WAKATI kilio cha kutaka katiba mpya kikizidi kushika kupamba moto, serikali imeamua kutoa tamko kuhusu suala hilo leo wakati Waziri Mkuu Mizengo Pinda atakapokutana na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es salaam.
Tangu Chadema ilipoamua kususia matokeo ya uchaguzi wa rais kwa kutoka kwenye ukumbi wa Bunge wakati Rais Jakaya Kikwete akianza kuhutubia na kufufua kilio cha kuandikwa upya kwa katiba, watu wa kada mbalimbali wakiongozwa na majaji wameibuka na kueleza umuhimu wa kuondokana na katiba ya sasa.
Miongoni mwa watu hao ni mawaziri wakuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba na Frederick Sumaye, Jaji Agustino Ramadhan, Jaji Robert Kisanga, Jaji Amir Manento, Jaji Mark Bomani, mhadhiri wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Issa Shivji na Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa.
Miongoni mwa watu hao ni mawaziri wakuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba na Frederick Sumaye, Jaji Agustino Ramadhan, Jaji Robert Kisanga, Jaji Amir Manento, Jaji Mark Bomani, mhadhiri wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Issa Shivji na Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa.
Katika mkutano huo wa wahariri ambao taarifa ya mwandishi wa waziri mkuu ameelezea kuwa ni wa kuwajulisha na kuufahamisha umma juu ya utekelezaji wa masuala mbalimbali ya shughuli za serikali katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Pinda atazungumzia suala hilo nyeti.
"Kwa vile kuna maoni mbalimbali yanayotolewa kuhusu katiba ya Jamhuri ya Muungano, Waziri Mkuu anatarajia kutoa maelezo kuhusu suala hilo," inaeleza taarifa hiyo kutoka ofisi ya Waziri mkuu iliyosainiwa na mwandishi wa habari wa waziri mkuu, Said Nguba.
"Kama kawaida yake na kadri anapopata nafasi, Mhe Pinda hukutana na wahariri wa vyombo vya habari kuwajulisha kwa ajili ya kuufahamisha umma masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa shughuli za serikali na pia wahariri kupata nafasi ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali," inasema taarifa hiyo.
Waziri Pinda, ambaye anashikilia wadhifa huo tangu mwaka 2008, anazungumza na wahariri kwa mara ya kwanza tangu serikali ya awamu ya nne irejeshwe madarakani.
Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani alishawahi kueleza kuwa suala la kuandikwa kwa katiba mpya haliwezekani kwa kuwa serikali haina fedha na kwamba itaendelea na utaratibu wake wa kuweka viraka pale inapohitajika.
Kauli kama hiyo pia ilitolewa na katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba na katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, John Chiligati ambao walikwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa Chadema inataka kusababisha vurugu kwa kudai katiba mpya.
Ikifafanua kuhusu msimamo wake, Chadema ilisema kuwa iko tayari kukaa mezani na serikali kuzungumzia katiba mpya na katika mchakato huo mawazo na fikra kama za Chiligati na Makamba yasizingatiwe.
Juzi, Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa alitahadharisha kuwa iwapo katiba haitaandikwa upya, nchi inaweza kupata madhara makubwa na akabainisha kasoro kadhaa zilizomo kwenye katiba ya sasa, ikiwemo ya kumpa rais madaraka makubwa.
“Hata kama tuko katika taasisi za serikali, lazima tueleze ukweli. Mnaona wenyewe jinsi Bunge lilivyo na kigugumizi cha kuundwa kwa katiba mpya,” alisema Tendwa.
Wakati mjadala huo ukipamba moto, Jmuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) jana ilitoa tamko lake ikitaka katiba mpya ipatikane haraka iwezekanavyo, lakini baada ya utafiti wa kina kufanyika.
Viongozi wa makanisa yanayounda umoja huo waliwaambia waandishi wa habari jana kuwa uundwaji huo wa katiba mpya ni lazima uzingatie sauti na utashi wa watu kwa kuzingatia nyakati na mazingira ya nchi.
Viongozi hao pia waliungana na kilio cha kutaka tume huru ya uchaguzi, wakipendekeza kuwa iundwe kwa kushirikisha vyama vyote vya siasa, wasomi, watafiti na wadau mbalimbali.
Akizungumzia uchaguzi mkuu uliopita katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es salaam jana, mwenyekiti wa CCT, Askofu Peter Kitula alisema wanaamini kuwa elimu bora na ya kutosha kwa wapiga kura na wananchi kwa ujumla pamoja na kuwa na taratibu huru na wazi zitakazowakilisha ari za vyama, makundi yote ya kijamii na zitakazoboresha mahusiano mema katika jamii ndiyo njia pekee ya kuondokana na kero na machungu ambayo yameonekana katika uchaguzi wa mwaka huu.
