Na Florence Majani
NIPO katika basi la abiria nikielekea Gongo la Mboto ambako maafa yametokea baada ya makombora katika ghala la kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kulipuka.Ninapofika nawakuta wakazi wa hapa wengi wakiwa bado wana wasiwasi, wengine wengi wakiwa wanachechemea na baadhi wakiwa wanaokoteza mabaki ya mali zao baada ya nyumba zo kuungua au kubomolewa na makombora yaliyolipuka usiku wa kuamkia juzi.
Nazungumza nao na kwa nyakati tofauti wakazi hawa wanatoa usemi ambao unawiana, kuwa wameona miujiza.
Wanasema, pamoja na makombora hayo kuacha misiba katika nyumba na familia kadhaa, kusababisha uharibifu mkubwa wa makazi na hata baadhi ya ndugu hasa watoto wadogo kupotezana, lakini wao walikuwa wakikoswa koswa kwa karibu kabisa na makombora hayo na wengine wanakiri kwamba kifo kiliwakosa sentimita chache au ilikuwa chupuchupu.
Kichanga kilichokoswa na bomu kitandani
Wengi husema kuwa watoto ni malaika wa Mungu. Naam ipo miujiza kadha wa kadha ambayo wakazi wa Gongo la Mboto hawataisahau, achilia mbali madhara yaliyotokana na milipuko ya mabomu. Miongoni mwa miujiza ambayo Mungu ameionyesha katika maafa hayo, ni kupona kwa kichanga cha miezi sita.
Makobora matatu yanayokadiriwa kuwa na urefu wa mita tatu na nusu kila moja, yalitua ndani ya chumba kilimokuwa kimelezwa kichanga hicho na moja ya makombora hayo kujikita katika kitanda ambacho alilala kchanga huyo, malaika wa Mungu. Chumba na hata kitanda viliwaka moto kutokana na kulipuka kwa makombora hayo, lakini hii leo kichanga hikipacha, kinachojulikana kwa jina la Kulwa mbali na kupata majeraha madogo madogo kiko hai.
Nazungumza na mama mkubwa wa kichanga hicho, Adia Roki mkazi wa Gongo la Mboto, Mzambarauni, ambaye anasema, siku ya tukio wakiwa hawana hili wala lile, mdogo wake, Rose Roki, mwenye watoto pacha alikuwa nje na Doto wakati Kulwa alikuwa amelala ndani.
“Mdogo wangu ana watoto mapacha, Kulwa na Doto, Doto alikuwa nje amepakatwa na mama yake wakati Kulwa alikuwa ndani amelala, ghafla mlio mkubwa ulisikika lakini watu waliudharau na kudhani kuwa itakuwa radi, lakini ngurumo zilivyozidi ilibidi watu waanze kuchukua hadhari ili kujinusuru,” anasema Adia.
Anasema, baada ya kusikia ngurumo zinakithiri na nyingine zikisikika ndani kabisa ya chumba alimolala mtoto Nasri Kasim(Kulwa) mwenye umri wa miezi sita, mama wa mtoto huyo alinyanyuka na kukimbilia chumbani ambapo alikuta kombora likiwa limejikita katikati ya kitanda ambacho Nasri alilala.
“Alichofanya ni kumchukua mtoto na kutoka nje lakini kabla hajamalizikia kutoka, kombora jingine lilijikita ardhini karibu kabisa na mlango wa chumba hicho na kuzama kabisa sakafuni na kubaki kichwa pekee,” anasema Adia.
Anasema, licha ya majeraha kidogo ya kuungua aliyoyapata, jambo ambalo wanamshangaa Mungu, ni kitendo cha kombora lenye ukubwa ule kukita pembeni na kumuacha mtoto Nasri akiwa salama.
Baba mwenye nyumba wa Rose, Adam Kasaba, anasema, hakuna aliye tegemea usalama wa Nasri kwani kishindo kilichosikika ndani ya chumba kile kilikuwa cha kutisha lakini kwa muujiza wa Mungu, kombora lilimkwepa na kutoboa kitanda likimuacha yeye hai.
Bibi Kizee naye anusurika
Mama Samjela mwenye umri wa miaka 78, mkazi wa Pugu Kajiungeni, shuleni, anasema, ilikuwa saa mbili usiku wakisikiliza taarifa ya habari akiwa na mtoto wake ambaye ni Diwani wa kata ya Pugu, Imelda Samjela, ghafla wakasikia ngurumo za radi, wakazipuuzia lakini walipoona hali hiyo inazidi wakaamua kuzima luninga na kuanza kujisalimisha.
“Tulipoona ngurumo zinazidi mimi na wajukuu na wanangu tuliamua kukimbia lakini mimi presha ikanipanda nikapelekwa hospitali ya Kisarawe, pale tukakuta watu wamejaa na hakukuwa na huduma ndipo nilipopelekwa Tumbi,” anasema mama Samjela.
Anasema, kombora lilitoboa paa la chumba anacholala yeye na kubomoa ukuta hivyo kama siyo Mungu yeye naye angekuwa anaitwa marehemu hivi sasa. Anasema anawaza ingekuwaje kama wakati huo angekuwa amelala katika chumba hicho?
“Baada ya kukimbizana hospitali, huku nyuma kombora lilikuja na kutoboa ukuta wa chumba changu, kwa hiyo kama siyo Mungu, hata mimi ningekuwa nimekufa tayari,” anasema.
Muuguzi anusurika, nyumba yake yateketea kwa moto
Muuguzi wa hospitali ya Buyuni iliyopo Gongo la Mboto, Maserlina Maeda, anasema,licha kuunguliwa nyumba yake, lakini anamshukuru Mungu kwa kunusurika na kifo kwani kombora lilienda kutoboa ukuta wa chumba anacholala na kujichimbia kitandani tena palepale anapoweka kichwa wakati wa kulala.
“Usiku huo mimi na mwanangu tukiwa tumetulia hatuna hili wala lile, tulisikia vishindo tukadhani ni majambazi lakini hali hiyo ilipozidi, mwanangu alipata woga akaanza kukimbia, mimi nikarudi ndani kuchukua fedha lakini nikakuta mlango umefungwa na mimi nikaamua kujisalimisha,” anasema Maeda.
Anasema, yeye na mtoto wake walipotezana na baadaye wasamaria wema walimfuata na kumpa taarifa kuwa nyumba yake inateketea kwa moto.
“Niliposikia hivyo nilichanganyikiwa, nilidhani mwanangu atakuwa naye ameungua na kufariki lakini majirani walinitia moyo kuwa mtoto yu mzima isipokuwa nyumba na mali zilizopo ndani yake vimeungua,” anafafanua muuguzi huyo ambaye sasa anaishi maisha ya kusaidiwa kila kitu kuanzia malazi mpaka mavazi.
Maeda anasema, bomu lile liliangukia katika kitanda chake na kulipuka tofauti na mengine ambayo yalikuwa yanatoboa nyumba bila kulipuka, jambo lililosababisha mali zake zote kuteketea kabisa.
Makombora yavuka nyumba za watu na kuchimbua makaburi
Katika hali isiyo ya kawaida, wakazi wa Gongo la Mboto, Mzambarauni, wanasema , baadhi ya makombora yalikuwa yanavuka nyumba zao na kutua katika makaburi hatua chache yalipo makazi yao.
Mkazi wa eneo hilo, Jamila Mwainunu anasema, anashangazwa na hali ile kwani, nyumba yake haijaguswa hata kidogo na kombora wala haikupata ufa, sio kwamba makombora hayo hayakuwa yakifyatuka upande wake bali yalivuka na kutua katika makaburi yaliyo jirani na nyumba yake.
“Mungu kweli ni wa ajabu, kwangu huu ni muujiza kwani, bomu lile pale (ananyoosheaa kidole juu ya kaburi ambapo bomu limejikita) limevuka nyumba yangu na kwenda kuchimbua kaburi,” anasema Jamila.
Anasema, pamoja na kusikitishwa na maafa ambayo yamewakuta ndugu jama na marafiki zake lakini anamshukuru Mungu kwani makombora makubwa yalikuwa yakivuka nyumba yake na kuangukia katika makaburi jirani kabisa na nyumba yake.
Upendo na kusaidiana
Upendo ulionekana wazi, kwani licha ya purukushani zilizokuwepo wakati wa mlipuko wa mabomu, Watanzania walisaidiana kwani baadhi walichukua jukumu la kuwaokoa watoto wadogo walioonekana kupotezana na wazazi wao.
Nazungumza na Baraka Tumsifu, mkazi wa Gongo la Mboto, Mzambarauni, ambaye anasema, katika kukimbiza roho yake hapo juzi alijikuta akiwaonea huruma watoto wadogo sita ambao walikuwa wamepoteza wazazi wao.
“Imenilazimu kuwaokoa kwani roho yangu haikuiruhusu kuwaacha wapate shida katika kipindi kile, wengine ni wadogo wana miaka mitatu na wanalilia maziwa lakini sina budi kuwalea hadi wazazi wao watakapopatikana,” anasema Tumsifu.
Kwa ujumla, wakazi hao walisema, pamoja na maafa hayo waliyoyapata lakini wanamshukuru Mungu kwa kuwanusuru na makombora hayo hatari ambayo yaliwakatakata baadhi ya watu na kuwatenganisha viungo vya miili yao.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment