TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars jana ilishindwa kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya Bonde la Mto Nile baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Uganda.
Matokeo hayo yanaifanya Uganda iungane na Misri kufuzu nusu fainali, na Stars ikisubiri Burundi ifungwe na Misri ili ipate nafasi ya kuwania mshindi wa tatu, lakini Burundi ikishinda, Stars itakosa nafasi hiyo kwa vile itakuwa ya mwisho kwenye kundi lao.
Stars ilianza vizuri mechi ya jana ambapo ilikuwa ikifanya mashambulizi kadhaa, kabla Athumani Machuppa hajaandika bao la kuongoza katika dakika ya 24.
Machuppa, anayesakata soka ya kulipwa Sweden alifunga bao hilo kwa shuti baada ya kupokea mpira wa juu na kuujaza mpira wavuni.
Mapema katika kipindi hicho, kulikuwa na mashambulizi ya hapa na pale ambapo Daniel Wagaluka nusura aipatie Uganda bao katika dakika ya 10 pale alipowatoka mabeki wa Stars na kupiga shuti kali ambalo liliishia mikononi mwa kipa wa Stars Juma Kaseja.
Dakika mbili baadaye Kaseja aliokoa hatari katika lango la Tanzania kutokana na shuti kali la Derick Walulya.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na safari hii ni kwa upande wa Uganda ambapo walilisakama lango la Stars kwa dakika kumi za mwanzo lakini washambuliaji wake walishindwa kulenga lango la Stars.
Katika kipindi hicho, Kocha Jan Poulsen aliamua kufanya mabadiliko ili kunusuru jahazi lake ambapo aliwatoa Salum Machaku, Saidi Maulidi na kuwaingiza Mrisho Ngassa na Idrissa Rajabu.
Hata hivyo mabadiliko hayo hayakusaidia kwani dakika ya 71 Yudah Mugalu aliisawazishia Uganda bao hilo kwa kichwa kutokana na mpira wa kona.
Katika kipindi hicho, Stars ilicheza vibaya na kuifanya Uganda kutawala karibu sehemu kubwa ya mchezo, pamoja na kocha Poulsen kufanya mabadiliko mengine ya kuwatoa Machuppa na Shaaban Nditi na nafasi zao kuchukuliwa na Jabir Azizi na Ally Ahmed ‘Shiboli’ lakini hakukuwa na matunda.
Stars ilipangwa kama ifuatavyo: Juma Kaseja, Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Juma Nyoso, Aggrey Morris, Nurdin Bakari, Salum Machaku/ Mrisho Ngassa, Shaaban Ndiri/ Ally Ahmed ‘Shiboli’, Nizar Khalfani, Athumani Machuppa/ Jabir Azizi, Saidi Maulidi/ Idissa Rajabu.
Chanzo:Habari Leo
No comments:
Post a Comment