Mapenzi yanabeba sehemu kubwa ya maisha ya kila binadamu ndiyo maana tunayachambua. Inapendeza kushauriana na zaidi, inavutia tunapowekana sawa kwenye mambo muhimu yenye sura ya kujenga siyo kubomoa.
Mada hii ambayo nilianza nayo wiki iliyopita, ina maana kuwa hata kama mwenzi wako ana kasoro ya uchafu kiasi gani, wewe huna budi kuchukua hatua ili ufurahi ukiwa naye. Ukimkimbia unakosea, kwani hujui uendako utakuta nini.
Sehemu ya kwanza nilichambua aina mbalimbali za uchafu, itakuwaje wewe unamkimbia mwenzi wako kwasababu umeona anatoa harufu kali ya kwapa halafu unapokwenda unakutana na mwingine ambaye eneo lake nyeti linatisha kwa namna lilivyokosa huduma?
Mtu bora kwenye mapenzi ni yule anayeamua kuchukua tatizo la mwenzi wake kama lake kisha anaamua kulifanyia kazi ili kuliweka sawa. Utawakimbia wangapi? Kubadilisha wapenzi kila mara jamii haitakuelewa, itakuona mwenye matatizo.
Vinginevyo, utamkimbia mwenye kikwapa leo, kesho utamvaa anayetoa harufu kali eneo nyeti, naye utaona hafai, utamkimbilia anayesumbuliwa na uchafu wa mdomo, akizungumza unabana pua. Nakutaka umvumilie uliyenaye, halafu ushike ninachokupa.
UNAWEZAJE KUINJOI NA MWENYE HARUFU?
Ni rahisi na kama nilivyokueleza mapema kuwa ni vyema kubeba tatizo kama lako halafu uamue kuchukua hatua ya kulimaliza. Ni busara kutambua kiini chake kisha uanze kufanya kile kinachostahili.
Suluhisho la kila uchafu linategemea na njia zake ambazo nitazieleza. Hakuna kitu cha jumla. Pamoja na kila unachoweza kufanya, ni busara wewe mwenyewe uhakikishe upo nadhifu kila eneo muda wote kabla ya kushughulika na mwenzako.
Wanasema, “Yako duh! Ya wenzako midomo juu!” Kwamba unakuwa maridadi kutambua kasoro za mpenzi wako ilhali wewe mwenyewe unavumiliwa sana. Anza kujisafisha kwa kiwango kinachotakiwa, baada ya hapo tekeleza mengine.
NYWELE
Za kawaida mpeleke saluni, akirudi atakuwa yupo vizuri. Mjengee mazoea ya kwenda mara kwa mara, siku zikikaa muda mrefu bila kutengenezwa au kunyolewa, yeye mwenyewe ataona kero, hivyo atachukua hatua haraka.
Wanasema kawaida ni kama sheria. Utakapomfanya azoee utaratibu wa kuhudhuria saluni mara kwa mara, angalau kwa wiki mara moja, siku hata usipokuwepo atakwenda kwa miguu yake. Huoni hapo utakuwa umejenga?
Ni wazi kwamba kuna watu hawatunzi nywele zao za kichwa mpaka zinatoa harufu kali, lakini hiyo haikupi sababu ya kumkimbia. Muoneshe njia badala ya kulalamika kwa watu wa pembeni. Usimuaibishe, mhudumie kwa faida yako leo na kesho.
NYWELE ZA FARAGHA
Ni kipengele muhimu mno kwasababu huhifadhi uchafu ambao matokeo yake hutoa harufu inayotisha. Inahitaji umakini na busara katika kushughulikia tatizo hili ikiwa lipo kwa mwandani wako badala ya kukurupuka.
Huwezi kumbeba mpaka saluni akanyolewe na mtu mwingine. ‘Shame on you!’ Ni wewe unayepaswa kuhusika kikamilifu kuhakikisha mwenzi wako anakuwa safi ili uweze kufurahi unapokuwa naye muda wote.
Angalizo; Hutakiwi kumtolea lugha za kumnyanyapaa, kama vile kumsema kwamba yeye ni mchafu na maneno mengine kama hayo. Unaweza kuwa kimya, ukahusika naye kwa vitendo na baada ya muda utaona matunda ya uvumilivu wako.
Wahuni au watu wasio na adabu kwa wenzi wao wanaweza kuthubutu kutoa lugha chafu kwa wenzi wao, kama vile kuwaambia ‘wananuka’, lakini igonge kwenye kichwa chako kwa neno kavu kwamba ‘unanuka’, halitamsaidia, litambomoa na atakuchukia.
Ukifanya kwa vitendo zaidi, huku ukitumia lugha laini utafaulu vizuri kumbadilisha. Atakuona wewe ni mwalimu wake kwenye mapenzi, atakuheshimu kwa maana unaujua vyema mwili wake, atakupenda sana.
UNAZIFANYAJE NYWELE HIZO?
Upo chumbani na mwenzi wako, bila shaka unahitaji huduma. Mwili umesisimka na akili yako inakwambia kwa wakati huo, huna kingine kinachoweza kutuliza ‘Wazaramo’ wa kichwani kwako, isipokuwa ni tunda la katikati.
Katika kipindi cha ‘romansi’ unagundua kuwa nywele za faragha za mtu wako zimesimama kama kiduku. Bila shaka unanyong’onyea, hujafurahishwa kwa namna ulivyomkuta, lakini hiyo isikurudishe nyuma. Una nafasi ya kufurahia zaidi mapenzi yako.
Kuhusu za kwapa inategemea uvumilivu wako lakini zile nyeti ni tatizo endapo utaamua kufumba macho na kuhusika naye hivyo hivyo. ‘Kudili’ na mtu mwenye nywele nyingi za huko inaweza kukusababishia michubuko na maumivu makali.
Kuna athari ya maradhi ya ngono (STD) na Ukimwi. Hata kama utatumia kondomu lakini wingi wa nywele zake za faragha zitakuchubua na kukusababishia maambukizi kwa njia ya damu au jasho kwasababu hazitakosekana uwapo mchezoni.
Kawaida mtu anapokuwa na nywele nyingi na harufu huwa kali kwasababu zina kawaida ya kuhifadhi jasho lenye mafuta, kwahiyo jukumu lako namba moja ni kuzinyoa ili kuondosha yote.
Kuna njia ya kuzinyoa ambayo itafanya iwe sehemu mojawapo ya ‘romansi’, yaani wakati unamfanyia usafi wa nywele hizo, yeye anakuwa anaburudika na kusogeza hisia zake karibu, ukimuona anavyohangaika bila shaka nawe utavutika. Mapenzi mazuri sana.
Tuendelee wiki ijayo...
No comments:
Post a Comment