LEO tunaadhimisha miaka 49 ya Uhuru tukiwa na jambo moja kubwa la kujivunia ambalo ni umoja wa taifa letu. Ingawa umoja huu umekabiliwa na mawimbi na misukosuko ya kila aina, bado Watanzania tumeweza kuulinda umoja wetu kwa kucha na meno. Umoja wetu ulisukwa katika misingi ya kujenga taifa moja lisilokuwa na matabaka, ukabila wala udini, lakini kidogo kidogo misingi hiyo ikaanza kukiukwa, kwa kuanzia na kuwapo kwa matabaka ya walio nacho na wasio nacho. Pengo baina ya masikini na matajiri likawa kubwa, hapo ndipo watu wakaanza kuhoji kulikoni? Ule ukabila na umajimbo uliokuwa ukipigwa vita mara baada ya uhuru, sasa unaibuka kwa kasi kubwa. Udini nao umeanza kujenga mizizi yake taratibu.
Mwaka 1961 tulipopata Uhuru, tuliweka vipaumbele vyetu, kwamba tunataka kutokomeza umasikini, ujinga na maradhi. Tumejitahidi kiasi fulani lakini si kwa kiasi cha kuridhisha. Umasikini bado ni tatizo kubwa, kiwango chetu cha elimu kinashuka siku hadi siku na mapambano dhidi ya maradhi yanazidi kuwa magumu. Na hata pale tulipoweka malengo ya millennia ya kupunguza umasikini ifikapo mwaka 2015 inaonyesha kwamba kwetu itakuwa ni ndoto kufikia dhamira hiyo.
Haya yote tunaweza kusema kwamba yanahatarisha uzalendo wetu, kwa sababu watu hawafikirii tena maslahi ya nchi bali wanafikiria wapi watapata fedha za kuwapeleka watoto wao kwenye shule inayotoa elimu bora na wala si zile zinazotoa bora elimu.
Watu sasa wanafikiria ni wapi watakwenda kupata matibabu bora na wala si kule ambako watakwenda kumuona tabibu na baada ya kujulikana maradhi yao waambiwe dawa hakuna. Hata pale ambapo huduma zote zimekamilika, bado mama mjamzito ataambiwa kuwa atoe kitu kidogo kama anataka kuhudumiwa, kinyume cha hivyo ataachiwa kitanda ajifungue peke yake bila msaada.
Hali ya maisha kwa ujumla badala ya kuboreka kwa walio wengi inazidi kudidimia. Watu hawana uhakika wa kupata angalao kijio cha siku moja. Kima cha chini cha mshahara kimebakia katika kiwango cha kumdhalilisha mfanyakazi, kwani hakimtoshelezi kumudu hata huduma za msingi kama chakula, malazi, matibabu, usafiri, maji salama au elimu bora kwa watoto wake. Hesabu za gharama zote hizi na nyinginezo zikijumlishwa kwa kweli tutagundua kwamba mtu huyu anaishi kwa miujiza. Hiyo ndiyo jaza ya miaka 49 ya Uhuru wetu.
Serikali imesema kwamba kauli mbiu yetu katika kusheherekea Miaka 49 ya Uhuru ni ‘Tudumishe Uzalendo’. Lakini katika hali kama hiyo, uzalendo unaweza kupatikana kweli? Uzalendo unatokana na mtu kuwa na matumaini ya kupata maendeleo na amani. Mtu ataipenda nchi yake kama nchi hiyo nayo inampenda, kwa maana ya kuweka mazingira yatakayomuwezesha kujiendeleza na kuendesha maisha yake kwa salama na amani. Uzalendo unachochewa na viongozi wanaoendesha nchi kwa uadilifu, kwa maana ya kuzingatia maadili ya uongozi, siyo kwa kujikita na kubobea katika vitendo vya rushwa na ufisadi.
Miaka 49 si haba na wala hatustahili tena kuitwa taifa changa, kwa sababu huo ni umri wa mtu mzima ambaye tayari pengine ameshaanza kupata wajukuu. Huu ni wakati wa kutafakari tulikotoka, tulipo na tuendako kama taifa. Je, haya tuliyonayo sasa ndiyo yale tuliyoyapigania?
Kwa maneno mengine, ile ndoto yetu ya Uhuru na Maendeleo tumeitimiza kwa kiasi gani? Ni wapi tulipokwenda mrama na ni vipi tujikwamue ili tupige hatua mbele? Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa wakati wenzetu wanatembea, sisi tunapaswa tukimbie. Je, zile mbio tulizohamasishwa kukimbia zimekwama kwenye ukingo gani?
Wakati tukiwapongeza Watanzania kwa kutimiza miaka 49 ya Uhuru,tunadhani itakuwa vyema iwapo tutatafakari kwa pamoja wapi uhuru wetu ulipokwama ili tutafute mbinu za kujikwamua.

No comments:
Post a Comment