ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, February 19, 2011

Dk Mwinyi, Mwamunyange Waonja adha ya umeme

Joseph Zablon
MSAFARA wa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk  Hussein Mwinyi na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, wameonja adha ya mgawo wa umeme baada ya kukwama kwenye lifti kwa muda wa zaidi ya dakika nne, kufuatia kukatika umeme. 

Adha hiyo iliwakuta wakati walipokwenda kuwajulia hali watoto wawil,i ambao wamelazwa wodi zilizopo ghorofa ya tatu jengo la wodi ya watoto.


Dk Mwinyi baada ya kupokelewa, aliongozwa hadi kwenye jengo hilo na kufunguliwa lifti ambayo walipanda na msafara wake, baada ya milango kujifunga na kabla safari haijaanza umeme ulikatika.

Hali hiyo ilizua kizazaa cha muda na askari na maofisa wengine waliokuwa nje, walianza kuwasiliana na wenzao waliotangulia na Dk Mwinyi na Mwamunyange.

Maelekezo yaliyotoka kwa baadhi ya wauguzi ni kuwataka wasome namba ambazo zipo ndani ya lifti, hivyo askari hao waliwapigia simu wenzao waliokuwa na waziri na kuwapa maelekezo. Waliwapigia simu mafundi ili kwenda kuwasaidia.
"Someni namba hizo zilizopo hapo pembeni karibu na hivyo vitufe tuwapigie simu," alisema muuguzi mmojawapo jirani na mlango.

Wakati hekaheka za kuwasaka mafundi zikiendelea, ghafla mlango ukafunguka na haikujulikana ni njia iliyotumiwa na waziri aliyekuwa amevaa koti alitoka nje akiwa amelishika mkononi huku akijifuta jasho.

Kutokana na kadhia hiyo, ilibidi Waziri Mwinyi na Jenerali Mwamunyange kutumia ngazi kwenda kuona majeruhi hao, walimkuta mtoto moja na mwingine tayari alikuwa ameruhusiwa.

Waziri na msafara wake waliendelea na ziara yao wodi zingine, ikiwamo Mwaisela na Kibasila na kuzungumza na waathirika wa mabomu na baadhi ya madaktari wamelalamikia kuhusu mgawo wa umemu hospitalini hapo.

"Kipindi hiki cha janga kama hili sioni logic (msingi) ya kuendelea kwa mgawo hata kwa hospitali ya Taifa, pengine kutokana na kilichompata waziri kuna kitu watajifunza," alisema daktari mmojawapo ambaye hakutaka kutajwa.

Daktari mwingine hospitalini hapo, alilalamikia hali hiyo kuwa inachangia vifo vya majeruhi na wagonjwa wengine, kwani madaktari wapo na wanataka kufanyakazi lakini wanatatizwa na ukosefu wa umeme.

No comments: