ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 21, 2011

Paka aua binadamu

Tukio lisilo la kawaida limetokea mkoani Shinyanga, baada ya mkazi wa kitongoji cha Mshikamano, Kata ya Ndembezi, Manispaa ya Shinyanga, Modesta Bundala (45), kufa kwa kung’atwa na paka anayehisiwa kuwa ana kichaa.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, Modesta ambaye alifariki dunia Feb. 16, mwaka huu, aling’atwa na paka wa jirani yake wakati akitoka kuteka maji jirani na nyumbani kwake hivi karibuni.

Walisema alipotoka kuchota maji na kukaribia nyumba yake, ghafla alitokea paka na kumrukia mguuni kisha kuanza kumng’ata, hali iliyomfanya Modesta kupiga kelele za kuomba msaada.
Waliongeza kuwa baada ya kelele hizo za kuomba msaada, majirani walifika eneo la tukio kujaribu kumwondoa paka huyo kwa kumfukuza, lakini aliendelea kung'ng'ania mguu wa mwanamke huyo.
Walisema baada ya kuona hivyo, mmoja wa majirani wa Modesta alikwenda kuchukua nyundo ndani kwake na kumpiga kichwani na ndipo paka huyo alipoachia mguu huo na kufa papo hapo.
“Ilitubidi tumpige paka huyo kwa nyundo kumnusuru jirani yetu, tulimtwanga nyundo ya kichwa ndipo akaachia mguu wa mama huyo na kufa,” alisema mmoja wa majirani hao.
Hata hivyo, ilielezwa kuwa pamoja na kung’atwa na paka, mama huyo alipuuza kwenda kupata tiba hospitalini kutokana na jeraha alilopata.
Akisimulia mkasa huo, mume wa Modesta, Jilala Mipawa, alisema baada ya mke wake kung’atwa na paka huyo waliona ni jambo la kawaida tu, lakini siku tatu kabla ya kifo chake, Modesta alitokwa na upele mwili mzima na kujikuna sana, kucheka cheka hovyo huku akipiga kelele za kuchekesha na kuonyesha dalili zote za kuchanganyikiwa.
Alisema mbali na kupiga kelele, alikuwa akitapika mfululizo hali ambayo iliwapa wasiwasi na hivyo kuamua kumkimbiza katika hospitali ya serikali mkoani Shinyanga ili kupatiwa matibabu.
Hata hivyo, alisema mkewe alifariki dunia Februari 16, mwaka huu.
Ofisa Mdhibiti wa Magonjwa ya Mifugo katika Manispaa ya Shinyanga, Varen Mwaluko, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo alisema hata ofisi yake ilipatwa na mshtuko mkubwa kutokana na paka kusababisha kifo cha binadamu.
Alisema baada ya tukio hilo, tahadhari kubwa imetolewa kwa wananchi walioshiriki kumuuguza hadi kifo mama huyo kwani huenda walimshika bila tahadhari na hata kujikuta wakipata majimaji kutoka sehemu mbalimbali za mwili wake.
Aliongeza kuwa kuanzia kesho (leo) timu ya wataalamu inakwenda kuanza kuwachanja paka na mbwa wote walioko katika eneo hilo na amewataka wananchi wengine wenye dalili kama hizo kufika mara moja katika hospitali ya mkoa ili waweze kupatiwa chanjo ya kujikinga na kichaa cha mbwa.
Tukio hilo liliwashangaza wengi kwani ni nadra mno paka kumshambulia binadamu kwa kumuuma meno na mara nyingi hutumia kucha kwa kuparura tu.
CHANZO: NIPASHE

No comments: