ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, February 19, 2011

Phiri: Kaseja bado `Tanzania One`

Kocha wa Simba, Mzambia Patrick Phiri, amesema kuwa kipa Juma Kaseja ataendelea kuwa chaguo lake la kwanza katika timu hiyo inayotetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara licha ya hivi karibuni kudaiwa kuwa kiwango chake kimeshuka.
Akizungumza na NIPASHE, Phiri aliyejiunga Simba kwa mara ya kwanza mwaka 2004 na kuondoka kabla ya kurejea tena, alisema kuwa Kaseja bado ni kipa bora zaidi kwake na anaamini kuwa ndiye
anayestahili kuwa namba moja nchini na hali ya kuruhusu magoli inayomtokea katika siku za hivi karibuni ni ya kawaida katika mchezo wa soka.

Phiri alisema kuwa yeye hawezi kumtupia lawama kipa huyo kwa kuruhusu magoli kutinga wavuni na badala yake, anawaomba viongozi, mashabiki na wadau wa timu hiyo kumpa ushirikiano wa kila hali.
"Ni kipa bora kwangu na anavyofungwa sasa ni sehemu ya mchezo, anahitaji ushirikiano kutoka pande zote. Mchezo wa soka hubadilika wakati fulani kwa mchezaji na, ninaamini hali hiyo itaisha," alisema Phiri.
Aliongeza kuwa mbali na ushirikiano, Kaseja pia anahitaji kupata mapumziko marefu ili arejee katika kiwango chake, lakini ratiba ya mechi za ligi na za kimataifa ndizo zinazomfanya akose muda wa kupumzika kiakili na kimwili.
Phiri alisema kuwa Kaseja amekuwa uwanjani kwa muda mrefu zaidi ukilinganisha na wachezaji wengine, lakini uwezo wake si wa chini kama wengine wanavyofikiria hivi sasa.
"Sikatai kwamba anafanya makosa, yeye ni binadamu na hawezi kuwa sawa kwa asilimia 100, mwisho wa yote naheshimu uwezo wake, yeye ndiye kipa bora kwa sasa," aliongeza Phiri.
Aliongeza kuwa Ally Mustapha 'Barthez' pia ni kipa mzuri na ndio maana anampanga katika mechi za ligi msimu huu na hiyo imetokana na uwezo wake kuongezeka akiwa ndani ya kikosi hicho.
Phiri alisema kuwa anaamini timu yake itafanya vizuri katika mechi zinazofuata na sare ya 2-2 waliyoipata dhidi ya Toto African isionekane kuwa ni kigezo cha kulaumu baadhi ya wachezaji.
Alisema kuwa wachezaji wake watakuwa katika mapumziko leo na kesho huku wakitarajia kurejea uwanjani Jumatatu ili kujiandaa na mechi yao itakayocheza Februari 27 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Kaseja ambaye mwaka jana alitwaa tuzo ya kipa bora, juzi aliiambia gazeti hili kuwa anaumia moyoni kufungwa lakini hana budi kukubaliana na matokeo hayo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: