
Najua kwamba tumejadiliana mambo mengi ya mapenzi katika mwaka uliopita wa 2010, mengi yalikuwa mazuri na yenye manufaa katika kuendeleza uhusiano kati yetu na wapenzi wetu.
Lakini katika hayo, kuna wale ambao walikosa mafaniko na wakajikuta wakiwa nje ya uhusiano na wenza wao hadi kufikia kukosana au kugombana na kuachana kabisa, wenyewe wanasema wameumaliza mwaka vibaya.
Je, wewe ni mmoja wao? Basi leo ninataka kuongea na mwanamke aliyeachwa na mpenzi wake mwaka jana, nataka nimwambie kwamba kuvunjika kwa koleo siyo mwisho wa uhunzi na kuishi kwingi ni kuona mengi.
Dada yangu usikate tamaa na kujisikia vibaya baada ya kuachwa na mwanaume uliyempenda na kumthamini ndani ya moyo wako, kwani hiyo ni sehemu tu ya maisha ya mapenzi ambayo wengi wameyapitia.
Historia inaonesha kwamba wanawake wengi huishi kwa kutegemea wanaume na wengi wao wanaamini kuwa, hakuna maisha bila ya kuwa na mwanaume wa kumtegemea, hilo ni kosa kubwa sana kuliendekeza katika nafsi.
Nataka ujue kwamba, mwanamke ana kila kitu cha kuweza kumfanya ajiamini kwa kujijenga kiakili na kimaarifa zaidi ili kudumu katika penzi lake na hata kuweza kuyaendesha maisha ya mwanaume anayempenda.
Nasema hivyo kwa sababu mwanamke anakumbana na vizingiti vingi vya kumfanya asiweze kujiamini na hatimaye kusambaratisha penzi lake na mumewe au mwenza wake bila ya kutarajia.
Kizingiti cha kwanza siku zote huwa ni ndugu wa familia ya mwanaume, kwa ujumla, mwanamke anatakiwa kukwepa husuda na visa vya mawifi, mashemeji na hata wazazi wa mwanaume aliyepanga kuwa naye katika maisha ya ndoa.
Kingine mwanamke anatakiwa kuwaangalia mashoga zake na hata marafiki wa mwanaume wana mtazamo gani juu ya penzi lake na mwenza wake huyo.
Msomaji wangu, kama wewe ni mmoja wa waliokumbwa na visa katika uhusiano wako, bado una mambo mengi ya kufanya kuhakikisha kwamba penzi lako jipya linakuwa bora na kuweza kuimarika zaidi ili lisiweze kuvunjika kama lile lililopita.
Kumbuka vitabu vya dini vinasema kwamba mwanamke mpumbavu huivunja ndoa yake kwa mikono yake mwenyewe na mwanamke mwerevu huijenga ndoa yake kwa mikono yake, hivyo jukumu kubwa la ndoa yako liko mikononi mwako.
Kama umeachwa na mwenza wako au mumeo mwaka ulioisha wa 2010, sasa jipange kwa kuangalia mwaka huu 2011 unafanya nini kudumisha penzi jipya.
Awali ya yote jichunguze tabia zako, angalia ulikosea wapi katika kufanikisha mipango yako ya kudumu katika ndoa au uhusiano wako, hebu angalia tabia hizi, je unazo? Kama ndiyo jisahihishe na ujipange upya.
Kwanza hakikisha kwamba wewe ndiye unakuwa ‘steringi’ wa kuliongoza penzi lako na mwenzako kule unakotaka lielekee kwa kutumia masikilizano zaidi na maelewano ndani na nje ya nyumba.
Jipange jinsi ya kuongelea masuala ya ndoa yako, kwa kumtambua unayeongea naye ni nani kama ni mkwe, shemeji, wifi, shoga yako, jirani yako au mume hata kama ni mtarajiwa wako.
Usichonge sana
Hutakiwi kuwa muongeaji sana wa mambo yako na yale ya mwenza wako kwa watu wengine na pia usiwe mshadadiaji wa mambo mengine ya ndugu pale unapohadithiwa visa na mikasa yao.
Wanawake wengi huingia katika matatizo na familia kwa tabia zao za kuongelea mambo yasiyowahusu, hali hiyo huwafanya kuitwa majina mabaya katika familia za wanaume kwa kuonekana wambea, waongo na wazandiki.
Kuwa mpole, hata pale ukilazimika kuongea uwe mchaguzi mzuri wa maneno ya kuzungumza, yaani uwe unaongea kwa kutumia lugha nzuri na kwa mtazamo wa kushauri kwa ufasaha kuliko wa kiushabiki au kukosoa zaidi.
Uwe daraja la familia
Niliwahi kutoa usia katika sherehe ya ‘send off’ moja iliyomuhusu dada yangu mmoja, nakumbuka nilimwambia bibi harusi mtarajiwa kwamba, awe daraja zuri la muungano kati ya familia mbili, asiwe mtu wa kwanza kulivunja daraja hilo.
Unapoolewa mwanamke unatakiwa kuwa mtu wa kuunganisha familia mbili kwa kuwa wewe ndiye unayekwenda kuijenga nyumba nyingine ambayo inatakiwa ilindwe na amani, upendo na furaha ndani na nje ya nyumba hiyo.
Unatakiwa kuziunganisha familia hizo kwa shida na raha kwa kutoa ushirikiano wako wa ari na mali kwa kadiri uwezavyo.
Usiwe mtu wa kuanzisha mikasa, chokochoko au kuzua maneno ndani ya nyumba yako na familia kwa ujumla, bali uwe mtu wa mwisho wa kusimuliwa jambo lililotokea na wala usishadadie hata kama jambo hilo linahusu mtu wa familia ya mwanaume wako kuumbuka.
Usimuamini anayekusimulia na wala usiwe kimbelembele kwa kuongea kwa kulifurahia, bali sikitika na mtangulize Mwenyezi Mungu mbele katika kila sentesi yako unayoizungumza.
Tafuta kazi ya kufanya
Usikubali kuwa golikipa hata kama huna elimu, jitahidi kadiri uwezavyo kuepuka kukaa nyumbani huku ukipokea na kusambaza maneno. Tafuta kibarua kitakachokufanya uwe ‘bize’ na mambo ya msingi.
Unatakiwa uwe unajivunia mchango wako wa kuchangia maendeleo na mwanaume uliyenaye na siyo kukubali kukaa tu ndani huku ukingojea kupokea tu.
Ushinde moyo wa tamaa
Inawezakena ukatamani hata glasi au shuka kutoka kwa ndugu wa familia ya mumeo au mwanaume wako mtarajiwa, tafadhali nakusihi kaza moyo na wala usithubutu kuiomba kwani tabia hiyo ya kuombaomba inaweza kukusababishia matatizo makubwa.
Kama leo utaomba glasi na kesho ukaomba nguo kwa ndugu mwingine, ujue unajipalia makaa ya moto kwenye ndoa au uhusiano wako, utasemwa vibaya na kuchafuka katika familia hiyo na kuonekana hufai kuingia kwa tamaa zako zisizo na msingi.
Kwa muendelezo wa makala haya, tuonane tena wiki ijayo, nawatakia wasomaji wote heri ya mwaka mpya!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi ambaye anaandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Secret Love vilivyopo mitaani.
Mtembelee kwenye mtandao wake www.shaluwanew.blogspot.com
No comments:
Post a Comment