Watu wasiopungua ishirini wameripotiwa kuuwawa nchini Ivory Coast huku wanajeshi walio watiifu kwa marais wawili wapinzani nchini humo, wakikabiliana vikali kwa risasi katika barabara za mji wa Abidjan na hivyo kuzua hofu kwamba taifa hilo huenda likatumbukia tena katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Msemaji wa rais aliyekwamilia madarakani Laurent Gbagbo Amesema walioaga dunia ni waandamanaji kumi na maafisa kumi wa kijeshi.
Tume ya uchaguzi ilimtangaza bwana Alassane Ouattara kuwa mshindi wa uchaguzi wa mwezi uliopita uliozingirwa na utata, lakini rais wa sasa Laurent Gbagbo amekataa kuondoka madarakani.
Vifo vya wengi waliouwawa vilitokea wakati wanajeshi watiifu kwa bwana Gbagbo walipowazuia wafuasi wa bwana Ouattara kuchukuwa uthibiti wa kituo cha televisheni ya kitaifa.
Waandamanaji hao wamesema watajaribu tena kukiteka kituo hicho hivi leo Ijuma.
Kumekuwa pia na makabiliano makali tika mji wa kati wa Tiebissou. Baraza la usalama la umoja wa mataifa limeonya kuwa yeyote atakayewashambulia raia atakabiliwa na mkono wa sheria za kimataifa.
No comments:
Post a Comment