ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 12, 2011

Umeachwa 2010? Jipange upya 2011 sehemu ya pili

NAAM, karibuni tena katika safu hii ya Uwanja wa Huba, wiki iliyopita tulizungumza na dada zetu walioumaliza mwaka wa 2010 vibaya kwa kuachana na wenzawao. Niliwataka akina dada hao kujipanga upya kwa ajili ya mwaka huu wa 2011.


Katika makala hiyo nilizungumza mambo mengi ya kuyaepuka na kuwa makini ili kuweza kujipanga upya, nilimtaka mwanamke ambaye amechwa kuwa na mtazamo chanya wa maisha badala ya ule hasi ambao huwapoteza wengi.

Nilitaka mwanamke huyo kuangalia yale aliyoyakosea mwaka ulioipita na kujisahihisha kwa msimu huu ili aweze kudumu katika chaguo lake jipya.

Nawashukuru kwa wote waliojitokeza kuchangia mada hii kwa njia moja ama nyingine, dada zangu leo nitaendelea pale nilipoishia wiki iliyopita, kwa kuwapa misingi imara ya kuboresha mapenzi n wenza wenu wapya.
Nani wa kumpa nafasi?

Kama wewe umeachika lazima utakuwa unafikiria kuwa na mpenzi mpya, kwa mila na desturi zetu za Kitanzania ni vigumu kwa mwanamke kumfuata mwanaume na kumwambia kwamba unampenda na kuanza kumtongoza.

Hilo ni gumu kwani mara nyingi huwa linashusha thamani ya mwanamke na kumfanya aonekana ni kicheche, hivyo wanawake wengi huwa wanasubiri kutokewa na wanaume na wao kuwa na uamuzi wa mwisho wa kusema ndiyo au hapana.

Je, wewe umejiandaa kumkubali mwanaume wa aina gani? Au yeyote tu atakayejitokeza?

Mara nyingi wanaume husema dawa ya mwanamke ni mwanamke, yaani kama kuna mwanamke anawasumbua suruhisho lililo rahisi kwao ni kutafuta mwanamke mwingine haraka ili kuziba nafasi hiyo maisha yaweze kuendelea, wapo wanaume wanaochagua wanawake wa kuishi nao, wanawake wa kubuzibuzi nao na wanawake wa kustarehe nao.

Binafsi huwa sikubaliani na falsafa hizo za wanaume wenzangu, kwani mara nyingi huweza kumfanya mtu kuweza kuingia sehemu ambayo siyo sahihi.
Sasa hata wewe unaweza kukurupuka na kuingia katika uhusiano mpya bila ya kufanya tathimini ya kina, lengo linakuwa ni kuziba nafasi na si kumpata mtu muafaka kwenye nafasi hiyo.

Sasa dada yangu, kama ulifanya kosa awali usikubali tena kurudia kosa hilo kwa kuingia katika mtego mwingine wa  kujirahisha, kwani siyo kila mwanaume anayesema anakupenda anamanisha hivyo.

Katika hilo usimuamini kila mwanaume, kwani utajikuta ukipendwa na wanaume wengi na kujivinjari nao na mwishowe wakakuacha pabaya.
Usitake kutoa mkosi

Kwa hasira tu za kipumbavu mwanamke anaweza kuamua kuolewa baada ya kuachwa na  yule aliyempenda, kwa kuwa anakuwa hana  mtu wa kumuhakikishia kumuoa, hivyo anaamua kukubali kuolewa na mwanaume yeyote atakayejitokeza mbele yake na kumwambia kwamba anampenda na anataka kumuoa.

Hapana, kuwa na msimamo usikubali kuyumbishwa katika uhusiano wako, lakini usiingie katika mapenzi ‘kwa ilimradi’ tu uingie, kwani hujui Mwenyezi Mungu amekupangia nini katika maisha yako, hivyo usikate tamaa, jijengee tabia ya kujiamini kwamba unaweza kupata chaguo lako.

Katika hili la kujiamini, mwanamke unatakiwa kujihakikishia kwamba unaweza kuishi bila ya kumtegemea mwanaume ili kuepuka mapenzi ya ilimradi.

Mapenzi ya ilimradi huwa hayana tija wala mwelekeo wa maisha yako, vuta subira kwa ustahamilivu, unaweza kupata chaguo sahihi.
Usiende kwa mganga

Usijione kwamba una mkosi na kuamua kutaka kwenda kuanza tiba za kutupa vitu njia panda ili uweze kumdhibiti mwanaume, kwani mapenzi hayapatikana kwa waganga wa kienyeji.

Kuna wanawake wanaliamini sana jambo hili, kwamba unaweza kumpagawisha mwanaume kiasi cha kumfanya kuwa zuzu, yaanii hasikii wala haoni kwa mapenzi juu yako.

Wengi wanawadanganya wenzao kwa kuwapeleka kwa waganga ili waweze kumpata au kumtuliza mwanaume fulani, kwa imani zao wengine hudai kwamba wamekuwa wakifanikiwa, lakini penzi la aina hiyo huisha vibaya sana.

Napenda ufahamu kwamba mganga wa kwanza ni wewe mwenyewe kwa kile unachokifanya katika kujijenga, kujiamini na kukidhamiria kukifanya.

Mfano, usiwe kicheche cha mtaa, usiwe mgomvi kiasi kwamba mtaa mzima unajua kwamba fulani ni mgomvi au ugomvi wake hauishi,  jitunze na uwe na heshima katika jamii na fuata miongozo ya dini yako na utakuja kuvikwa chanda chema bila hata ya kutarajia.

Kumbuka wazee waliposema kwamba chanda chema huvikwa pete hawakukosea, waliona mbali kwa kujua kuwa mwanamke anayejitunza  na kuwa na heshima huweza kuwa na thamani kubwa mbele ya jamii.
Usikubali kuwa bidhaa

Wazazi wengi siku hizi wanapoletewa barua za posa za watoto wa wao wa kike huingiza tamaa za kutaka kutaja mahari kubwa ya kuweza kumkomoa mwanaume.

Hilo si sawa, mara nyingi wazazi hao humwita mtoto wao na kuanza kumuuliza kwamba mchumba aliyeleta barua kama anamfahamu, akijibu ndiyo wataanza kumuuliza ana nini?

Watataka kujua anafanya kazi wapi na ana nafasi gani kazini! Pia watataka anatoka katika familia ya akina nani ili kujua kama ana pesa au laa!  Na mambo mengine mengi yasiyo na msingi katika uhusiano wa kimapenzi.

Dada yangu, usiingie katika mkumbo huu, kumbuka pesa huwa haileti mapenzi bali mapenzi ndiyo huleta pesa, kwa maana kwamba wewe na mumeo mkiwa na mapenzi yenye neema ndipo Mwenyezi Mungu huweza kushusha neema zake.

Hivyo usikubali kubomoa pale unapotaka kujenga, waoneshe wazazi wako msimamo wako kwamba wewe si bidhaa ya kuuzwa kwa thamani kubwa na  mapenzi hayaweza kulinganisha na thamani ya kitu chochote.

Sidhani kama nina la kuongeza, ila naamini kama umenisoma vyema katika makala ya wiki iliyopita na hii ya leo, utakuwa  umepata jambo la msingi la kuweza kukusaidia katika maisha yako ya kumsaka mwenza mpya, asante
Hivyo jipange upya na uweze kuwa na maisha mema baada ya kumpata mpenzi mpya wa mwaka huu  wa 2011. Bado nawatakia heri ya mwaka mpya!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa mambo ya Mahaba ambaye anaandikia magazeti ya Global Publishers,  ameandika  vitabu vya True Love na Secret Love vilivyopo mitaani. Mtembelee kwenye www. Shaluwanew.logspot.com

No comments: