ANGALIA LIVE NEWS

Friday, January 14, 2011

Wachezaji Kongo wawaponda Stars


TAIFA Stars leo inajitupa uwanjani kuwania nafasi ya tano katika michuano ya Nchi za Bonde la Mto Nile, huku wachezaji wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wakisema ilistahili kucheza nusu fainali, lakini wachezaji wake wamejaa utoto mwingi na hawajali kazi. 

Stars inalazimika kuwania nafasi ya tano ambayo zawadi yake ni zaidi ya Sh milioni 40 za Tanzania, ili angalau itoke mrisi katika mashindano hayo, baada ya Jumanne kutoka sare ya bao 1-1 na Uganda 'The Cranes' hivyo kuishia
kushika nafasi ya tatu Kundi A na leo itacheza na Sudan ambayo imeshika nafasi ya tatu Kundi B. 

Bingwa wa mashindano hayo atazawadiwa zaidi ya Sh milioni 200 za Tanzania. 

Mchezo huo wa Stars utaanza saa 9:45 kwa saa za Afrika Mashariki, kisha utafuatiwa na ile ya nusu fainali, ambapo DRC itacheza na Uganda na baadaye Misri na Kenya yote ikifanyika mjini Ismailia, umbali wa saa 1:30 ama saa mbili kwa gari ndogo kutoka jijini Cairo. 

Wakizungumza juzi baadhi ya wachezaji wa DRC walieleza kuwa Stars ina wachezaji wenye vipaji, lakini wasiojua kazi na hawauchukulii mpira kwa uzito unaostahili. 

"Nimeona mechi za Tanzania, wachezaji wanapoteza pasi halafu hawajali wanafungwa goli wanatabasamu, hiyo inatakiwa iwe kwenye mechi za kujifurahisha Tanzanua lakini si hizi za kuwania zawadi kubwa. 

"Unafungwa bao tano hata kadi ya njano hupewi kwa kucheza rafu angalau kupunguza kasi yao, Vijana wenu wamejaa utoto mwingi sana, hawajui thamani ya mpira," alisema kiungo Kasongo Ngandou, ambaye pia huchezea klabu bingwa ya Afrika TP Mazembe. 

Mchezaji mwingine wa DRC ambaye ni nahodha wa TP Mazembe, Mihayo Kazembe naye aliisikitikia Stars kwa kusema namna alivyoona viwango vya timu mbalimbali katika mashindano hayo, Stars ilitakiwa icheze nusu fainali, lakini wachezaji wenyewe hawakutilia mkazo. 

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen yeye alizungumzia kushindwa kufuzu nusu fainali kwamba kulitokana na wachezaji wake kukosa umakini hasa katika ulinzi na ufungaji, wakati baadhi ya wachezaji wake walipoulizwa kuhusiana na kauli kwamba timu imejaa utoto walitofautiana katika majibu. 

"Kila mtu ana mtazamo wake, sidhani kama ni sahihi haya yaliyosemwa, wote tunajua thamani ya mpira," alisema nahodha wa Stars, Shadrack Nsajigwa. 

"Ni kweli timu yetu ina utoto mwingi, tunapaswa kubadilika," alisema mmoja kati ya wachezaji mahiri lakini alitaka jina lake lisitajwe. 

Mechi zote leo zinatarajiwa kuwa na msisimko wa aina yake, ambapo ya Stars na Sudan licha ya kuwa zinawania nafasi ya tano, lakini kikubwa ni kutaka zawadi, ndiyo maana wachezaji wa Stars wameahidi kupambana ili kushika nafasi hiyo. 

Pia mchezo wa Misri na Kenya na ule wa Uganda na DRC nayo inatarajiwa kuwa ya vuta nikuvute, kikubwa ikiwa ni kila moja kuhakikisha inaingia fainali ya michuano hiyo. 

Mchezo wa fainali utafanyika Jumatatu. 

Wakati huohuo, wachezaji wawili wa Taifa Stars, Nizar Khalfan anayechezea Vancouver Whitecaps na Idrissa Rajabu anayechezea Sofapaka ya Kenya walitarajiwa kuondoka jana usiku jijini hapa kurejea Dar es Salaam ili waende kwenye timu zao. 

Ofisa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Idd Mshangama aliyepo na Stars mjini hapa alisema kulikuwa na makubaliano na klabu zao kwamba wanatakiwa wawe wamefika kabla ya Januari 15, mwaka huu.

No comments: