MWEKEZAJI mzalendo akishirikiana na wenzake wa ndani na nje ya nchi, amewasilisha mapendekezo ya mradi wa kuzalisha umeme wa upepo utakaofua megawati 100 kwa gharama nafuu kuliko umeme wa mafuta.
Mwekezaji huyo, Alex Lema, amesema kwa kushirikiana na kampuni za Norway na China, mradi huo utafua megawati hizo kwa mwaka, kwa gharama zisizozidi dola milioni 3.5 za Marekani sawa na Sh bilioni 5.1.
Lema alisema Dar es Salaam jana kuwa umeme huo ni nafuu maradufu kuliko wa mitambo ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL), aliyodai kuwa kwa mwaka inatoa megawati 100 kwa gharama za mafuta tu dola milioni 150 sawa na Sh bilioni 219.
“Nimechukulia mfano wa IPTL pekee, lakini tuna mitambo mingi kama huo, gharama za mafuta pekee kwa mwaka kuendeshea mtambo ni Dola milioni 150 sawa na gharama za ujenzi wa mtambo kamili kama huu wa upepo, ambao unazalisha kiwango sawa cha megawati 100, Serikali inaweza kunufaika na teknolojia hii ya upepo, kuliko inavyodhaniwa,” alisema Lema.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi ripoti ya upembuzi yakinifu wa mradi huo kwa Wizara ya Nishati na Madini, mwekezaji huyo alisema mradi huo unatarajiwa kuanza kutoa umeme nafuu katika Gridi ya Taifa mwaka 2014 na vifaa vya ujenzi vimeanza kupelekwa Makambako, Iringa.
Awali katika makabidhiano ya ripoti hiyo yaliyofanyika sambamba na uwasilishaji wa mada kuhusu namna mradi huo ulivyoanza, Lema pia alisema uzalishaji wa umeme huo utakapoanza baada ya makubaliano kufikiwa baina yake na Serikali, utapunguza uhaba wa umeme kwa asilimia 10.
Lema, ambaye ni Mwenyekiti wa Kampuni ya SinoTan Renewable Energy Limited yenye mradi huo, bila kutaja lini, alisema muda mfupi ujao, mazungumzo yatafanywa baina yake na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (EWURA) na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ili kuingia mkataba na kupewa idhini ya kuanza rasmi mradi.
Kwa mujibu wa mtaalamu na Meneja Mradi wa kampuni ya Norks Vind Energi ya Norway, Torstein Ekeon, ujenzi wa mradi utafanyika kwa miezi 16 kuanzia Septemba 2012 na hadi Julai 2013 megawati ya kwanza itazalishwa kabla ya megawati zote 100 kukamilika Februari 2014.
Mtaalamu huyo alisema kwa sasa baadhi ya vifaa vya ujenzi vimepelekwa eneo la mradi lenye ukubwa wa ekari 500 na wanatarajia uzalishaji utaongezeka zaidi kwa kuwa upepo wa eneo hilo hauyumbi wala kubadilika.
Kwa mujibu wa Ekeon, upepo wa kuzalisha umeme katika eneo hilo ni mzuri kuliko kote iliko miradi ya aina hiyo duniani, ikiwamo ya Urusi, Bulgaria, Norway na nchi kadhaa za Afrika ambazo hakuzitaja.
Hata hivyo gharama za Tanesco katika kununua umeme huo utakapoanza kuingia kwenye Gridi, hazijafahamika, kwa kuwa bado mazungumzo ya mwisho hayajahitimishwa, lakini taarifa na makubaliano ya awali zinaonesha ni senti nane za dola (sawa na Sh 1,168) kwa kilowati.
Kaimu Kamishna wa Nishati wa Wizara ya Nishati na Madini, Hoseah Mbise aliyepokea ripoti hiyo, alikiri kuwa teknolojia ya upepo ni ukombozi wa tatizo la nishati nchini na duniani.
Alisema lengo la Serikali ni kushirikiana na kampuni kama hizo kuhakikisha kuwa umeme unaifikia jamii kwa gharama nafuu.
“Uzalishaji wa upepo ni suluhisho ya tatizo la umeme si tu hapa nchini, bali hata kwa mataifa mengine kama Kenya, Norway, China na India, ambao wako mbali pia, lengo ni kufikisha zaidi ya megawati 1,000 mwaka 2015 na zaidi ya megawati 6,000 mwaka 2033,” alisema Mbise.
Kwa mujibu wa Lema, kampuni ya China MCC 20- Hainan International inamiliki asilimia 14 ya hisa za mradi huo, Norks Vind Energi asilimia 50 na wawekezaji wa ndani asilimia 36.
Kampuni hiyo itakayoajiri wafanyakazi wa kudumu kati ya 20 na 30, ilianza mwaka 2004 nchini ikiwa ni kampuni ya kizalendo ikifanya utafiti katika wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa Lema, kutokana na upepo usio imara katika wilaya hiyo, walihamishia utafiti wa mradi huo Makambako mwaka 2006. Tangu hapo upembuzi yakinifu na utafiti umekuwa ukifanywa hadi mwaka jana.
Hatua ya kampuni hiyo imekuja siku moja baada ya taarifa za kampuni nyingine ya Sichuan Hongda ya China kuanza mazungumzo na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kuhusu kuzalisha umeme wa makaa ya mawe wa megawati 600 utakaoingia katika Gridi ya Taifa.
Kwa sasa, Tanzania inahitaji megawati 900 za umeme wakati katika hali ya kawaida uzalishaji ni megawati 773.
Ikiwa kampuni hizo zitaingiza umeme huo wa megawati 600 za makaa ya mawe na megawati 100 za upepo, Tanzania itakuwa na megawati 1,400 za umeme na ziada ya megawati 500.
Chanzo:HabariLeo
No comments:
Post a Comment