.jpg)
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema,
amezungumzia mauaji yaliyofanywa na askari wa jeshi hilo dhidi ya raia mjini Arusha bila kulaani tukio hilo.
Alizungumzia tukio hilo wakati akijibu maswali yaliyoulizwa na waandishi wa habari, katika mkutano ulioitishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha, jijini Dar es Salaam jana.
Kushindwa kwa IGP Mwema kulaani tukio hilo, kulidhihirika wakati wa kipindi cha maswali, ambapo waandishi walimtaka Waziri Nahodha kueleza kama haoni kuna haja kwa yeye na IGP Mwema kuwajibika kisiasa kutokana na tukio hilo.
Akijibu swali hilo, IGP Mwema alisema madhara yaliyotokea katika tukio hilo, yalitokana na viongozi wa Chadema na wafuasi wao kukaidi amri ya Jeshi la Polisi iliyowataka kusitisha maandamano kwa vile kulikuwa na tishio la kuvunjika kwa amani.
“Taarifa za Kiintelijensia lilizokuwa nazo Jeshi la Polisi na wananchi ni sehemu ya habari. Hamkuona gari na nyumba zimechomwa? Hamkuona fujo zilizotokea?,” Alihoji IGP Mwema.
Aliongeza: “Wataalamu wanasema kuwa makosa mawili hayatafanya mmoja awe sahihi zaidi ya mwingine. Kulikuwa na tishio, tishio la kweli. Tukawaambia wenzetu tishio lipo. Sasa wao wakakaidi na kufanya yale maandamano. Sasa ukiyafanya halafu madhara yakitokea, unasema mwenzako awajibike.”
“Kwa hiyo kama kuna kuwajibika, yako mambo ya sheria. Hili suala si letu peke yetu. Watu tuliowakamata, upelelezi wa jalada tunaupeleka kwa mwanasheria. Mwanasheria akisoma, akaona kwamba kuna kilichokosewa kwa mujibu wa sheria, kama ni sisi tutawajibika, kama ni wao watawajibika. Lakini mambo yatafuata sheria.”
Alisema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye, awali aliruhusu maandamano ya Chadema, lakini baadaye akayazuia kwa maandishi.
“Kwanza hilo lieleweke. Kuna barua ya ruksa na katazo la RPC Arusha,” alisema IGP Mwema.
Alisema kilichomfanya aongeze msisitizo wa katazo la Kamanda Andengenye, kilitokana na barua za Chadema zilizopelekwa polisi kuomba kuruhusiwa kufanya maandamano kumnukuu yeye (IGP Mwema) kwa kurejea mazungumzo aliyoyafanya na Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe kuhusu suala hilo.
Kutokana na hilo, alisema barua ya Chadema ya kuomba kufanya maandamano, ilikuwa imeandikwa kurejea mazungumzo yake na Mbowe.
Hivyo, akasema kwa kuondoa utata ikabidi aonyeshe wazi kwamba, taarifa alizonazo Kamanda Andengenye na zile walizokuwa nazo polisi makao makuu, kulikuwa na umuhimu wa ngazi ya kitaifa waliyokuwa wameongea na yeye pia aieleze wakati huo, ili ieleweke kwa wote.
“Kwa hiyo hakuna RPC (Kamanda) anaruhusu, halafu IGP anakataa. Ipo ruhusa aliyoitoa RPC hadi ilipokwenda na habari alizozipata za Kiintelijensia na zetu, akatoa katazo. Na akatuambia na sisi, tukamwambia sawa... Kwa hiyo hatusemi mambo mawili tofauti. Lazima litakuwa jambo moja, mkoa mmoja, nchi moja,” alisema IGP Mwema.
Naye Waziri Nahodha alisema polisi walilazimika kuwazuia wafuasi wa Chadema, ambao walivamia kituo cha polisi kwa ajili ya kuwatoa wenzao waliokuwa wanashikiliwa kituoni hapo.
Alisema hali hiyo ilisababisha kuzuka vurugu, ambapo magari yalianza kushambuliwa, vibanda vya biashara na nyumba kuchomwa moto na watu wapita njia kupigwa.
Nahodha alisema kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi lililazimika kudhibiti hali hiyo ili kunusuru raia na mali zao.
Alisema kutokana na vurugu hizo, wananchi wawili walipoteza maisha, kulikoelezwa na IGP Mwema kwamba, kulitokana na kupigwa risasi na wengine sita kujeruhiwa.
Nahodha alisema Tanzania ni nchi ya Watanzania wote, hivyo, wanasiasa wote wenye fikra na mawazo tofauti na wasiokuwa wanasiasa, wakubwa na wadogo, wanawake na wanaume, wana wajibu mkubwa wa kulinda amani ya nchi.
Alisema hali inayotokea Arusha si nzuri na si jambo la kufurahisha kwa wote wapenda amani, hivyo, akasema serikali inapaswa kuituliza hali hiyo.
Alisema kwa kuwa suala la Arusha ni mgogoro wa kisiasa, serikali imedhamiria na kukusudia kuwakutanisha wanasiasa wa pande zinazohusika ili kutafuta njia mwafaka itakayoleta utengamano Arusha kwa kuwa wanaamini mgogoro wa kisiasa unasuluhishwa kisiasa.
“Biblia Takatifu inasema: “Heri wapatanishi kwani wao watarithi nchi,” alinukuu Nahodha.
MARANDO AJA JUU
Mwanasheria wa Chadema, Mabere Marando, alisema vurugu hizo zimesababisha na Jeshi la Polisi wakishirikiana na serikali.
Alisema kuwa wamesikitishwa na kitendo cha Jeshi la Polisi kujichukulia sheria mkononi wakati maandamano hayo yalikuwa ni ya amani na kwamba tayari yalishapatiwa kibali na Polisi mkoa.
Marando alisema jeshi hilo lisingefanya vurugu ambazo walizionyesha, kusingetokea madhara na kwamba waliokamatwa hawakuwa na kosa lolote.
Alisema kuwa Mkuu wa Polisi katika mkoa huo alitakiwa kutoa taarifa kuhusiana na kusitisha kwa zoezi hilo kutokana na kwamba alisharuhusu zoezi hilo kuendelea.
Marando aliyekuwa akizungunza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, alisema Jeshi hilo lilipaswa kutoa taarifa katika chama hicho kuwa wasiandamane kwa kuwa awali walisharuhusiwa kuandamana.
CUF YALAANI VIKALI
Chama Cha Wananchi (CUF) kimepinga vikali kitendo cha kinyama kilichofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwapiga na kuwajeruhi viongozi na wafuasi wa Chadema.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema kuwa kitendo hicho ni cha kinyama na kwamba Jeshi la Polisi lisingetakiwa kujichukulia sheria mkononi.
Alisema kuwa maandamano hayo yalikuwa ya amani kwani chama hicho kilikuwa na haki ya kuandamana kwa kuwa kuandamana ni haki ya kikatiba na sio vinginevyo.
“Cuf tunaamini kuwa Chadema ni chama cha siasa kilichosajiliwa kihalali, hivyo kilikuwa na haki ya kikatiba na kisheria kufanya maandamano yao ya amani ambayo tayari Jeshi la Polisi la Arusha lilishakubali na kuahidi kuwa watatoa ulinzi wa kutosha,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema kuwa asilimia kubwa ya madhara yaliyotokea kwa wananchi yametokana na Jeshi la Polisi pamoja na serikali na kuwa hao ndio wanatakiwa kulaumiwa kwa uvunjaji wa amani uliotokea Arusha.
Profesa Lipumba alisema ushahidi wa kimazingira unaonyesha wazi kuwa amri ya kusitisha maandamano iliyotolewa na IGP Said Mwema saa chache kabla hayajafanyika kutokana na shinikizo la kisiasa.
Alisema hoja iliyotolewa kuwa taarifa za kiintelijensia kuna watu watavunja amani na ndiyo maana maandamano yanazuiliwa.
“Taarifa hizo ni za kisanii na kama ni kweli polisi wana taarifa za kiintelijensia kuwa kuna watu watavunja amani, basi wazitumie taarifa hizo kuwadhibiti watu hao na sio kuyasitisha maandamano na kuwanyima wananchi uhuru wa kisheria wa kufanya maandamano,” alisema.
Alisema nchi hii inapaswa kuongozwa na katiba na sheria na kwamba Watanzania wasikubali serikali iliyopo madarakani kutumia vyombo vya dola kuua uhuru wa demokrasia.
Alisema jeshi la polisi limekuwa mstari wa mbele kuzuia kila aina ya madai yanayotolewa na vyama ili mwisho wa siku wawe wanalinda maslahi ya CCM na utawala wao.
“Haiwezekani kila watu wakitaka kuandamana kwa amani Jeshi la Polisi lianzishe hoja eti kwa sababu za kiintelijensia maandamano hayo yanafutwa je, hizo taarifa za kiintelijensia ni zipi?” alihoji.
Alisema kuna haja ya kujiuliza kuwa kama magaidi wakitaka kulipua Tanzania wasingeshindwa kwani kuna sehemu nyingi ambazo wanaweza kufanya hivyo bila kusubiri maandamano ya Chadema au CUF.
“Hivi tujiulize kama kweli pana tishio la ugaidi iweje mechi za mpira zinaendelea bila kuzuiwa na polisi wakati mikusanyiko yote inafanyika isipokuwa maandamano ya vyama vya siasa je, hao magaidi wanatokea wapi katika kulipua maandamano peke yake kwanini nchi hii iendeshwe kisanii na ni kwanini serikali inaogopa maandamano?” alihoji Lipumba.
Alisema kitendo walichokifanya ni kwamba wameweka doa kubwa katika Jeshi la Polisi ambalo linaongozwa na Mwema anaheshimika.
Hata hivyo, alisema IGP anachotakiwa ni kulinda heshima yake na sio kutumiwa kisiasa kwa ajili ya kukandamiza demokrasia ya nchi kwani atasababishia kuvuruga amani.
Alisema chama chake kinatoa pole kwa wahanga wote waliopigwa na kuumizwa na mabomu ya maji ya kuwasha na risasi katika tukio hilo la kihistoria la kudai haki ya wanyonge.
Profesa Lipumba alisema kuwa Rais Jakaya Kikwete anatakiwa kutumia busara zake katika kuendesha nchi vizuri ili aweze kukumbukwa kwa mambo ya heri na sio kwa mambo ya shari.
“Kukaa kimya kwa Rais wakati polisi wanatumia nguvu kubwa kuua demokrasia ndani ya nchi kunaashiria kuwa wanatimiza amri ya Rais,” alisema.
TENDWA AZUNGUMZA
Msajili wa vyama vya Siasa, John Tendwa, amesikitishwa na kitendo cha viongozi wa Chadema kuwaamrisha wafuasi wake kufanya maandamano ili hali wakijua maandamano hayo yameshapigwa marufuku.
Akizungumza na NIPASHE jana ofisini kwake, Tendwa alisema siku moja kabla ya kufanya maandamano hayo, Dk. Slaa alimpigia simu na kumweleza kuwa Polisi wamezuia maandamano yao na wameruhusiwa kufanya mkutano pekee.
Alisema kitendo cha Dk. Slaa kuutangazia umma kuwa maandamano hayo yalikuwa ya halali si kweli kwani Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Thobiasi Andendenye alipeleka barua ya kuzuia maandamano hayo siku moja kabla.
“Kila mtu atimize wajibu wake kwa kutii sheria na amri za mamlaka husika, tusijidanganye kuwa kwa kutumia nguvu tutatatua tatizo letu, ilikuwa ni faraja kwao kwa kuruhusiwa kufanya mkutano wangeweza kusema yale yote ambayo wanayo na wahusika wangesikia, lakini yaliyotokea ndio hayo,” alisema Tendwa.
Alisema baada ya mazungumzo hayo, Dk. Slaa alimtumia ujumbe mfupi unaosomeka: “Tumepokea barua ya RPC sasa hivi, inafuta barua ya 1 na sasa wamepiga marufuku maandamano na wameruhusu mkutano sababu ya uvunjifu wa amani.”
Tendwa aliwataka wananchi kuchukua tahadhari katika mambo wanayoshawishiwa kwa kuangalia ukiukwaji wa sheria. “Wasikubali kila kitu, waangalie jambo hili ni haki au kuna walakini, wasiwe kama Kenge kwa Mamba, japokuwa wao walikwenda pale kwa nia nzuri ya kusikiliza mkutano, lakini yakatokea hayo yaliyotokea,” alisema.
Alisema kwa kuwa Chadema wanalalamika kuwa wameibiwa kura zao katika uchaguzi wa Meya na kuwa ingekuwa ni busara kwa viongozi hao kufungua kesi mahakamani ambayo ni haki yao ya msingi na kama ushahidi ungekuwepo haki yao wangepata.
“Haipendezi kufanya hicho kilichofanyika, nchi inaongozwa kwa sheria, wangefuata sheria, na wangetii amri za mamlaka husika na kile ambacho walikitaka kingefanikiwa kwa urahisi zaidi,” alisisitiza.
