Mtoto Deus Juma (7) akiwa wadi namba moja katika Hospitali ya Wilaya ya Geita akiuguza majeraha kwenye mikono yake baada ya kuchomwa moto na mama yake mzazi. (Picha na David Azaria). |
POLISI wilayani Geita katika mkoa wa Mwanza wamemkamata mwanamke kwa tuhuma za kumuunguza mwanawe kwa maji ya moto mikono yote miwili na kisha kumfungia ndani kwa siku tatu.
Mary Dominick anadaiwa kufanya kitendo hicho wiki iliyopita nyumbani kwake katika Mtaa wa Msalala, mjini Geita baada ya kumtuhumu mtoto huyo kuiba Sh 6,000 zilizokuwa ndani ya nyumba.
Mtoto huyo, Deus Juma (7) anayesoma darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Kivukoni amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Geita.
Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Abdallah Dihenga alisema walimpokea mtoto huyo juzi akiwa na majeraha mikononi.
Akiwa katika wodi namba moja hospitalini hapo chini ya uangalizi wa majirani waliodai ni wanakikundi cha kusaidiana ambacho mama yake ni mwanachama, mtoto huyo alisema siku ya tukio baada ya mama yake kurejea nyumbani akitokea kwenye shughuli zake, alimuita na kuanza kumpiga huku akimtuhumu kuiba fedha licha ya yeye kujitetea.
Juma ambaye alikuwa akijieleza huku akilia, alisema, “pamoja na kujitetea kwa muda mrefu lakini mama hakunielewa hata kidogo na kuendelea kuning’ang’aniza kwamba mimi ndiye mwizi niliyemuibia fedha zake,” alisema na kuongeza:
“Aliniingiza ndani na kisha kunifunga mikono yote miwili pamoja na miguu kwa mpira wa kufungia mizigo kwenye baiskeli na kuanza kunipiga” .
Alidai baada ya kipigo hicho, mama yake hakumfungulia mpira aliokuwa amemfunga miguuni na mikononi hali iliyomlazimu kulala sakafuni kwa siku tatu kabla ya kufunguliwa na kukutwa mikono imevimba.
Kwa mujibu wa mtoto huyo, mama yake alipokuta mikono imevimba alichemsha maji ya moto na kumkanda na alipoona uvimbe haupungui, aliamua kuchukua barafu na kumuwekea kwenye mikono.
Inaelezwa kwamba jana asubuhi ndipo mtoto huyo alifunguliwa na baada ya kutoka nje, alikimbilia barabarani alipokutana na wasamaria wakampeleka kwa Mwenyekiti wa Kitongoji, Sosthenes Mahushi.
Kiongozi huyo wa kitongoji alithibitisha kumpokea mtoto huyo na kisha kumpeleka polisi kabla ya kumfikisha hospitalini hapo.
Mtoto huyo alishuhudiwa akiwa na majeraha usoni na kichwani anayodai yalitokana na kupigwa na kipande cha ubao.
Vile vile mikono imevimba huku akiwa na vidonda vikubwa katika viganja kiasi cha kushindwa kukunja vidole.
Polisi wilayani hapa imethibitisha tukio hilo na kusema mwanamke huyo anashikiliwa na kwamba atafikishwa mahakamani wakati wowote uchunguzi utakapokamilika.
Wakati huohuo, wanawake waliokutwa hospitalini hapo wakimhudumia mtoto huyo hawakuwa tayari kuzungumza na kuandikwa majina yao gazetini.
Pia hapakuwa na ndugu wala jamaa waliopatikana mara moja kuzungumzia undani wa maisha ya mtoto huyo.
Mama yake pia hakupatikana kuthibitisha tuhuma kutokana na kushikiliwa na polisi.
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment