Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Zanzibar, Rashid Ali Juma (45), amemwagiwa tindikali na mtu asiyejulikana alipokuwa amekaa nje ya msikiti wa Amaan mara baada ya kumaliza kuswali sala ya Isha saa mbili na nusu usiku.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Maghribi, Aziz Juma Mohamed, Mkurugenzi huyo alikuwa amekaa na wenzake wanne, nje ya msikiti huo, ndipo alipotokea mtu mmoja na aliyekuwa amevaa koti maalum na kumwita jina la Mkurugenzi ‘Rashid’ na aliponyanyua uso wake alimwagiwa tindikali hiyo usoni na mtu huyo kukimbia.
“Ni kweli tumepokea taarifa inayohusu shambulio la hatari, la kumwagiwa kwa tindikali Mkurugenzi wa Manispaa ya Zanzibar, Rashid Ali Juma, ambaye kwa mujibu wa maelezo ya watu aliokaa nao, alipiga kelele zilizokuwa zikiashiria kuwa amepata maumivu makali katika sehemu za mwili wake ikiwemo usoni, kifuani, tumboni na ubavuni,” alisema Kamanda Aziz.
Alisema kwamba mtu huyo ambaye hajafahamika, baada ya kuita jina la Rashid, alitoa chupa kutoka ndani ya koti lake, na kumwagia usoni, majimaji yanayosemekana kuwa ni tindikali, na papo hapo alikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya Mnazi Mmoja.
Kamanda huyo alieleza kuwa watu wanne waliokuwa wamekaa pamoja na Mkurugenzi huyo, walijaribu kumkimbiza mtuhumiwa huyo, lakini aliwatishia kuwamwagia tindikali, na hivyo kushindwa kufikia lengo la kumkamata na kumwacha akikatiza katika vichochoro vya eneo la Amaan mjini Zanzibar.
Hata hivyo, alisema ni mapema kusema kama tukio hilo lina uhusiano na mgogoro wa uongozi katika msikiti wa Amaan, ambapo Rashid Ali Juma ni miongoni mwa viongozi wa msikiti huo, au mgogoro kati ya wafanyabishara wa makontena ya Darajani na Baraza hilo la Manispaa.
Alisema Jeshi la Polisi tayari limeshaanza kufanya uchunguzi wa tukio hilo, ikiwemo kuwahoji watu waliokuwa na mazungumzo na Mkurugenzi, ingawa hakueleza walikuwa wakizungumza nini baada ya kumaliza kuswali.
Rashid Ali Juma ambaye anaishi upande wa pili wa barabara inayotenganisha msikiti huo na makazi yake, inadaiwa kuwa amehamishiwa jijini Dar es salaam kwa matibabu zaidi baada ya kusafirishwa kwa ndege ya kampuni ya Zenith Air, jana saa tano asubuhi ingawa haijafahamika hospitali ya rufaa aliyopelekwa.
Hata hivyo, watu waliokuwa wakizungumza naye kabla ya tukio hilo kutokea, jana walikataa kuzungumza na waandishi wa habari, kwa madai walishatoa maelezo yao katika kituo cha Polisi Ng’ambo hasa baada ya waandishi kutaka kujua mazingira ya tukio na mgogoro wa uongozi unaoukabili msikiti huo.
Katibu Msaidizi wa Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, Omar Abdallah Ali, alithibitisha kufikishwa kwa Mkurugenzi huyo majira ya saa 5:00 usiku, ambapo kwa mujibu wa ripoti ya kitabibu, Rashid Ali Juma ameathirika mwili wake kwa asilimia 25 kutokana na tindikali aliyomwagiwa.
Aliyataja maeneo yaliyoathirika katika sehemu za mwili wake kuwa ni usoni, kifuani, mikononi na kwenye mapaja, na aliendelea kupata matibabu chini ya uangalizi wa madaktari mbalimbali wakiwemo wa macho, ngozi, koo na pua na kwamba ilipofika asubuhi jana, maumivu yote yalikuwa yamepotea na mnamo saa 4:30 asubuhi, Mkurugenzi huyo alikuwa akilalamika kuwashwa na jicho, hata hivyo daktari wa macho baada ya kumuangalia alisema kuwa halina shida yoyote.
“Rashid Ali Juma, alianza kukohoa, na sisi tumempatia ruhusa ya uhamisho kwa ajili ya uchunguzi wa ziada kama kuna athari zaidi, mara nyingi tunatoa ruhusa za uchunguzi wa ziada katika hospitali za rufaa ikiwemo Muhimbili, lakini mgonjwa ana uhuru wake kama anataka kutibiwa hospitali binafsi,” alisema Katibu huyo.
Mkasa huo umekuja huku wafanyabiashara wa maduka ya makontena Darajani wakiwa wamefungua kesi Mahakama Kuu Zanzibar kupinga maduka yao kuondolewa ili kupisha ujenzi wa bustani na maegesho ya magari, kazi ambayo ilikuwa ikisimamiwa na Mkurugenzi wa Baraza hilo, Rashid Ali Juma.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment