ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 11, 2011

DAKTARI BINGWA AMUUA MSANII KWA KISU

Richard Bukos na Issa Mnally
Daktari wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Lumuli Mbonile anashikiliwa na jeshi la polisi nchini kwa tuhuma za kumuua kwa kisu, Stanley Balingilaki ambaye alikuwa ni mwanamuziki wa kizazi kipya wa Kundi la Wakushi Camp.


Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, daktari huyo ambaye pia anasoma chuo kimoja nchini Afrika Kusini, anadaiwa kufanya mauaji hayo usiku wa kuamkia Januari 6, mwaka huu, maeneo ya Sinza Makaburini, jijini Dar es Salaam akimtuhumu marehemu kumvamia na kumpora mali zake akiwa pamoja na kundi la vibaka sita usiku wa Januari 1, mwaka huu.

Chanzo hicho kilieleza kwamba kijana huyo na wenzake walimpora vitu vyenye thamani ya shilingi 2,000,000.

Ikazidi kudaiwa kuwa, baada ya daktari huyo kufanyiwa ‘umafia’ huo alikwenda kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi Mabatini huku akiendelea kuwasaka watuhumiwa wake ambapo siku iliyofuata alipewa taarifa kuwa mmoja wa watuhumiwa alikuwa Sinza Makaburini kwenye Pub iitwayo Hellenic.

“Daktari huyo alitoka mbio mpaka maeneo aliyoelekezwa ambapo alimkuta marehemu eneo hilo, akamvamia na kutaka kumtia mikononi lakini akaishia kukatwa visu mikononi.

“Alichokifanya daktari huyo ni kumnyang’anya kisu na kumchoma marehemu kisha akakimbilia Kituo cha Polisi Mabatini kutoa taarifa kuwa alimpata mwizi wake na kuwaomba wakampe msaada zaidi,” kilisema chanzo chetu.

Habari zinasema kuwa, maafande hao walifuatana na daktari huyo na baada ya kufika eneo la tukio walikuta mtu waliyemfuata ameshakufa ndipo walimtia mbaroni Dk. Mbonile na kumfungulia kesi ya mauaji kwa jalada  namba KJM/RB/121/2011.

Ikaelezwa kuwa, taarifa za kifo cha msanii huyo kiliwashtua wasanii wenzake akiwemo Ruta Bushoke ambaye alipofika nyumbani kwa marehemu alishindwa kujizuia kutoa machozi.

Akizungumza kwa uchungu, baba mzazi wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Balingilaki Mushobozi, alisema ameshtushwa na kifo cha mwanae huyo kwani siku zote alikuwa akimfahamu kama mfanyabiashara na mwanamuziki na hakuwahi kusikia akijihusisha na tuhuma zilizomsababishia umauti.

“Naliomba Jeshi la Polisi nchini kufanya uchunguzi wa kifo cha mwanangu ambacho kimegubikwa na utata mkubwa na sheria ichukue mkondo wake baada ya uchunguzi huo kukamilika,” alisema mzee Mushobozi kabla ya kuusafirisha mwili wa mwanaye Ijumaa iliyopita kuupeleka Dodoma kwa mazishi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema uchunguzi unaendelea.



chanzo:Global Publishers

No comments: