
Rais Jakaya Kikwete
Akizungumza na HABARILEO Jumapili kwa njia ya simu jana, Bana alisema Rais Kikwete anastahili kupongezwa na kila mtu wenye mapenzi mema na Taifa la Tanzania, kwa kuwa msikivu na kupokea hoja zilizotolewa na makundi mbalimbali ya Watanzania kisha kutangaza mchakato wa kuunda Katiba hiyo.
Juzi Rais Kikwete alitoa salamu za mwaka mpya kwa Taifa na kusema ameamua kuunda Tume
maalumu ya Katiba, ambayo itakuwa na wajumbe wanaowakilisha makundi mbalimbali katika jamii kutoka pande mbili za Muungano.
Rais Kikwete alisema Tume itaongozwa na mwanasheria aliyebobea ili kuongoza na kuratibu mchakato wa kuunda Katiba hiyo kwa kushirikisha wananchi, vyama vya siasa, wafanyabiashara, vyama vya kiraia, mashirika ya dini na wanataaluma na makundi mbalimbali ya watu wote, katika kutoa maoni kuhusu Katiba ya nchi.
Dk Bana alisema uamuzi wa Kikwete wa kuandaa mchakato wa kuunda Katiba mpya, unadhihirisha kuwa Serikali yake ni sikivu, inawajibika na kukubali kupokea mabadiliko pasipo kushurutishwa.
Alifafanua kuwa suala la kuunda Katiba mpya haliko kwenye ilani ya CCM na inaonekana kuwa halikuwa kipaumbele cha Serikali, lakini Rais ameamua kulipa uzito ili kukidhi matakwa ya wananchi.
Alisema ili kufanikisha lengo la kuunda Katiba mpya, Watanzania wanapaswa kuwa wavumilivu na kumpa Rais muda wa kutoa hadidu za rejea na taarifa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutangaza majina ya Tume atakayounda na vigezo vilivyotumika kuteua wajumbe wa Tume hiyo.
Pia Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, alisema Rais anastahili pongezi kwa kuwa amesikia maoni ya wananchi na kuyafanyia kazi mara moja.
Alisema kwa kuwa Rais Kikwete ni Mwenyekiti wa CCM, hakuna mtu anayeweza kuhoji juu ya uamuzi wa kuruhusu mabadiliko ya Katiba ya nchi, kwa kuwa amefanya hivyo kwa maslahi ya Taifa.
Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa wamekuwa na hisia tofauti na wameonesha wasiwasi wakidai kwamba huenda Rais Kikwete hana dhamira ya dhati ya kuunda Katiba mpya ya nchi.
Profesa Mwesiga Baregu wa Chadema, alisema ili kufanikisha mchakato wa kuunda Katiba ya nchi, ni vema Rais akatoa mwanya wa kuunda Tume huru ambayo itawakilisha wananchi wakati wa kukusanya maoni badala ya Rais kuunda Tume ambayo inaweza kutiliwa shaka kwa kuwa itawajibika kwa Rais.
“Asasi, vyama vya siasa na taasisi mbalimbali ziruhusiwe kuteua wajumbe wa Tume ya kukusanya maoni katika mchakato wa kuunda Katiba ili kuimarisha demokrasia kwa kuwa ni ya Watanzania,” alisema Profesa Baregu.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alisema hana imani na Tume itakayoundwa na Rais kwa madai kuwa itawajibika kwake, hivyo kupeleka maoni ya kumridhisha badala ya Watanzania.
Alisema Rais Kikwete anapaswa kuwa mwangalifu na kufanya uamuzi kulingana na mazingira ya sasa kwa kuwa Watanzania wa leo si wa miaka 10 iliyopita, ambao hawakuwa na elimu wala uhuru wa kuhoji na kutetea maslahi ya nchi.
“Kuna mifano hai ya Tume zilizoundwa na Rais na hazikuzaa matunda, ikiwamo ya Jaji Kisanga, Jaji Nyalali na White Paper … hazikufanikiwa kwa sababu ziliwajibika kwa Rais na kufanya kazi kwa matakwa ya Rais, kama Kikwete anataka kutumia mbinu hiyo haitawezekana,” alisema Slaa.
Tume ya Nyalali ndiyo iliyokuja na uamuzi wa kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa ambao ulianza kutekelezwa rasmi mwaka 1992, licha ya idadi kubwa ya Watanzania waliohojiwa kutaka kuendelea na mfumo wa chama kimoja.
Dk Slaa alidai kuwa Watanzania wameshavumilia vya kutosha na hivi sasa nchi imejaa wasomi wenye uwezo na nguvu za kupigania haki kwa maslahi ya nchi na kumshauri Rais Kikwete atumie mbinu shirikishi kudumisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Naye Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila alisema Chadema ilikurupuka na kudandia hoja ya Katiba mpya ya nchi bila kuzingatia maslahi ya Watanzania na kuonya kuwa mchakato wa kuunda Katiba unaweza kushindwa kama utafanywa kwa lengo la kukidhi matakwa ya watu wachache wanaoshinikizwa na wageni.
Akizungumza kwa simu jana, Mtikila alisema si viongozi wa Chadema wala wa CCM wenye dhamira ya dhati ya uundaji wa Katiba mpya kwa maslahi ya Watanzania, kwa kuwa wapo watu wachache wanaotaka Katiba iundwe, kwa maslahi binafsi kwa lengo la kuendeleza zama za ukoloni.
“Mimi nilipojaribu kuzungumzia Katiba mpya na haja ya kuwa na Serikali tatu, watu waliniona kichaa, jambo ambalo lilisababisha kampeni ya kutaka Katiba kuwa ngumu na isiyo na mafanikio … sasa watu hao hao wanataka Katiba mpya kwa maslahi yao,” alisema.
Hata hivyo Mtikila alimwomba Rais Kikwete, asisahau kumjumuisha kwenye Tume atakayoiunda kwa kuzingatia kuwa ametumia muda mwingi kudai Katiba mpya ya nchi akiwa na dhamira ya dhati.
Madai ya Katiba mpya yalianza baada ya uchaguzi mkuu mwaka jana, ambapo viongozi mbalimbali walijitokeza kuzungumzia haja ya kuwa na Katiba hiyo na kuungwa mkono na vyama vya siasa, mashirika ya dini na asasi za kiraia.
Chanzo:Habari Leo
No comments:
Post a Comment