ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 20, 2011

Halmashauri zabanwa

UJANJA uliokuwa ukitumiwa na baadhi ya halmashauri za wilaya nchini wa kutopeleka mafungu yao ya pensheni kwenye Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa (Lapf) umefika ukingoni. 

Kuanzia sasa halmashauri hizo zitakatwa moja kwa moja fedha hizo Hazina kutoka fungu lao la Serikali Kuu ili kuhakikisha Sh bilioni 3.3 zilizokuwa zinadaiwa katika Sh bilioni 7.7 za deni, zinalipwa. 


Hatua hiyo inatokana na agizo la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alilolitoa jana Dar es Salaam wakati anafungua mkutano mkuu wa tatu wa wadau wa Lapf. 

Na ili agizo hilo litekelezwe kikamilifu ili kumaliza deni lililosalia katika kipindi cha mwaka mmoja, Waziri Mkuu aliiagiza Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuingia mikataba na wakurugenzi wa halmashauri zinazodaiwa na kuandika barua Hazina makato hayo yafanyike. 

“Wakati wa mkutano wa pili Desemba mwaka juzi malimbikizo ya waajiri yalikuwa Sh bilioni 7.7 lakini hadi Desemba mwaka jana yalilipwa na kubaki Sh bilioni 3.3 ikimaanisha marejesho yalifikia asilimia 57.7, naelewa kiasi kikubwa cha madai haya kinatokana na adhabu kwa kutowasilisha michango ya wafanyakazi ambao hawako kwenye orodha ya malipo,” alisema Pinda. 

Aliwasihi waajiri wote kutimiza makubaliano yaliyofikiwa katika kumaliza madeni hayo kwa kutolimbikiza tena na wala kutosubiri mpaka suluhisho la kisheria litafutwe “kwani tukiendelea kuvutana, tutaumiza wasio na hatia ambao ni haki yao kulipwa mafao hayo,” alisisitiza. 

Alipongeza uamuzi wa Mfuko huo katika kuongeza mafao kuwa sita - ya uzazi, mazishi, uzee, urithi, ulemavu na elimu kwamba ni ishara kuwa Mfuko unazidi kuimarika na kushauri kuongeza mafao ya muda mfupi ambayo ni kilio cha wanachama wengi. 

“Najua mnatoa mikopo kwa Saccos na sehemu ya pensheni kwa wanachama waliofikia umri wa miaka 55 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba, lakini nasema hiyo bado haitoshi, endeleeni kufanya utafiti kuhusu mafao ambayo wanachama wanayataka hasa wanaojiajiri,“ alisisitiza Pinda. 

Alizikumbusha taasisi za hifadhi za jamii kuwa changamoto zilizonazo ni kuwekeza katika miji mingine nchini, kwa kuwa fursa za uwekezaji zipo, hivyo zisiache Jiji la Dar es Salaam likajaa kuzidi kiasi, kwani takwimu zinaonesha kuwa watu wanaoishi jijini humo ni takriban milioni tano. 

Aliwataka kuelekeza uwekezaji katika mikoa ya mingine hususani Mtwara, Ruvuma na Lindi, ambako watu wao hawafiki hata milioni mbili kwa pamoja, ili watu wasikimbilie Dar es Salaam kufuata huduma mbalimbali kutokana na uwekezaji wa mashirika hayo. 

Naibu Waziri wa Tamisemi, Aggrey Mwanri, alisema amepokea maagizo ya Waziri Mkuu na atayafanyia kazi mapema iwezekanavyo, kwa kuanzia na halmashauri za Mkoa wa Kigoma na kufuatiwa na Tabora na Mwanza. 

Aliwaomba wakurugenzi ambao bado hawajawasilisha malipo ya wafanyakazi wao wafanye hivyo kabla hajafika kwenye mikoa yao. 

Mkurugenzi Mkuu wa Lapf, Eliudi Sanga, alisema michango ya wanachama imeongezeka kutoka Sh bilioni 11.84 mwaka 2005 hadi Sh bilioni 54.24 Juni mwaka jana huku wakiendelea kukamilisha mfumo wa kompyuta ili wanachama wapate taarifa zao kwa wakati. 

Alisema Mfuko unatarajia kuwekeza kwenye ujenzi wa maduka makubwa Dar es Salaam, kuwekeza katika kituo cha mabasi Ubungo na mradi mpya wa maegesho ya malori eneo la Mbezi Luis ambapo thamani ya vitega uchumi vyake hadi Juni mwaka jana ulifikia Sh bilioni 266.


                                                                                  Chanzo:Habari Leo

No comments: