,kufurahia ufuko huo.