"Vinginevyo tumeanza kuhofia kuwa uchaguzi, unaopaswa kuwa huru; haki na amani, sasa unatishiwa kuwa wa vurugu, uvunjifu wa amani, vitisho na kubezana, matusi na kejeli zisizojenga nchi," alisema Kitula.
Kuhusu suala la udini kuhusishwa na siasa, Askofu Kitula alisema kuhusisha dini katika siasa ni kosa, kadhalika kuhusisha siasa katika dini ni kosa hivyo nchi na vyama vya siasa havitakiwi kutangaza dini yoyote au maslahi yake.
Askofu Kitula alisema kuwa viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa serikali na jamii waelewe kwamba wanaongoza watu wote hata wasio wa itikadi zao au dini zao, hivyo waepuke kutafuta malengo yao kwa kupitia vyombo vya dini.
"Jambo hili liwekwe bayana katika katiba mpya na sheria nyingine za nchi. Tunaangaliza bayana kuwa jambo hili lisipofanyika, kuna hatari kubwa zaidi ya kutokea mgawanyiko mkubwa na hatarishi wa kidini kwa Watanzania katika uchaguzi wa mwaka 2015," alisema Kitula.
Viongozi hao pia wameeleza kusikitishwa na kejeli, matusi, vitisho na mauaji yaliyotokea kipindi cha kampeni na kutaka hali hiyo ikemewe ili ilisije ikajitokeza katika uchaguzi ujao.
"JWTZ waliota vitisho, mgombea mmoja wa Chadema alimtukana mgombea urais wa CCM jambo ambalo lilishtua na kusikitisha taifa zima," alisema.
Askofu Kitula alisema kuwa CCT inatahadharisha kuwa tabia za jazba, munkari na kulipa kisasi au kufanyia mzaha au kejeli maneno ya imani za kidini kwa faida ya mambo ya kisiasa zikiendelea, zitakuza hisia za mafarakano na kuathiri umoja wa kitaifa.
Akizungumzia vyombo vya ulinzi na usalama, Askofu Kitula alisema kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vibaki kuwa vyombo vya usalama kwa wananchi na vyama vya siasa vyote vitekeleze wajibu wake pasipo upendeleo wala kutumia vitisho.
Katika hatua nyingine, wasomi na wanasiasa wamesema mambo yanayoendelea nchini Kenya kwa sasa yanaweza kutokea na Tanzania iwapo katiba haitafanyiwa marekebisho.
Mapema wiki hii, mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Luis Moreno Ocampo alitaja majina ya viogogo wanaotuhumiwa kuhusika kwenye mauaji yaliyotokea baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi.
Zaidi ya watu 800 walipoteza maisha katika vurugu hizo baada ya Mwai Kibaki kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais katika mazingira ya kutatanisha.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, wananchi hao walisema bila katiba inayokidhi haja na matakwa ya wananchi, Tanzania imsubiri Ocampo baada ya uchaguzi wa mwaka 2015.
"Chimbuko la yote haya ni ukosefu wa katiba yenye misingi mizuri ya kidemokrasia iliyosababisha uchaguzi mbovu, usimamizi, utangazaji na uchakachuaji wa matokeo ya uchaguzi kuvurugwa," alisema mwenyekiti wa CUF, Ibrahim Lipumba.
"Inafurahisha kuona sasa hakuna misamaha kwa wanasiasa wanaosababisha mauaji ya raia kwa sababu hata wakikimbia na kujaribu kulindana, kina Ocampo watawatafuta na kuwafikisha katika vyombo vya kisheria.
"Hivyo kama hatukujipanga na kuandika katiba mpya 2015 ni zamu yetu.”
Aliongeza kusema: “Ni vyema tukaangalia na kufanya mambo haya mapema wakati tuko katika amani na utulivu ili tupate katiba mpya na kuepukana na vurugu za baada ya uchaguzi.”
Mkuu wa Idara ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema sheria inatakiwa kuchukua mkondo wake.
“Kenya na mahakama ya kimataifa inabidi zishirikiane kujua ukweli na kama itabainika basi sheria ichukue mkondo wake,” alisema Dk Bana.
Dk Bana alisema ni wazi kuwa vurugu hizo zilitokana na wananchi kutokuwa na imani na Tume ya Uchaguzi na kuongeza kuwa inawezekana pia vurugu hizo zilisababishwa na misingi na kanuni ya katiba ya nchi hiyo.
“Lakini pamoja na hayo hili suala inatakiwa waachiwe wakenya wenyewe," alisema Dk Bana
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila alisema kilichotokea Kenya ni fundisho kwa viongozi wa Afrika, hivyo nchi za Afrika zinapaswa kuwa na mfumo wa uchaguzi ambao ni huru na unao tenda haki kwa pande zote.
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila alisema kilichotokea Kenya ni fundisho kwa viongozi wa Afrika, hivyo nchi za Afrika zinapaswa kuwa na mfumo wa uchaguzi ambao ni huru na unao tenda haki kwa pande zote.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment