
Tunakutana tena kupitia safu hii kwa mara ya kwanza ndani
ya mwaka 2011 nikiamini kwamba umejaaliwa kuuona ukiwa mzima wa afya njema. Ni jambo la kumshukuru Mungu kwa kuwa, wapo waliotamani hadi leo wawe hai lakini kwa bahati mbaya au nzuri wameshatangulia mbele za haki.
Wapenzi wasomaji wangu, kabla ya kukiandika kile ambacho nimedhamiria kukiandika kwa wiki hii, kwanza niwaombe mawazo pamoja na ushauri wenu kuhusu safu hii ili niweze kuiboresha.
Mnashauriwa pia kuuliza maswali yanayohusiana na yale yanayowatatiza katika maisha yenu ya kimapenzi nikiamini kwamba, kutoka kwenye maswali hayo nitapata mwanga wa nini mtapenda nikiandike. Natarajia ushirikiano wenu.
Baada ya kusema hayo sasa nirudi katika kile nilichokuandalia kwa siku ya leo. Nazungumzia jinsi ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakiikosa furaha ya maisha kwa kukubali kuingia katika uhusiano wa kimapenzi wa kujifichaficha.
Ni wengi ambao sasa hivi wako katika aina hiyo ya mapenzi kutokana na sababu mbalimbali, baadhi zikiwa za msingi lakini wengine wakiwa hawana sababu zinazokubalika kulifanya penzi lao lisiwe wazi bali ni utapeli tu.
Ukijaribu kuchunguza utagundua kuwa, wengi walio katika mapenzi ya siri ni wale waliooa au walioolewa. Unakuta mwanamke ameolewa lakini kutokana na tamaa zake anaanzisha uhusiano na mwanaume mwingine nje ya ndoa na kumuomba iwe siri kwani bado anampenda mumewe.
Ukiachilia mbali hao walio katika ndoa, cha ajabu sasa unakuta mtu hajaolewa/hajaoa anaingia katika uhusiano lakini analazimisha penzi lao lisijulikane.
Hapo ndipo kwenye walakini. Awali, tumeona wanandoa wanaingia katika uhusiano nje ya ndoa na kutaka iwe siri kulinda ndoa zao (licha ya kwamba haikubaliki).
Je, wewe ambaye uko singo na unataka mtu wa kuwa naye maishani mwako na umempata, kwa nini unataka penzi lenu liwe la kuibia?
Ninachokiona hapa ni kwamba, mtu anayeng’ang’ania kutaka penzi lenu liwe la siri atakuwa ni tapeli na inawezekana ama kaolewa, kaoa au ana mpenzi wake na tamaa zake ndizo zinamsukuma kuanzisha uhusiano na wewe. Huyu ni mtu ambaye unatakiwa kuachana naye mara moja.
Hata hivyo, kukubali kuingia kwenye penzi la siri na mtu ni kujinyima furaha ambayo baadhi ya watu wamekuwa wakiipata kutoka kwa wapenzi wao. Soma madhara ya kuingia katika uhusiano wa aina hiyo hapa chini.
Kumfaidi kwako ni faragha tu
Aina hii ya uhusiano haiwezi kukufanya ukawa huru na huyo uliyempa nafasi katika moyo wako. Hautakuwa huru kwa sababu, kuna wakati utahitaji kuongozana naye kwenda sehemu fulani, hatakuwa tayari kwa hilo.
Hata kukutana sehemu za wazi itakuwa ni vigumu hali inayoweza kukufanya ukashindwa kumfaidi mwenza wako. Sana sana utamfaidi faragha.
Usipokuwa makini utabambikiwa
Ukiachilia mbali hilo la kutokuwa huru naye, kama wewe ni mwanaume na ukakubali kuwa na uhusiano na msichana kwa siri, ni rahisi sana kubambikiwa hasa linapokuja suala la mimba.
Mpenzi wako anaweza kuwa anatembea na mwanaume mwingine kwa siri na akapewa ujauzito lakini kwa kuwa unajua kwamba wewe ndiye ambaye uko naye, huwezi kuikataa, utasema ni yako kumbe umebambikiwa!
Huenda hauko peke yako Staili ya ‘penzi letu liwe la siri’ hutumiwa sana na wale ambao wametawaliwa na tamaa za kijinga, wasioridhika na mpenzi mmoja. Matokeo yake sasa kila anayemtamani anamchomekea lakini anaomba penzi lao liwe la siri ili wengine wasijue.
Ndio maana nikasema, mpenzi wako akikuambia uhusiano wenu uwe wa siri, huyo yaweza kuwa siyo muaminifu.
Baada ya kusema hayo naomba nishauri kitu. Unapoingia katika uhusiano wa kimapenzi na mtu na akaonekana si mtu wa kutaka watu wajue kuwa nyie ni wapenzi, una kila sababu ya kujua sababu za kutaka iwe hivyo, nyingine ziko wazi na zinavumilika kwa wakati flani.
Ni hayo tu kwa leo, tukutane wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment