ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 15, 2010

Pacha wawili wafariki dunia

WATOTO wawili pacha kati ya pacha watano waliozaliwa juzi wilayani Kahama katika Mkoa wa Shinyanga, wamefariki dunia.

Pacha hao walihamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza kwa ajili ya kuchunguzwa afya zao na ya mama yao mzazi. 


Wauguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando walithibitisha jana alasiri kufariki kwa watoto hao ambao walizaliwa salama alfajiri ya Jumapili, na mkazi wa Kijiji cha Bulungwa wilayani Kahama, Shija Maige (33). 

Kati ya watoto hao, wawili walikuwa ni wa kiume na watatu ni wa kike, na wengi wao walizaliwa wakiwa na uzito mdogo tofauti na ule unaokubaliwa kitaalamu. 

Watoto hao walikuwa na uzito wa kilo 1.7, 1.45, wawili kilo 1.4 na wa mwisho kilo 1.2. 
Akizungumza na gazeti hili jana kwenye wadi ya uangalizi maalumu wa watoto wachanga, Ofisa Muuguzi wa zamu, Deoniza Adrian alisema watoto waliofariki ni wa kwanza kuzaliwa aliyefariki jana saa moja asubuhi baada ya kuwasili hapo kwa uchunguzi zaidi wa afya, wakitokea Hospitali ya Wilaya ya Kahama. 

“Wa kwanza alifariki muda mfupi tu mara baada ya watoto hao kufikishwa hapa, huyu ni mtoto wa kwanza kuzaliwa na wa pili alifariki jana mchana na huyu ni mtoto wa mwisho kuzaliwa kati ya watoto mapacha waliozaliwa,” alisema Adrian na kuongeza kuwa hali ya watoto watatu waliobakia inaendelea vizuri. 

Gazeti hili jana liliwashuhudia watoto hao hospitalini wakiwa wamepangwa kwenye kitanda maalumu kwa kufuata umri wao wa kuzaliwa na walionekana kuwa katika hali nzuri na mmoja alikuwa akilia wakati huo. 

“Umewaona ni watoto wazuri sana na imani yetu ni kuwa watoto hawa wataendelea vizuri na kupata afya nzuri…hawakuwa na matatizo makubwa, wale nadhani walifariki kutokana na mama yao kujifungulia nyumbani na inawezekana walizaliwa wakiwa na matatizo,” aliongeza Adrian. 

Mtaalamu wa Magonjwa ya Watoto, Dk. Akwila Temu alisema mjamzito kujifungua pacha watano kwa mpigo inaweza kusababishwa na hali ya maumbile ya uzazi wa mama ambaye wakati anaingia katika hedhi, inawezekana yaliingia mayai matano kwa pamoja na kurutubishwa na yai la mwanamume na hivyo kujifungua idadi hiyo ya watoto. 

“Sababu nyingine wakati mwingine kwa akinamama ambao huwa wamekaa muda mrefu bila ya kujifungua na siku akipewa dawa ya kienyeji, kuna uwezekano wa kujifungua watoto mapacha zaidi ya watatu,” alisema Dk. Temu. 

Akizungumza katika Wadi Namba C.4 alikolazwa, mama wa watoto hao, Shija alisema hali yake inaendelea vizuri na kwamba kilichomsikitisha licha ya kujifungulia nyumbani salama salimini watoto pacha watano, ni kuondokewa na watoto wake wawili, aliotamani kuwalea na kuwatunza. 

Kabla ya kujifungua mapacha hao watano, alisema huo ulikuwa ni uzao wake wa 10 na kwamba alikuwa na watoto wanane walio hai na kwa sasa atakuwa na jumla ya watoto 11. 

“Nilijifungua salama na baada ya kujifungua, nilichukua nguo zangu nikazifua ndipo baadaye nilianza kuhisi maumivu,” alisema Shija ambaye alionekana ni mwanamke mtulivu licha ya kufiwa na watoto hao. 

Aliwatambulisha watoto waliofariki kuwa ni Kurwa Charles ambaye ni wa kiume na Kamuli Charles ambaye ni wa kike na kwa sasa mapacha walio hai ni watoto wa kike wawili na wa kiume mmoja. 

Muuguzi wa wadi ya kina mama alimolazwa Shija, Joyce Mahendeka alisema hali ya mzazi huyo ilikuwa inaendelea vizuri na kwamba haikuwa kama ambavyo alipokelewa juzi na kulazwa hospitalini hapo. 

“Kwa jinsi tulivyompokea jana na sasa ana nafuu kubwa sivyo kama ambavyo alivyokuja…inaonekana mara baada ya kujifungua, alitokwa na damu nyingi, tumemuongeza chupa moja ya damu na kwa sasa anaendelea vizuri na uvimbe wa miguu aliokuwa nao umepungua kabisa,” alisema Mahendeka. 

Muuguzi huyo alitoa mwito kwa wajawazito wawe wanahudhuria kliniki na waachane na tabia ya kujifungulia nyumbani kwani wanaweza kupata madhara na kusababisha kifo. 

Wakati huo huo, Mwandishi Wetu, Joachim Nyambo kutoka Mbeya, anaripoti kuwa mtoto wa ajabu asiyekuwa na jicho moja la kushoto, pua na pia mdomo wake wa juu umegawanyika, amezaliwa katika Hospitali ya Wazazi ya Meta iliyopo jijini humo. 

Kuzaliwa kwa mtoto huyo kumekuwa gumzo, huku mtoto huyo akilazimika kupumua kwa kutumia mdomo, lakini hawezi kula hivyo mama yake kulazimika kukamua maziwa katika kikombe kisha kumnywesha. 

Mama wa mtoto huyo, Hilda Mavazi, mkazi wa Mbata jijini Mbeya akizungumza katika wadi ya wazazi alisema alijifungua salama Desemba 11, mwaka huu, lakini alishangaa kuona mwanawe akiwa na upungufu wa viungo. 

“Hawezi kunyonya ziwa mwenyewe, hivyo nalazimika kumkamulia maziwa kwenye kikombe na kumywesha,” alisema Hilda na kuongeza kuwa baada ya kujifungua, ameambiwa na madaktari ampeleke Hospitali ya Rufaa kwa ajili ya upasuaji, lakini hajui gharama zitakazohitajika. 

Muuguzi Msajili wa Kitengo cha Wazazi, Mtawa Enisa Kabage alisema mtoto huyo alizaliwa katika mazingira ya kawaida japo maumbile yake si ya kawaida. Alizaliwa akiwa na kilogramu 2.7.
                                                              CHANZO HABARI LEO

No comments: