Azam waliocheza kwa zaidi ya nusu saa wakiwa wamebaki 10 uwanjani baada ya kiungo wao Ibrahim Mwaipopo kutolewa kwa kadi nyekundu, walikwea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Bara kufuatia ushindi wa 2-0 dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam jana.
Mwaipopo aliifungia Azam goli la kwanza katika dakika 42 lakini alitolewa kwa kadi nyekundu na mwamuzi Oden Mbaga wa Dar es Salaam katika dakika ya 57 baada ya kumchezea rafu kiungo wa JKT, Nashon Naftari.
Licha ya kubaki 10 uwanjani, Azam walipata bao la pili katika dakika ya 72 lililotokana na beki wa JKT, Stanley Nkomola kujifunga wakati akijaribu kuokoa mpira wa kona iliyopigwa na beki Ibrahim Shikanda.
Kwa ushindi huo, Azam imeshika usukani wa ligi baada ya kufikisha pointi 35, sawa na Yanga iliyo katika nafasi ya pili. Tofauti nzuri ya magoli inaiweka juu Azam, ambayo imecheza mechi moja zaidi. Simba yenye pointi 34 iko katika nafasi ya tatu, ikiwa na mechi mbili mkononi.
Jijini Mwanza, Toto African walivuruga sherehe za AFC za ushindi wa mechi mbili mfululizo kwa kuichapa timu hiyo ya Arusha kwa magoli 2-1, wakati mjini Dodoma, wenyeji Polisi waliifunga timu inayochechemea ya Majimaji kwa magoli 3-2 kwenye Uwanja wa Jamhuri.
Mpira ulianza kwa kasi kwenye Uwanja wa Uhuru na JKT walihitaji sekunde 30 tu kupeleka hatari ya kwanza langoni kwa Azam wakati Bakari Kondo alipomtengea pasi safi Haruna John katika eneo la hatari lakini beki wa Azam Luckson Kakolaki alifika haraka na kuondoa hatari.
Azam walijibu kwa shambulizi kali katika dakika ya 6 kufuatia gonga safi baina ya Mrisho Ngassa, Ibrahim Shikanda na Ramadhani Chombo 'Redondo' lakini nyota wa zamani wa Simba, Redondo alipiga "shuti-mtoto" lililoishia mikononi mwa kipa wa zamani wa Taifa Stars, Shaaban Dihile wa JKT.
Kipa wa JKT, Dihile alifanya kazi ya ziada kuokoa mashuti kutoka kwa nyota wa Azam akiwemo Mrisho Ngassa, lakini hakuwa na ujanja wakati Mwaipopo alipofumua shuti la mbali lililokwenda wavuni wakati mabeki wakidhani anatoa krosi katika dakika ya 42 na katika dakika ya 72 wakati Nkomola alipojifunga.
Cosmas Mlekani anaripoti kutoka Mwanza kuwa; timu ya Toto ilijiimarisha katika nafasi ya 7 ya msimamo kwa kufikisha pointi 20 kufuatia ushindi wa 2-1 dhidi ya AFC kwenye uwanja wa CCM Kirumba katika mechi ambayo wageni wangeweza kupata sare kama mfungaji bora wa zamani Abdala Juma asingepaisha penalti katika dakika ya 33.
Hussein Swed aliitangulia kuifungia Toto goli la kwanza katika dakika ya 37 na Sammy Kessy aliongeza la pili katika dakika ya 59 kwa shuti la mbali.
AFC walipata penalti katika dakika 78 wakati beki wa Toto, Laban Kambole alipotolewa kwa kadi ya pili ya njano kwa kufanya madhambi ndani ya eneo la hatari, lakini Abdala Juma alishindwa kufunga kabla ya kurekebisha makosa yake dakika nne baadaye kwa kufunga goli la kufutia machozi.
Jacqueline Masano anaripoti kutoka Dodoma kuwa wenyeji Polisi walishinda 3-2 kupitia kwa magoli ya Juma Semsue (dk.19), Keneth Masumbuko (dk.40) na John Kanakamfumu (penalti dk.58) huku magoli ya Majimaji yakifungwa na Kulwa Mobu (dk.28) na Ulimboka Mwakingwe (dk.44)
Vipigo vya jana vimeongeza "maisha magumu" kwa AFC na Majimaji zilizobaki mkiani mwa ligi kwa pointi 11 kila moja, tofauti nzuri ya magoli ikiiweka Majimaji juu.
Vikosi katika mechi ya Azam na JKT Ruvu vilikuwa:
Azam: Jackson Chove, Ibrahim Shikanda, Malika Ndeule, Aggrey Morris, Luckson Kakolaki, Ibrahim Mwaipopo, Ramadhan Chombo 'Redondo'/Jamal Mnyate (dk.68), Mrisho Ngassa, Jabir Aziz, John Bocco 'Adebayor'/ Peter Ssenyonjo (dk.57), Himid Mao/Salum Aboubakar (63).
JKT Ruvu: Shaaban Dihile, Kessy Mapande, Stanley Nkomola, Shaibu Nayopa, Damas Makwaiya, Nashon Naftari, Haruna John, Mwinyi Kazimoto, Bakari Kondo/Pius Kisambale (dk. 64), Hussein Bunu, Sostenes Manyasi/Amos Mgisa (dk.51).
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment