RAIS Jakaya Kikwete amesema Serikali yake ya Awamu ya Pili itahakikisha elimu inayotolewa nchini ni ya kiwango chenye ubora wa juu kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari awamu ya pili (MES II).
Amesema, ili kufanikisha ubora huo, Serikali yake imejipanga kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuwekeza zaidi katika miundombinu ya utoaji wa elimu kwa kuwa suala la kuwekeza katika sekta hiyo ni la lazima na si anasa.
Akizindua mpango huo wa awamu ya pili Dar es Salaam jana, Rais Kikwete aliwataka wananchi waendelee na moyo na ari ya kusaidia maendeleo ya sekta hiyo na kuwapuuza wote wenye kukebehi mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo kupitia awamu ya kwanza ya mpango huo.
“Tumepata mafanikio makubwa katika awamu ya kwanza ya mpango huu ambayo yamekuwa gumzo hata nje ya mipaka ya nchi yetu na kutujengea heshima, katika awamu hii ya pili changamoto kubwa kuliko yote ni kuhakikisha elimu inayotolewa kwa watoto wetu ni ya kiwango cha ubora wa juu,” alisema Rais Kikwete.
Alisema, kupitia mpango huo Serikali itahakikisha wanafunzi wote wa sekondari wanapata Sh 25,000 kwa ajili ya vitabu na vifaa vya maabara, walimu wa kutosha wenye elimu na ujuzi unaostahili na kuwapo kwa mazingira mazuri ya kusomea na kuishi kwa walimu.
Tayari Benki ya Dunia imechangia dola za Marekani milioni 150 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo ambapo dola za Marekani milioni 50 zimeshatolewa.
Rais Kikwete aliwapongeza wananchi kwa jitihada na moyo walioonesha kufanikisha ujenzi wa shule nyingi za kata nchini ambazo zimesaidia kupunguza tatizo la wanafunzi wengi kukosa nafasi za kuendelea na masomo ya sekondari.
Alisema kupitia juhudi hizo, hadi Juni mwaka 2010 idadi ya shule za sekondari za Serikali ilifikia 3,397 ikilinganishwa na shule 824 zilizokuwepo mwaka 2004.
Aliwataka kuendelea na moyo huo hata katika awamu ya pili ya mpango huo na kuwapuuza wanaokebehi mafanikio yaliyofikiwa kwa pamoja katika sekta hiyo ya elimu kwa kuwa wanaofanya hivyo hawaitakii mema Tanzania.
“Anayebeza mafanikio tuliyofikia katika sekta ya elimu, anatubeza sisi sote kwa maana shule hizi nyingi zimejengwa kwa nguvu ya wananchi, naomba tusikubali kuyumbishwa katika mambo yahusuyo elimu na ustawi wetu binafsi na wa taifa letu,” alisema.
Chanzo:Habari Leo
No comments:
Post a Comment