
Mbunge huyo amesema, hawezi kufuta kauli hiyo na yupo tayari kupigwa risasi kutetea msimamo wake.
Lema amesema, alikuwa tayari kuutoa ushahidi huo leo bungeni mjini Dodoma hivyo uamuzi wa Spika wa Bunge, Anne Makinda kuagiza aupeleke ofisini umemsononesha.
Kwa mujibu wa Lema, anauamini ushahidi wake kwa zaidi ya asilimia 100, hivyo akiambiwa achague kufuta kauli yake au kupigwa risasi atachagua kupigwa risasi.
Mbunge huyo amekataa kuwaeleza waandishi wa habari endapo ushahidi alionao ni wa maandishi, wa picha au wa aina nyingine.
“Mimi nilikuwa tayari na ushahidi wangu na nilikuwa vizuri sana, na nipo vizuri sana” amesema Lema leo wakati anazungumza na waandishi wa habari katika ofisi za habari za Bunge mjini Dodoma.
Kwa mujibu wa Mbunge huyo kijana, kanuni za Bunge zilimtaka awasilishe ushahidi hue leo bungeni kutekeleza agizo Makinda lakini Spika katoa uamuzi mwingine.
Amesema,kaambiwa apeleke ushahidi wake katika ofisi ya Spika wa Bunge hivyo ameshangaa kwa nini asiuwasilishe ushahidi huo bungeni kama kanuni zinavyotaka.
“Sijui kwa nini ameamua alivyoamua” amesema mwanasiasa huyo aliyekuwa miongoni wa wafuasi wa Chadema waliokuwepo wakati wa vurugu hizo mjini Arusha.
Wakati wa maswali ya papo hapo kwa Waziri Mkuu Alhamisi iliyopita, Pinda alisema hakukuwa na sababu za kutokea kwa vurugu hizo na akawalaumu viongozi wa Chadema kuwa walikuwa chanzo cha tatizo hilo lililosababisha mauaji ya watu watatu.
Pinda alisema bungeni kuwa, viongozi hao wa Chadema walikaidi amri ya kuzuia maandamano na waliwahamasisha wananchi wakavamie kituo kikuu cha polisi cha Arusha ili kuwatoa viongozi wa chama hicho waliokuwa wamekamatwa.
Baada ya Pinda kusema hayo, Lema alisimama, akaomba mwongozo wa Spika kwa kutumia Kanuni Namba 64 ya Bunge akitaka kufahamu iwapo Waziri Mkuu amesema uongo bungeni, Mbunge anapaswa kuchukua hatua gani.
Spika wa Bunge alimtaka Lema athibitishe kuwa Waziri Mkuu kasema uongo, na kwa kuzingatia muda aliokuwa amepewa, ilibidi leo awasilishe ushahidi huo.
1 comment:
Mh Lema tupo nawe maana serikali ya CCM lazima wajue liberty is meaning less where the right to utter one's thoughts and opinions has ceased to exist.Ndio maana wamebaidilisha na wanaitaka hiyo report ofisini ili waichakachue.
Post a Comment