ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 10, 2011

Baada ya kumtia mimba bintie,Aua wanae watatu

Mkulima wa kijiji cha Makere wilayani Kasulu, Filbert Kafonogo, amewaua watoto wake watatu kwa kuwanyonga na kisha kujinyonga yeye mwenyewe kwa kamba kwenye mti, baada
ya kutuhumiwa kumpa ujauzito mmoja wa binti zake.

Taarifa iliyopatikana kutoka kijijini hapo jana na kuthibitishwa na familia ya marehemu, zinaeleza kuwa maiti hao waligundulika juzi kijijini hapo.

Kwa mujibu wa habari hizo, Filbert anadaiwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mtoto wake mkubwa wa kike ambaye jina halikupatikana na katika uhusiano huo msichana huyo alibeba ujauzito.

Inadaiwa baada ya msichana huyo kubeba ujauzito na mke wa Filbert, Mandebe Mahungi kupata habari za uhusiano wa kimapenzi uliopo kati ya mzee huyo na binti yake, kulianza ugomvi wa kutaka kujua kama ujauzito wa binti huyo ni wa baba yake.

Taarifa hizo zinasema haikuwa rahisi kwa mtoto huyo kueleza moja kwa moja kama kweli ujauzito huo ni wa baba yake au wa mtu mwingine, kwa kuwa Filbert alimtishia mtoto wake
kwamba akimtaja kwa mke wake, atamuua.

Ugomvi huo baina ya wanandoa hao uliendelea kwa muda mrefu na ndipo wakati wa sikukuu ya mwaka mpya, mke wa Filbert alikimbilia kwa wazazi wake katika kijiji cha Kitagata wilayani Kasulu kusalimisha maisha yake baada ya kuona amani ndani ya nyumba ina utata.

Inadaiwa Filbert alipogundua kwamba siri yake imeenea sehemu kubwa anayoishi, ndipo alipoamua kuchukua uamuzi wa kuwaua watoto aliokuwa akiishi nao na kujitoa uhai yeye binafsi.

Phares alisema kuwa asubuhi ya juzi, Filbert aliwachukua watoto wake na kutoka nao lakini alipofika porini aliwanyonga watoto mapacha kwa kuwakaba shingo.

Alisema kuwa baada ya kufanya kitendo hicho, aliondoka na mtoto wake wa kiume Obedi ambaye inadaiwa alimnywesha sumu kutokana na mazingira ya ilipokutwa maiti ya mtoto huyo ambaye aliangukia kilometa moja kutoka mahala alipojinyonga baba yake.

Miili miwili ya watoto hao na wa baba yao ilikutwa juzi hiyo na baba wa marehemu Mzee Kafonogo ambaye alitoa taarifa kwa uongozi wa kijiji na polisi walifika eneo la tukio.

Mwili wa mtoto Obed uliokotwa jana asubuhi ukiwa umeharibika vibaya hali iliyowafanya ndugu wa marehemu na uongozi wa kijiji waamue azikwe mahali alipokutwa kutokana na mwili huo kushindikana kubebeka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, George Mayunga hakupatikana kuelezea hatua zaidi za tukio hilo na kama kuna mtu yeyote aliyekamatwa kwa ajili ya kuisaidia Polisi.

                                       CHANZO:darhotwire

No comments: