Na Gladness Mboma
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetembelea na kuwafariji majeruhi wa ajali ya milipuko ya mabomu iliyotokea Februari 16 katika
kambi ya 511 KJ Gongolamboto waliolazwa katika Hospitali ya Amana, Dar es Salaam.
Mbali na kuwafariji chama hicho pia kimetoa msada wa dawa yenye thamani ya zaidi ya sh. 600.000 na shuka 166.
Ziara hiyo ya wabunge na viongozi mbalimbali wa CHADEMA iliongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho Dkt. Willibrod Slaa pia walikwenda kuaga miili ya familia moja ya watoto na mke wa Bw. Jacob Nyajiego waliofariki kwa milipuko hiyo.
Akikabidhi msaada huo wa madawa, Dkt. Slaa alisema kuwa CHADEMA wameguswa na matatizo hayo yaliyowakumba Watanzania wenzao na kwamba dawa walizotoa zinaendana na mahitaji halisi.
Dkt. Slaa alisema kuwa wakati walipokuwa katika Hospitali ya Amana walielezwa kwamba kuna upungufu wa mashuka na kwamba leo watapeleka mashuka 166 kwa ajili ya kuwasaidia majeruhi.
"Kesho asubuhi tutapeleka mashuka 166 kwa sababu tumeelezwa kwamba kuna upungufu wa mashuka na tutamkabidhi Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana,"alisema.
Alisema kuwa msaada wa dawa na mashuka yote wataelekeza katika Hospitali ya Amana ambako walitembelea na watendelea kutoa msaada zaidi pale itakapowezekana.
Wakati huo huo kampuni, taasisi mbalimbali zimeendelea kutoa misaada mbalimbali ikiwemo vyakula nguo, mahema kwa wathirika wa mlipuko wa mabomu hayo.
Akitoa msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya sh. milioni saba. Mkurugenzi wa Kampuni ya Uwakala wa Dalali wa Mahakama ya Yono Auction Mart, Bi. Scholastica Kevela alisema kutokana na tukio hilo imeguswa na janga hilo.
Bi. Kevela alisema kuwa kampuni hiyo inafanya kazi na jamii, hivyo ni wajibu wao kusaidia jamii kupitia janga hilo kwa hali na mali.Nao Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) kupitia Shirikisho la Vyuo Vikuu Dar es Salaam walitoa msada wa sh. 400,000 kwa ajili ya kusaidia majeruhi hao na waathirika wa mlipuko huo.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi fedha hizo Mwenyekiti wa tawi wa shirikisho hilo, Bw. Kusekelo Melson alisema kuwa fedha hizo zimepatikana baada ya kuchangishana.
Taasisi zingine ambazo zimetoa misaada mbalimbali vyakula na nguo ni ni Jumuiya ya Memon, Taasisi ya dini ya kisabato kutoka Tabata Kisukulu, Hindu Mandal na Lions Club ya Dar es Salaam
Akizungumza baada ya kupokea misaada hiyo Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Said Meck Sadick alisema kuwa misada yote hiyo itakusanywa sehemu moja kwa lengo la kuhakikisha kwamba inawafikia wathirika wote.
"Michango yote ambayo inatolewa na wahisani na wasamaria wema tungependa ipitie katika mkondo mmoja ili uthibiti uweze kuwa mzuri na pasiwepo na malalamiko,"alisema.
Alisema kuwa wao ndio wanaojua waathirika wa mabomu hayo waliko na kusisitiza kwamba misaada yote hiyo itawafikia ambapo alitoa wito kwa wasamaria na taasisi nyingine kujitokeza kutoa misaada hiyo.
Naye Laurent Samatta naripoti kuwa Kampuni ya Mariedo inayojihusisha na mavazi imekabidhi misaada ya vyakula,nguo na maji kwa watoto waliyo athirika na milipuko ya mabomu
yenye thamani ya sh. milioni 3.
Akikabidhi msaada huo jana Mkurugezi wa kampuni hiyo, Bw. Edward Amri, alisema kwa upande wao wamepokea maafa hayo kama janga la kitaifa ambalo linahitaji huruma za kila Mtanzania kusaidia waathirika.
Alisema wataendelea kutoa misaada kwa watoto hao hadi pale serikali itakapo wapatiwa makazi ya kudumu ikiwa sambamba na kukutana na wazazi,ndugu au walezi wao.
Alisema kampuni yao ilikuwa inajihusisha na utoaji misaada kwa yatima na wamepanga kuongeza bajeti yao ili kufanya kazi kwa umakini ya kuwafikia walengwa wakuu.
CHANZO:MAJIRA
No comments:
Post a Comment