Mabingwa wa Afrika TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamefuzu kucheza fainali ya kuwania kombe la klabu bingwa duniani, baada ya kuwalaza mabingwa wa Amerika ya kusini- Internacional kutoka Brazil mabao 2-0 mjini Abu Dhabi.
TP Mazembe inakuwa klabu ya kwanza barani Afrika kufikia hatua ya fainali ya Kombe la Dunia,
na inasubiri kucheza fainali dhidi ya mshindi kati ya mabingwa wa ulaya Inter Milan ya Italia na mabingwa wa Asia, Seongnam IIhwa kutoka Korea Kusini, ambazo zinachuana Jumatano katika nusu fainali ya pili.Bao la kwanza la TP Mazembe lilifungwa katika dakika ya 53 na mshambuliaji Mulota Kabangu, naye Dioko Kaluyituka akafunga la pili katika dakika ya 85.
Internacional walipata nafasi nyingi katika kipindi cha kwanza lakini ngome imara ya ulinzi ya TP Mazembe ikayakomesha mashambulizi yote, na pia mlinda mlango Muteba Kidiaba akaokoa mikwaju mingi.
Fainali itachezwa siku ya Jumamosi tarehe 18.
No comments:
Post a Comment