WAZIRI WASIRA NAYE ANENA
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (Mahusiano na Uratibu), Steven Wasira, akizungumza sakata hilo, alisema kilichotokea juzi mkoani Arusha ni matokeo ya kutofuatwa kwa misingi ya amani na kutotii amri za mamlaka husika.
"Chadema kiliomba kufanya mkutano na maandamano ya amani, lakini katika hali ya kawaida kutokana na uzoefu wa polisi kwa kile walichokiona walisitisha maandamano hayo, lakini viongozi wakalazimisha kufanya hivyo na kilichotokea ni uvunjifu amani, wote walitumia nguvu,” alisema Wasira.
Waziri Wasira alisisitiza kuwa: “Kila Mtanzania ana haki ya kutoa maoni yake ambayo anafikiri yanafaa, kinachotakiwa ni kufuata taratibu, na si kila maoni lazima utumie nguvu kuyafikisha, stahili ya kutumia nguvu ni uvunjifu wa amani,” alisema.
“Ili kudumisha misingi ya amani, ni lazima tutii sheria kwa hiyari, sheria hizi tunazitunga sisi wenyewe, maana sheria hutungwa na mbunge uliyemchagua ambaye ni mwakilishi wako, kwa nini usizikubali na kuzitii?” alihoji Wasira.
SOPHIA SIMBA AWALAANI CHADEMA
UMOJA wa Wanawake Tanzania(UWT), kimelaani vurugu zilizosababishwa na na viongozi na wafuasi wa Chadema kwa kukaidi amri ya Jeshi la Polisi nchini kutofanya maandamano.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa UWT na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Waziri Simba alisema UWT inalaani vurugu hizo zilizotokana na Chadema kuandaa maandamano ambayo alidai kuwa ni ya maslahi binafsi kwa chama chao ikiwemo kushawishi wananchi kudai katiba mpya kwa nguvu.
“Kitendo cha viongozi na wafuasi wa Chadema kufanya maandamano bila ridhaa kina lengo la kuifanya nchi ya Tanzania isitawalike na kuingia kwenye machafuko na vita ili serikali iliyoko madarakani ishindwe kutimiza wajibu wake kwa wananchi,” alidai na kuongeza:
“Chadema imeandaa maandamano kwa maslahi binafsi kwa chama chao ikiwemo kushawishi wananchi kudai katiba kwa nguvu, jambo ambalo Rais Jakaya Kikwete ameshalitolea ufafanuzi na mchakato utakaofuatwa katika kufikia dhamira hiyo,” alisema Waziri Simba.
UVCCM NAYO LAWAMA
Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) umetoa onyo kwa Chadema kwamba kiko tayari kutumia mbinu na njia zozote zilizo katika uwezo wake ili kuhakikisha kwamba Tanzania inatawalika ,kinyume na nia ya Chadema ya kuanzisha vurugu zitakazopelekea nchi isitawalike.
Taarifa hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na Kaimu Mwenyekiti UVCCM, Benno Malisa, alipokuwa akitoa taarifa ya msimamo wa umoja huo kwa vyombo vya habari kufuatia vurugu kubwa iliyotokea juzi Arusha.
“Uvccm imesikitishwa na kukerwa kwa kiasi kikubwa na vurugu hizo hasa kwa vile ziliongozwa na viongozi wakuu wa Chadema akiwemo Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe; Katibu Mkuu, Dk.Wilbrod Slaa; wajumbe wa kamati kuu, Philemon Ndesamburo na Lucy Owenya, Wabunge na Viongozi Mbalimbali,” alisema.
“Niitumie nafasi hii kwa kutoa angalizo kwamba nchi yetu inaendeshwa kwa misingi ya utawala wenye kuheshimu sheria. Ni vema kwa raia wa Tanzania,vikundi mbalimbali na asasi zote nchini zikaendesha shughuli zake kwa kuheshimu sheria za nchi kinyume chake ni lazima sheria ichukue mkondo wake mara moja,” alisema.
Naye mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM Taifa, Ridhiwani Kikwete, aliwaasa Watanzania na hasa vijana kutokubali kutumiwa na Chadema kwa hali yoyote ile bali wafuate vyombo vya dola vinavyoelekeza.
Imeandikwa na Beatrice Shayo, Carren CyprianHellen Mwango, Raphael Kibiriti na Muhibu Said.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment