
Zingatia; Inawezekana mwenzi wako hakwambii lakini ukweli usimame kwenye kipimo chake kwamba anahitaji manjonjo yako ili afurahie penzi. Kama humtekelezei, tambua anaumia kwa sababu unabana.
Kauli ya Justin kama nilivyomnukuu kwenye makala haya toleo lililopita, inaweza kuwa fundisho kwako kwa sababu wengi wamejikuta wakipoteza mvuto wao, kisa ni vitu vidogo.
Hii ndiyo sababu ya kumtaka kila mmoja kuzingatia yale ambayo mwenzi wake atakuwa anapenda na kutekeleza kwa kiwango bora ili kumridhisha. Sanaa ya mapenzi kama ambavyo nimekuwa nikipigania kuisambaza siku zote, inamtaka mtu kuishi ndani ya mwenzake.
Kuugua kwa maumivu, kuhuzunika katika majonzi na kufurahia palipo na sherehe.
Ni kituko mwenzi wako anaumia wewe unacheka. Yupo kwenye maumivu makali, wakati huo kwa upande wako ni chereko kwa kwenda mbele.
Aina hii ya maisha haiwezi kuwa sawa na haikubaliki. Unapaswa kumjali mpenzi wako hata kama haikugusi lakini machoni muoneshe kuwa upo pamoja naye, vinginevyo ni mateso kwake.
Katika mapenzi, ogopa wewe na mwenzi wako kutofautiana kihisia. Falsafa ya mapenzi haifundishi ugumu wala haielekezi ubinafsi, inatoa mwongozo katika wawili kuwa kitu kimoja. Hii ina maana kuwa unapolazimisha kwenda kinyume na mwenzako, unakuwa unaonesha kiwango cha chini cha ufahamu katika mambo ya ‘malavidavi’.
ANGALIA USIPITWE NA WAKATI
Kwa kawaida, mtu ambaye ni mjanja wa mapenzi anabaki kuwa namba moja katika kuhakikisha hapitwi na wakati.
Ikiwa hujali hisia za mwenzi wako, wewe utaonekana wale wale. Badilika leo na uzichange karata zako vizuri, mwenzi wako anakuhitaji, anataka ukweli wako, kujali kwako, huruma yako na anapenda sifa zake njema zitamkwe na kinywa chako.
Mwanasaikolojia Born Lewis wa Marekani katika makala yake “Your Sentimental and True Love” anasema: “Inakuhitaji uwe mwelewa zaidi wa hisia za mwenzako ili uweze kudumu. Mfano;
Msome na ujue kwamba anahitaji kusifiwa halafu umsifie. Akienda kupewa sifa na mtu wa pembeni atajua humkubali. Hilo ni kosa kubwa katika mapenzi.”
Lewis anafafanua: “Ni kosa kubwa kwenda kumpongeza mfanyakazi mwenzako kwa muonekano wake, wakati hujafanya hivyo kwa mpenzi wako nyumbani.
Ukitaka kujua kwamba inauma, fikiria mwenzio amekuona ulivyovaa na hakukwambia kitu lakini unapata taarifa kuwa amemsifia jirani yenu. Itakuuma, itakupunguza imani yako kwa mwenzi wako.”
Sherry na Mosses ni wapenzi lakini hata siku moja Sherry hajawahi kuonesha kwamba anamkubali Mosses ingawa penzi lao linazidi kuvuta miaka.
Ilivyo ni kwamba mara nyingi ni Mosses ndiye huonesha hisia zake kwa Sherry na hata marafiki zao hufikia kusema kwamba jamaa ndiye anayesababisha uhusiano wao uendelee kuwepo, vinginevyo wangekuwa wamekwishapigana mwereka.
Sherry anapoambiwa amependeza anajibu ‘asante’ halafu imetoka. Akiambiwa yeye ni mwanamke mzuri jibu ni ‘thank you’.
Hathubutu kumwambia Mosses kuwa amependeza au ni mwanaume anayemvutia kuliko wote, ila akiwa kazini kwake, pongezi huzimwaga huko. “James umependeza!” Sherry anamwambia mfanyakazi mwenzake.
Wakati mwingine Sherry anakosa hekima, anamueleza Mosses: “Unajua sisi pale kazini kwetu kuna vijana wazuri. Unajua Jamal ana sura nzuri sana? Halafu Sam anajua kupigilia mavazi ukimuona hadi raha.”
Inawezekana Sherry anazungumza kweli lakini kichwani kwake kuna kelele za ndani (internal noise) zinazomsababishia umapepe, hivyo kukosa busara ya kuchagua maneno mbele ya mpenzi wake.
Ukitaka kujua mkuki kwa nguruwe, siku moja Sherry alikutana na Zawadi ambaye ni mfanyakazi mwenzake Mosses. Zawadi akaamua kuwa mkweli:
“Mosses nimemuacha ofisini ila kanifurahisha, amenisifia huyo. Anasema nimependeza sana leo.” Ilikuwa ni kama Zawadi kamroga Mosses kwani Sherry alikasirika mno siku hiyo.
Walipokutana nyumbani, Sherry alitaka maelezo ni kwa nini alimsifia Zawadi kwamba amependeza badala ya sifa hizo kuzielekeza kwake.
Mosses akaona mpenzi wake anampanda kichwani, akamjibu: “Mbona wewe huwa unawasifia wanaume wa kazini kwako mimi sisemi, tena mbele yangu.” Sherry ikamgonga kichwani, akapata pointi!
Sherry hakujua kwamba sifa alizokuwa anazimwaga kwa wanaume wa kazini kwake ilikuwa sawa na kuchezea hisia za Mosses.
Haikumgonga kichwani kwamba anamuumiza mwenzake. Alipokutana na Zawadi ikawa maumivu kwake. Kila mtu anatakiwa kujali, kusifu kwa sababu hivyo ni vionjo muhimu kwenye mapenzi.
Kama hukubali kwa jinsi mwenzi wako alivyo, ni bora kuachana naye kuliko kupotezeana muda. Tambua kuwa usipomsifu wewe anapokwenda atasifiwa halafu ukisikia itakuuma. Wewe humuelezi kama ni mzuri, anakokwenda wapo watakaomuona na kumwambia anavutia.
Je, hapo huoni kama utakuwa umepoteza kura kwa mwenzi wako?
Zaidi ya hayo, kuna vipengele vifuatavyo vya kuzingatia:
ITAKUONGEZEA MVUTO
Ukiwa unamjali na unamsifu, atajua unamkubali kwa jinsi alivyo. Hii itakuongezea ‘maksi’ za kuzidi kukupenda.
UTABORESHA PENZI
Pengine huko alikokuwa hakuwahi kumwagiwa sifa. Ukimjali na kumuonesha jinsi unavyomkubali kwa kumtamkia na vitendo, itamfanya akuone wewe ni mteule uliyeletwa na Mungu kwake. Atakupenda zaidi.
ITAMJENGA KUJIAMINI
Ukimwambia yeye ni mzuri na unampenda sana. Ukimsifia kwa mavazi yake na muonekano wake kwa jumla, itamfanya ajiamini. Hatokuwa na shaka yoyote juu yako. Hata akipita barabarani atajiona yupo kamili. Atakuheshimu!
INAPUNGUZA UWEZEKANO WA KUKUSALITI
Kuna watu husalitiwa siyo kwa sababu ya kuona wazuri pembeni, ila kwa tabia zao. Wewe hata siku moja humuoneshi kama unamjali, wala humwambii kuwa anavutia. Matokeo yake anakutana na mtu pembeni anayejua kumwaga sifa, anaanza kumuona bora kuliko wewe.
Anamjali na anamsifia kwamba ni mzuri, akivaa anamueleza anavutia. Wewe na ububu wako au uchoyo wa pongezi atakuacha. Atadandia gari la mtu anayejua nini maana ya mapenzi na anayefahamu jinsi ya kucheza na hisia.
Hivyo basi, ukimjali na kumwagia pongezi inavyotakiwa, uwezekano wa yeye kukusaliti utapungua.
UTAKITEKA KICHWA CHAKE
Atake nini tena? Kama ni kujali, wewe unamjali sana, sifa anazipata za kutosha kutoka kwako kwa hiyo hatokuwa na shaka yoyote juu yako kwa maana utakuwa umemteka kwa kiwango cha kutosha.
No comments:
Post a Comment