ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 17, 2011

SKENDO ZA IKULU: Mzee Kenyatta atajwa kuvunja ndoa ya Rais Moi

Mzee Kenyatta.
Na Mwandishi Wetu
Wiki hii tunagusa skendo ambayo ilitokea nchi jirani ya Kenya. Inamhusu Rais Mstaafu, Daniel Toroitich Arap Moi na marehemu mke wake, Helena Bommet au Lena Moi kama alivyojulikana zaidi.

Mtandao mmoja wa nchini Uganda, mwaka 2005 uliandika  kuwa sababu ya Moi kuachana na Lena haijulikani moja kwa moja lakini Baba wa Taifa la Kenya, mzee Jomo Kenyatta alihusishwa.


Moi na Lena walitajwa kuachana mwaka 1974 lakini wawili hao hawakutaka ijulikane.

Mmisionari Paul Barnett, aliyembatiza Helena kwenye Kanisa la Africa Inland Church, aliwahi kuzungumza kwenye kitabu cha Andrew Morton  kuwa ndoa ya Moi ilikuwa ya kichekesho.

Barnett alizungumza kwa msisitizo: “Ni bora walivyoachana.”

UTATA KUHUSU MZEE KENYATTA
Mmoja wa watu wa familia ya Moi alimueleza Morton kuwa sababu ya Lena kuachwa na Moi mwaka 1974 ni kwamba mwanamke huyo aligoma ‘kudansi’ na mzee Kenyatta.

Hata hivyo, maneno ya mwanafamilia huyo yalikosa nguvu pale picha zilipovuja na kumuonesha Lena ‘akidansi’ na mzee huyo. Tukio hilo lilitokea kwenye hafla moja iliyoshirikisha viongozi wa juu wa serikali.

Kutokana na picha hiyo, maneno ya chini chini yakaibuka kwamba pengine Moi alichukizwa na kitendo cha mkewe kucheza na mzee Kenyatta ndiyo maana ‘alimpiga chini’.

Wakati tukio hilo linatokea, Moi alikuwa Makamu wa Rais wa Kenya na kipindi hicho, mzee Kenyatta akiwa ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa taifa hilo.

MATESO YA LENA BAADA YA KUACHWA
Mtandao huo uliandika kuwa maisha ya Lena baada ya kuachwa na Moi yalijaa upweke.  Mwanzoni alilazimishwa kusimama kwenye macho ya jamii kama ‘First Lady’ (mwaka 1978).

Habari zinasema kuwa katika kipindi hicho, Lena alibadilika na kuwa mtu aliyekosa uvumilivu na anayepandwa na jazba kwa haraka.

Kabla ya hapo, First Lady huyo wa Pili wa Kenya alitajwa kwamba alikuwa mwanamke mnyenyekevu, aliye na ushirikiano muda wote.

“Alikuwa mnyenyekevu, anayemuogopa Mungu na mwerevu,” Rais wa sasa wa Kenya, Mwai Kibaki alisema kuhusu Lena, siku ya mazishi yake, Julai 31, 2004.

ALIKUWA FIRST LADY HEWA?
Imeelezwa kuwa Lena na Moi waliachana mwaka 1974 lakini mwaka 1978 baada ya mzee Kenyatta kufariki dunia, alilihudumia taifa hilo kama mke wa rais (Moi aliposhika hatamu).

Yapo maelezo kuwa Moi na Lena hawakutaka ‘ishu’ yao ya kutengana ijulikane haraka, hivyo wakawa wanajitokeza hadharani kama mke na mume hasa katika shughuli za kijamii.

NDOA YA MIAKA 24
Lena alifariki dunia Julai 22, 2004 na kuzikwa Julai 31 mwa huo. Alifunga ndoa na Moi mwaka 1950, ndoa ikadumu kwa miaka 24 kabla ya kuachana. Walifanikiwa kupata watoto nane.
chanzo:Global Publishers

No comments: