ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, February 19, 2011

Shinda majaribu ya fedha, faidi mapenzi katika ukata! - 2

Luqman Maloto
Tunapokutana katika sehemu ya pili ya makala haya leo, sote tunajiridhisha kwamba hivi sasa nchi yetu imekumbwa na baa kubwa la kiuchumi.

Umeme umesababisha uzalishaji upungue, kwa hiyo kwa namna moja au nyingine inawezekana pato lako au la mwanandani wako linatetereka.

Nchi imekuwa na misingi migumu. Mara Dowans mara yule lakini wananchi wa kawaida wanazidi kuangamia. Wajasiriamali waliowekeza kwenye saluni, hivi sasa wanaumia. Gharama za uendeshaji zimepaa mara mbili kutokana na matumizi ya jenereta.


Wengine wanalazimika kufunga ofisi kwa sababu hawamudu jenereta. Fedha zinakuwa ngumu, kwa hiyo wote tunakubaliana kwamba hali ni mbaya.

Tunapoliangalia hilo na tunaporudi kwenye uhusiano, unapaswa kuzingatia kuwa vyovyote mnavyojikuta mpo kwenye mazingira tata kiuchumi, mnapaswa kushirikiana mpaka pale yatakaponyooka.

Hii inajumlisha kupanga bajeti ya vitu na kujibana kuliko mwanzo, pia kujitahidi kutafuta bidhaa za gharama nafuu, yote hayo ili mfurahie maisha licha ya ukata unaowakabili.

Kushirikiana katika kutafuta vitu venye sura ya kimahaba, kutoka ‘out’ kwenye maeneo ambayo hayagharimu fedha nyingi, ni muhimu mno katika kuweka hai uhusiano wako, pale unapobeba tafsiri ya ‘mambo magumu.’

Ni aibu fedha ikawasababisha mtengane. Ni muhimu mambo ya fedha yakapata kujadiliwa na ninyi wote pamoja.

Ila mtikisiko huo hauruhusiwi kuwafanya muwe wazembe kujenga penzi endelevu. Ikitokea tofauti ni dhambi kubwa!
Hamna fedha, lakini yapo mambo ambayo mkiyafanya mtayafurahia, ingawa hayatagusa mfuko wa yeyote kati yenu.

Mfano, kukaa nyumbani na kuangalia muvi nzuri itawagharimu kiasi gani? Fikiria kwamba wewe na yeye mmeketi vizuri sebuleni, mnazungumza mambo yenye kuleta mwanga wa kimaisha, huku matukio ya filamu yakiteka hisia zenu.

Maisha yametofautiana, inawezekana ‘cha kuonea’ hakipo nyumbani, lakini hiyo siyo ishu! Kila mtu anahitaji kupewa elimu ya mapenzi, iwe mjini au kijijini.

Kwa maana hiyo, anaweza kuketi faragha na mwenzi wake na kusimuliana hadithi za kimapenzi.

Yapo mazingira mazuri yenye hewa safi, fukwe mbalimbali, bustani na kadhalika. Yote hayo ni maeneo ambayo unapaswa kuyatumia na mwenzi wako kuhakikisha furaha haipotei.

Lingine ambalo linaweza kufanyika bila kuwagharimu kutoboka mifuko ni kupika chakula kizuri cha usiku ambacho kitakupendeza wewe na mwenzi wako.

Furaha kidogo huyeyusha maudhi na msongo wa mawazo! Kula ‘msosi’ mtamu, kuchombezana kwa hadithi za hapa na pale ni kitu maalum sana.

Inawezekana pia kutoka ‘out’ na kwenda kujumuika pamoja kiwanja tulivu, kupata ‘dinner, huku mkiburudishwa na muziki laini.

Kuna mambo mengi ya kufanya, ila pointi ya msingi ni kuwa makini na uhusiano wako na kuhakikisha huyumbishwi na matatizo ya kifedha. Hustahili kuchachawa. Kuna wakati wa kupigana kwa ajili ya fedha lakini pia kipo kipindi cha kudumisha penzi.

Hisia zako kwenye fedha na mapenzi ni muhimu lakini si busara kuchanganya moja na lingine. Katika kukamilisha furaha yako ya kimapenzi wakati mambo ya kifedha yanapokwenda segemnege, hapa chini kuna pointi za kuzingatia.

Mlikuwa na hisia gani wakati mlipojikuta mnaangukia kwenye sayari ya kimapenzi kwa mara ya kwanza?
Ukipata jibu, basi nakukumbusha kuheshimu mlipotoka.

 Mlipendana na kila mmoja akili yake ilielekea kwenye mapenzi, hivyo ndivyo mnavyotakiwa kuwa siku zote. Iwe kwenye shida au raha!

 *Kumbuka jinsi mlivyokuwa mnasaidiana kipindi kile mambo yalipokuwa murua. Ni muda sasa wa kushirikiana wakati wa harakati za kutafuta ‘ankara’.

*Zingatia kuwa inahitaji wawili wanaopendana ili kuyafanya maisha yawe safi, pia kupitia kwao, sukari inaweza kugeuka shubiri.
Mkiishi kama timu moja ni ufunguo wa kufanikiwa kwenye njia zote.

* Siku zote fungueni masikio na msikilizane hata kama hamkubaliani. Kupuuza kitu alichosema mwenzako, kulaumiana au kufunga mjadala wakati mwenzako anachangia ni kosa.

Aidha, kutaka matatizo yako uyajadili wewe mwenyewe, ilhali naye angependa apewe fursa ya kutoa mchango wake, haiwezi kuwa suluhu ya matatizo, badala yake, inawezekana hali ikawa mbaya zaidi.

* Zingatia yote hayo, pia muwe na utaratibu kwamba mnapokutana kila mmoja anaweka mezani mpango wake wa kukabiliana na mtikisiko wa kiuchumi na kuheshimiana.
Huko nyuma nimewahi kuandika kwamba wapo watu wanaosema kuwa penzi bila fedha ni uhusiano wenye ulemavu!

Upande mmoja naamini kwa sababu nimeona na ninaendelea kushuhudia lakini maandishi haya yakizingatiwa, thamani ya penzi itabaki kusimama katika kipimo chake.

No comments: