ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 9, 2011

International Friendly Match,Taifa Stars 1-0 Palestine

Palestine National Team
Taifa Stars
NDOTO za kocha Jan Poulsen kupata ushindi wa kwanza katika mechi ya kimataifa imetimia baada ya jana timu yake, Taifa Stars kuilaza Palestina kwa bao 1-0  la Mrisho Ngassa, dakika ya 62 kutokana na kazi nzuri ya Mohammed Banka aliyetokea akitokea benchi kipindi cha pili.

Ngassa alifunga bao hilo kwa kumchambua kipa Abdallah Alsidawi kutokana na mpira wa  Banka, ambaye alikuwa ameingia uwanjani dakika tatu kabla ya bao hilo.



Awali, mchezo huo ulianza taratibu mbele ya watazamaji wengi kiasi waliojitokeza kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.  Kwa dakika 20,   Stars walimiliki mpira na kuwadhibiti wageni ambao nao walianza taratibu kuuzoea mchezo huo.

Iliwachukua dakika tatu wageni, Palestina kulifikia lango la Stars wakati Hisham Alsidawi  alipowafunga tela mabeki na kupiga krosi nzuri ambayo hata hivyo iliokolewa na Nadir Haroub 'Cannavaro'.

Dakika mbili baadaye, Mussa Hassan Mgosi alipiga kombora kali la umbali wa mita 25 ambalo kipa wa Palestina, Saed Abusalim aliliokoa kwa ustadi mkubwa.

Katika dakika ya 16, Shatrit Mohammed aliunasa mpira uliopigwa na Cannavaro, lakini akiwa na kipa Shaaban Kado alifyatua mkwaju ambao kipa huyo namba mbili wa Stars alilidaka.

Kama ilivyokuwa awali, Mgosi tena alichomoka vizuri kutoka ukuta wa Palestina upande wa kushoto, lakini krosi yake kwenda kwa John Boko aliyekuwa katika nafasi nzuri ya kufunga, ilipotea.

Boko alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 27 na mwamuzi Oden Mbaga  kwa kosa la kuunawa kwa makusudi mpira.

Kipindi cha pili, kocha  Poulsen aliwapumzisha Shadrack Nsajigwa na nafasi yake kuchukuliwa na Haruna Shamte. Pia, alimtoa Ramadhan Chombo 'Redondo' , dakika ya 59 na nafasi yake kuchukuliwa na mkongwe Mohammed Banka na Julius Mrope badala ya Ngassa.

Winga Shatrit Mohammed, ambaye kipindi cha kwanza alikosa bao, alimpa wakati mgumu kipa Kado katika dakika ya 55 ya mchezo huo baada ya kuachia mkwaju mkali ambao mlinda mlango huyo alijitosa kuuokoa.

Kocha huyo pia alimtoa Boko katika dakika ya 75 na kumwingiza Mbwana Samatta na kufuatiwa na Mgosi ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Gofrey Bonny.

Mwenzake wa Palestina, Bezaz Moussa alimpumzisha Hisham Salhi na kumwingiza Shad Alwisat na Khader Abuhamad na kuingia Fael Attal.

Stars walikaribia kupata bao la pili dakika ya 88, lakini Bonny alikosa umakini na kushindwa kutumia pasi ya Mrope ambaye alikuwa amewapiga chenga mabeki lukuki wa Palestina.

No comments: