ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 7, 2011

Majambazi yaua mwanajeshi katika utekaji wa magari-Mwananchi

ASKARI wa Jeshi la Kujenga Taifa(JKT), ameuawa na wengine watano kujeruhiwa baada ya kundi la majambazi likiwa na silaha za jadi kuteka magari manne katika barabara ya Chalinze – Segera mkoani Pwani.

Tukio hilo lililodumu kwa takribani dakika 20 lilitokea juzi majira ya saa 5:00 usiku eneo la Ng'wandu katikati ya kijiji cha Manga na Mbwewe.
 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Absalom Mwakyoma alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba watu saba wanashikiliwa na polisi wakituhumiwa kuhusika na tukio hilo.

Kamanda Mwakyoma alisema kuwa aliyeuawa ni Boniface Bukuru (25) wa kikosi cha JKT 835 KJ COY Tanga, mwenyeji wa Mkoa wa Kigoma huku waliojeruhiwa ambao wamelazwa katika hospitali ya Tumbi ni Joseph Edward (52), Mbwana Mwabindu (31), Athuman Mbaga (34), Harubu Zungu(28) na Mwinyihad Amri(24).

"Tayari watu saba wanashikiliwa kwa tuhuma za kuhusika na tukio hili. Eneo la tukio linaendelea kukaguliwa na uongozi wa polisi kwa kushirikiana kikosi cha utayari cha polisi,'' alisema Mwakyoma
Alisema katika tukio hilo magari matatu aina ya Fuso pamoja na lingine (Toyota Noah) yalitekwa.

Edward Shellukindo(50) ambaye ni mmoja wa waliotekwa katika tukio hilo lakini alinusurika, aliliambia Mwananchi kuwa majambazi hao walikuwa zaidi ya 10 na kwamba waliweka magogo manne katikati ya barabara.

"Tulikuwa katika gari dogo(Toyota Noah) tukitokea  boda ya Taveta Horiri kwenda Dar es Salaam . Tulipofika kati ya Kijiji cha Ngw’andu na Mnarani, dereva alioona magogo barabarani ikabidi asimamishe gari,'' alisema Shellukindo. 

Alisema ,” Ghafla likajitokeza kundi la watu zaidi ya 10 wakiwa na vipade vya nondo, marungu,na kuanza kutushambulia, wakamtaka dereva azime taa zote na kisha wakatuamuru kutoka ndani ya gari na kuanza kutupiga.''

Alisema kuwa alinusurika kipigo pamoja na kuuawa baada ya kutoa Sh 600,000 na kwamba wakati akitoa fedha hizo gari jingine(Fuso) lilikuwa limefika katika eneo hilo na majambazi hao wakalifuata na kuanza kumpiga dereva na msaidizi wake.

"Wakati wengine wakitupiga wengine walikuwa wakikagua  mifukoni na ndani ya gari, walichukua simu fedha taslimu pamoja na vitu vingine,'' alisema.

Akizungumzia kifo cha askari, Shellukindo alisema walikuwa wawili na waliombewa msaada  katika eneo la Kabuku kituo cha polisi na kwamba kutokana na kuwa walikuwa wamevaa sare za kazi, majambazi waliwapiga sana kwa marungu na nondo kichwani.

"Bukuru alipigwa sana kichwani, hali iliyomlazimu  kuanza kukimbia ndipo walipomfuata tena na kumpiga na kisha wakamtupa msituni wakati huo sisi tukiwa tumeamrishwa kulala chini. 

'' Dakika kama ishirini baadaye majambazi  yalitokomea msituni, polisi walifika, ndipo tukawaelekeza alipo Bukuru ambaye alikuwa akivuja damu puani, masikioni na mdomoni,'' alisema.

No comments: