WASOMI nchini wametakiwa kuitumikia jamii bila ya kuonesha dharau katika mila na desturi za watu kwa kuwa elimu si kibali cha kudharau mila, desturi na utamaduni.
Mwito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kanisa la Moravian Tanzania, Mchungaji John Italazyo, kwenye mahafali ya mafunzo ya falsafa ya dini na wahitimu wa kidato cha sita katika seminari ya Lusangi mjini Sikonge.
Alisema wapo wasomi wengi duniani ambao jamii zao zimewakataa licha ya kwamba wasomi hao wanaelimu ya kutosha kwa sababu tu wamejisahau na kufikiri elimu waliyoipata ndiyo jibu la kila kitu na kutotumia busara na hekima walizopewa na Mungu.
Mchungaji Italazyo alisema baadhi ya wasomi wamekuwa wakiishi bila kukubalika katika jamii zao kutokana na kushindwa kushirikiana na kuwaheshimu watu katika mila, desturi na utamaduni na kuwa kikwazo cha maendeleo.
Naye Mkuu wa seminari ya Lusangi, Mchungaji Sylivester Katikaza, ameilalamikia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kutoweka mfumo unaoendana na hali halisi wa kujiunga na kidato cha tano na kusababisha vijana wengi kushindwa kuendelea na masomo ya elimu ya juu.
Alisema pamoja na vijana kushindwa kupata elimu bora, pia taasisi zisizokuwa za kiserikali nazo zinashindwa kumudu gharama kubwa za kuendesha shule kwa sababu zinapata wanafunzi wachache wenye kukidhi viwango.
Aliishauri serikali iangalie upya mabadiliko hayo ya kujiunga na elimu ya kidato cha tano kwa sababu yanaweza kuleta udumavu katika sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya umma.
Chanzo:Habari Leo
No comments:
Post a Comment