ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 10, 2010

Stars chinja Waganda

Kikosi cha Kilimanjaro Stars.
Na Ezekiel Kitula
KOCHA Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Jan Poulsen amesema ana imani kubwa na mabadiliko katika kikosi chake yatasaidia kuichinja Uganda, The Cranes na kusonga hadi fainali.


Stars inakutana na The Cranes leo kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam katika mechi ya nusu fainali ya michuano ya Chalenji.

Stars imefika hatua hiyo kwa kuing’oa Rwanda, Amavubi kwa bao 1-0 huku Uganda ikiichapa Zanzibar kwa penaliti 4-3.

“Kweli tuna upungufu, lakini tumekuwa tukibadilika na ndiyo maana nilisema ninahitaji muda. Tukiendelea hivi, sina wasiwasi kuwa tutaenda fainali,” alisema Poulsen.

Kocha Mkuu wa Uganda, Bobby Williams amejigamba kuwa wana uhakika wa kufika fainali lakini akasisitiza hawataibeza Stars.

“Unaona ni timu yenye mabadiliko makubwa, wachezaji wake wanabadilika kutokana na michuano inavyokwenda. Maana yake tutatakiwa kuwa makini zaidi,” alisema.

Wakati Stars itawakosa, viungo wake wawili, Uganda itakuwa na furaha kwa nahodha Andy Mwesigwa kurejea baada ya kuikosa mechi ya robo fainali dhidi ya Zanzibar kutokana na kuwa na kadi mbili za njano.

Viungo wawili itakaowakosa Stars ni Mohammed Banka na Henry Joseph Shindika ambao ni majeruhi.

Banka alicheza dakika chache katika mchezo wa robo fainali dhidi ya Rwanda ambapo aliumia akatoka na nafasi yake ikachukuliwa na Jabir Aziz .

Daktari wa Kilimanjaro Stars, Mwanandi Mwankemwa alisema jana kuwa , wachezaji hao wawili hawatakuwa katika kikosi kitakachoivaa Uganda leo.

“Banka anasumbuliwa na nyonga. Na tatizo hili kwa kweli huwa linatusumbua sana sisi madaktari.

Tumeshampatia matibabu ya awali na leo (jana) tutampeleka kwenye kliniki ya AAR kwa ajili ya kupata matibabu zaidi. Siwezi kusema atarejea lini, lakini kwa ufupi hatacheza mechi ya kesho (leo). Anahitaji muda wa kupumzika.

“Henry Joseph yeye anasumbuliwa na malaria. Tulimfanyia vipimo jana (juzi) na tutaona kweli ana tatizo hilo. Kwa kawaida matibabu ya ugonjwa huo huchukua kama siku tatu hivi,” alisema Mwankemwa.

Huenda Poulsen raia wa Denmark, akawatumia Salum Machaku na Jabir Aziz kuziba nafasi za wakongwe hao.

Kocha huyo amekuwa akitumia viungo tu katika kikosi chake kwa mechi mbili mfululizo lakini juzi, alimrudisha John Boko ambaye alionyesha uwezo mzuri na ushindani.
                    CHANZO:GLOBAL PUBLISHERS

No comments: