ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, January 9, 2011

Familia za waliouawa Arusha kuiburuza serikali mahakamani

Moses Mashalla, Daniel Sabuni, Arusha
SAKATA vurugu zilizotokea wakati polisi eskivunja maandamano Chadema na kisha kuua raia watatu mkoani Arusha hivi karibuni, limechukua sura mpya baada ya familia za watu waliouawa kwa kupigwa risasi kuamua kuifungulia mashtaka Serikali. 

Mbali na uamuzi wa familia hizo Mbunge wa Viti Maalumu mkoani Kilimanjaro kwa tiketi ya Chadema, Lucy Owenya amesema aliliburuza mahakamani Jeshi la Polisi mkoani Arusha kwa madai ya baadhi ya askari wake kumpora simu mbili za mkononi na saa wakati wakidhiti kwa kipigo siku ya maandamano


Mmoja wa ndugu wa marehemu Ismaili Omari (38), Nyerere Kamili ( 55) aliliambia Mwananchi Jumapili kwamba ndugu wamepanga kufanya kikao cha kuandaa taratibu za kisheria kuifikisha Serikali mahamani kusababisha vifo vya ndugu zao waliouawa na askari polisi kwa kuwapiga risasi za moto wakati wa kuzima maandamano ya Chadema Jumatano iliyopita.

Alisema kikao hicho kilikuwa kifanyike mwishoni mwa wiki, lakini ilishindikana kutokana na kuwa subiri ndugu wengine wanaoishi Kondoa, mkoani Dodoma.

Akizungumza na Mwananchi Jumapili jana nyumbani kwa marehemu eneo la Sombetini, mjini Arusha alisema tayari wamewasiliana na mwanasheria wao na kukusanya ushahidi wa jinsi ndugu yao alivyouawa kwa kupigwa risasi.

Alisema kama sio polisi wasingepata mzigo mzito ulioachwa na marehemu wa kuaachia mjane na watoto wadogo wawili, Saumu wa miaka mitatu na Amina mwenye miaka sita, ambao wanataka kusoma na mahitaji ya kibinadamu ili waweze kukua na kujitegemea.

"Huyu kijana wetu alikuwa na familia ilikuwa inamtegemea akiwamo mtoto wake Saumu anayesoma, nani atabeba majukumu yake? Mimi nina watoto wangu na baba yake mdogo ana watoto watano sasa hawa ( wa marehemu) nani atawahudumia hawa?

"Nlienda kumuona huyu kijana pale chumba cha maiti katika hospitali ya Mount Meru ana tundu dogo katikati ya tumbo na la mgongoni tundu lilikuwa kubwa. Inawezekana risasi ilipita tumboni na kutokea mgongoni," alidai Kamili.

Naye Mke wa marehemu Aisa Ismaili (24), ambaye anaishi eneo Unga Limited, akiwa amejawa na huzuni kwa kuondokewa na mumewe, alisema siku ya tarehe tano mumewe aliamka kama kawaida na akamuandalia maji ya kuoga na chai baadaye aliaga kuwa anaelekea kazini mjini.

Alisema mumewe huyo ambaye alikuwa fundi wa umeme wa kujitegemea huwa hana tabia ya kuchelewa kurudi nyumbani hivyo ilipofika saa 2:00 usiku alipata wasiwasi, lakini akajipa moyo kwamba pengine amepata tatizo.

"Tulipoona imefika saa 5:00 usiku niliogopa nikawaita majirani nikawaeleza wasiwasi wangu ndipo wakaamua kupiga simu yake ya mkononi ambayo iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa.

"Baadaye majirani zangu walipiga simu ya mume wangu na kupokelewa na mtu ambaye alikataa kujitambulisha akawaambia Ismaili ameuawa katika maandamano na kwamba mwili wake upo katika hosptiali ya Mount Meru," alisema mke wa marehemu.

Alisema mara ya kwanza majirani walimficha wakimwambia kwamba mume wake ni mgonjwa sana. Kesho yake asubuhi alitayarisha chai kwa ajili ya kumpelekea hospitali ambako alipewa habari rasmi kuwa aliuawa katika vurugu.

Asubuhi alipofika hospitali akiwa na chupa yake ya chai mkononi alimkuta mume wake, Ismaili akiwa katika hali mbaya moyo ukimdunda kwa mbali hali ambayo ilimpa wasiwasi zaidi.

Asia alisema: “Muuguzi alipofika aliniambia kuwa kwa hali aliyokuwa nayo mume wangu hawezi kunywa chai hivyo akanishauri arudi nayo nyumbani, lakini baadaye akiwa njiani majirani walimwambia ameshafariki. 

"Nilipoteza fahamu nakujikuta niko hapa nyumbani. Siamini yaliyomkuta mume wangu," alisema. 
 
Jirani wa marehemu huyo, Deo Lyimo alisema maamuzi ya polisi hayakuwa ya kitaalamu na wanatakiwa wachukuliwe hatua za kisheria.

Lyimo alisema sheria ifuate mkondo wake kwa kuwa polisi wasingefyatua mabomu na kupiga waandamanaji, kusingetokea vurugu kwa kuwa walishatembea zaidi ya kilomita mbili kwa amani.

"Polisi ndio walianza uchokozi maana mimi nilikuwa mbele kabisa ya maandamano. Tulipotoka Hoteli ya Mount Meru viongozi wa Chadema wakiwa wametangulia na vitambaa vyeupe mikononi kuashiria amani walienda mpaka Tank la Maji na ndipo wakaanza kufyatua mabomu na kupiga watu virungu. Tungefika NMC bila vurugu yoyote na mkutano ungeisha vizuri," alisema Lyimo.

Jirani mwingine, Msafiri Shaban alisema jeshi la polisi limeshaweka uhasama kati yake na wananchi na ikizingatia kuwa askari polisi wanaishi na raia mitaani.

"Nilikuwa na mzee mmoja wa Majengo wala hata sikumuuliza jina anasema katika nyumba yake kuna askari polisi wawili wamepang. Ameamua kuwafukuza kutokana na tukio la kuwaua waandamanaji kuwafukuza," alisema. 

Jana viongozi kadhaa wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe walifika kuwafariki wafiwa na kuwapa pole.

Katika hatua nyingine mmoja wa majeruhi aliyepigwa katika vurugu zilizotokea Jumatano wiki hii mjini hapa ambaye pia ni dereva wa Mbunge wa Viti maalumu mkoani Kilimanjaro, Cyprian Mwigune (41) ahamishiwe katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, mkoani Kilimanjaro.

Mwigune ambaye ni Mkazi wa jijini Dar es Salaam  alihamishiwa KCMC jana baada ya viongozi wakuu wa Chadema, kuwatembelea majeruhi wa vurugu hizo.
 
Taarifa za uhakika zilizolifikia gazeti hili zinadai ya kuwa majeruhi huyo alihamishwa ghafla mapema juzi usiku baada ya kuona hali yake inazorota.
  
Hata hivyo, taarifa hizo zinabainisha kwamba kabla ya kuondolewa katika hospitali hiyo, hali yake ilikuwa mbaya kwani alikuwa akishindwa kugeuka kitandani kutokana na kukatika kwa mawasiliano juu na chini ya kiuno kufuatia kujeruhiwa uti wa mgonga na polisi.
 
“Alikuwa hawezi kugeuka wala nini kwasababu alipigwa na polisi na wakamjeruhi kwneye uti wa mgongo na hana mawasilino ya juu na chini ya kiuno kabisa,” alisema mtoa taarifa huyo.

Mbunge Owenya kwa upande wake, aliliambia Mwananchi Jumapili wakati askari hao wakimshuhushia mmoja wao ambaye alidai kuwa anakumbuka sura yake aliingiza mikono yake katika mifuko ya suruali aliyokuwa amevaa na kuchomoa simu mbili na kisha kutokomea nazo ghafla.
 
“Kuna askari mmoja ambaye naikumbuka sura yake alikuja na kuanza kunipekua mifukoni kisha kuchukua simu zangu mbili za mkononi na saa na kutokomea nazo,” alidai Owenya
 
Alisema kuwa kutokana na kitendo hicho anajiandaa kufungua mashtaka kwa askari huyo kabla ya kulifikisha suala hilo katika ngazi za juu za sheria.


                                                CHANZO:MWANANCHI

No comments: