ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 21, 2011

MMILIKI DOWANS AFIKA KUTETA NA TANESCO

*AKATAA KUONANA NA WAZIRI, AGOMA KUPIGWA PICHA  
WAKATI Mjadala wa Dowans ukibaki kwenye swali la nani mmiliki wake, raia wa Oman, Sulaiman Mohammed Yahya Al Adawi amejitokeza na kukiri kuimiliki kampuni hiyo inayoidai Tanzania mabilioni ya shilingi.

Al Adawi alikutana na wahariri wa vyombo vya habari nchini jana na kueleza ujio wake kuwa umelenga kukutana na Tanesco na kujadili suala la malipo ya Sh94 bilioni ambayo kampuni yake inaidai Tanzania. 
 

Ujio wa Al Adawi umemaliza mjadala uliogubika umiliki wa Dowans na kuwachanganya Watanzania huku baadhi yao wakiamini kuwa kampuni hiyo inamilikiwa na mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz. 

Al Adawi ni mmoja wa watu ambao majina yao yako kwa Wakala wa Usajili wa Kampuni nchini (Brela) waliojiandikisha kama wamiliki wa kampuni hiyo ya Dowans.  

Watu wengine waliotajwa na Brela kuwa ni wamiliki wa Dowans Tanzania Ltd, ambao ni Dowans Holding S.A, Costa Rica na Portek Systems and Equipment (PTE) Ltd na uraia wao kwenye mabano ni Andrew James Tice na Guy Picard (Canada), Gopalakrishnan Balachandaran (India), Stanley Munai (Kenya) na Hon Sung Woo (Singapore).
 
Akizungumza katika mkutano huo huku akigoma kupigwa picha, Al Adawi alisema yuko tayari kuzungumza na Tanesco kuhusu fidia ya Sh94 bilioni (hakutaja kiasi), baada ya kuvunjwa kwa mkataba baina ya kampuni yake hiyo na Tanesco. 

"Nimekuja kwa mambo mawili; moja ni kuondoa sintofahamu iliyopo hivi sasa kuhusu kampuni ya  Dowans na kuangalia kama kuna uwezekano wa kuwapo suluhisho la kile kilichopo hivi sasa kuhusu Dowans," alisema Al Adawi.

Kwa mujibu wa mfanyabiashara huyo, ambaye ni Mwanajeshi aliyestaafu katika ngazi ya Brigedia Jenerali, Tanzania ni nchi inayovutia kibiashara na inayofuata sheria za uwekezaji.  

Lakini Al Adawi ambaye katika mkutano huo aliambatana na mwanasheria wa kimataifa, John Miles na Mkurugenzi wa fedha, Stanley Munai wa Dowans Tanzania Ltd, alisema, licha ya Tanzania kuwa kivutio cha uwekezaji,  kampuni yake katika uwekezaji nchini imekumbwa na jinamizi.  

“Nimekuwa na imani na Tanzania na nimeitikia wito wa uwekezaji katika kipindi cha matatizo yenu, lakini yote yaliyojitokeza tangu niwekeze nchini ni unyanyasaji na mnaendelea kuninyanyasa hadi leo na hii katika hali ya kawaida hamnitendei haki," alisema Al Adawi.  

Mfanyabiashara huyo alieleza kuwa hakuwa ametaka kuishtaki Tanesco na kudai fidia ya mabilioni hayo ya shilingi, lakini alilazimika kufanya hivyo kutokana na namna alivyotendewa katika kipindi cha uwekezaji wake. 

Alifafanua kuwa Tanesco ilimhakikishia usalama wa uwekezaji wake na hivyo akakubali kuingia nao mkataba lakini, shirika hilo likavunja mkataba huo na kukiuka makubaliano yaliyofikiwa chini ya sheria zake yenyewe za manunuzi.  

Alisema jambo hilo halieleweki katika ulimwengu wa sasa wa biashara kimataifa akieleza kuwa linaweza kuisababisha nchi hasara kubwa.  Mfanyabiashara huyo aliyetumia sehemu kubwa ya taarifa yake kueleza historia ya namna alivyoingia mkataba, alisema katika ujio wake huo hana mpango wa kukutana na waziri wala kiongozi mwingine yeyote wa serikali bali Tanesco.  

Alikiri kuwa na uhusiano na mbunge wa Igunga (CCM), Rostam Aziz na kusema kuwa ni rafiki yake wa siku nyingi na ndiye aliyemtaka aje kuwekeza katika sekta ya umeme nchini mwaka 2005.  "Rostam ndiye aliyenipa nguvu ya kisheria za kusimamia masuala ya kampuni yangu hapa Tanzania," alisema. 

"Nimekuwa nikifuatilia maendeleo ya sekta ya mawasiliano ya Simu Afrika Mashariki kwa hamu kubwa. Nilikusudia Dowans iwe mwekezaji katika sekta hiyo Tanzania kwa kuwekeza mkongo wa mawasiliano ya ubora wa juu nchi nzima, tumenyimwa fursa na imeenda kwa Wachina, nimehamisha uwekezaji,"alisema.  

Alisema kuwa alitarajia kampuni yake iwekeze katika sekta ya mawasiliano ya simu, lakini ana taarifa kuwa serikali ya China imeikopesha serikali ya Tanzania kuwezesha kusimikwa mkongo huo wa taifa na kuwanyima wao fursa nchini.  

Adawi ambaye alidai kuwa yeye ni mfanyabiashara mdogo ambaye haoni sababu ya picha zake kutumia katika magazeti au vituo vya runinga, alisema ametumia mamilioni ya shilingi kukamilisha mradi huo, wenye mitambo mipya.

Dowans imekuwa ikiumiza vichwa vya wasomi, wanaharakati na wanasiasa hasa baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara (ICC), kuitaka Tanzania iilipe kampuni hiyo Sh94 bilioni kutokana na Tanesco kuvunja mkataba wake, kinyume na taratibu.

Lakini wakati CCM na serikali yake ikibariki malipo hayo,  Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kwa kushirikiana na wanaharakati wa haki za kijinsia nchini, waliwasilisha Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara, pingamizi ya malipo hayo huku CUF, ikifanya maandamano kushinikiza isilipwe.

Mvutano huo ulishika kasi tangu Desemba 27 mwaka jana, siku ambayo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Fredrick Werema aliposema kuwa ameisoma hukumu hiyo na kuridhika nayo hivyo, Serikali haitakata rufaa.   Siku chache baadaye, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja alitoa kile alichokiita tamko rasmi la Serikali kuhusu malipo hayo akisema kuwa Serikali imekubaliana na ushauri wa Mwanasheria Mkuu. 

Alisema ingawa kiwango kinachotakiwa kulipwa na Serikali kwa kampuni hiyo ni kikubwa, lakini alisema hakuna jinsi na badala yake Serikali imemua kulipa ili kuepuka kujiingiza katika matatizo makubwa ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa riba ya malipo hayo.  

Akitoa ufafanuzi wa mchakato wa usajili wa tuzo hiyo, Msajili Bongole alisema tayari tuzo hiyo imeshatumwa mahakamani hapo kutoka ICC na kwamba imetumwa na Katibu wa Sekretarieti ya ICC, Victory Oraowski, lakini akasema kuwa, bado haijapokewa rasmi kisheria. 

Alisema licha ya tuzo hiyo kuwasilishwa mahakamani hapo, mchakato wa usajili wake haujaanza kwa kuwa utaratibu wa kisheria bado haujakamilika kulinganga na taratibu za usuluhishi na tuzo zinazotolewa pasipo amri ya mahakama.  

“Sheria zinazotumika katika usajili wa tuzo hiyo ni sheria ya usuluhishi (Arbtration Act) Sura ya 15 ya Sheria za Tanzania pamoja na sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai (Civil Procedure Code- CPC), sura ya 33 jedwali la 2 kifungu cha 20.  

Alisema baada ya tuzo hiyo kuwasilishwa mahakamani, mshinda tuzo anapaswa kuwasilisha maombi ya maandishi akiambatanisha na hati ya kiapo ili tuzo yake iweze kusajiliwa.  Alisema baada ya mshindi wa tuzo kuwasilisha maombi hayo, Mahakama itatoa taarifa kwa mshindwa tuzo atoe sababu kwa muda maalumu atakaopewa na Mahakama aeleze kwa nini tuzo hiyo isisajiliwe.  

“Kama mshindwa tuzo akisema hana pingamizi tunaisajili na akisema ana pingamizi basi tunasikiliza kwanza pingamizi hilo na kulitolea uamuzi. Baada ya taratibu hizo ndIo tunaweza kuisajili sasa na kuwa nguvu ya kumlazimisha mdaiwa kulipa deni,” alisema Bongole. 

Alisema mbali na mshindwa, mtu mwingine yeyote ambaye pia ataona maslahi katika tuzo hiyo ana haki ya kuwasilisha pingamizi lake ambalo pia litasikilizwa na kutolewa uamuzi kabla ya tuzo kusajiliwa.  

“Kwa hiyo kwa sasa tumeletewa tu, hiyo tuzo ili tuihifadhi tukisubiri mwenye tuzo hadi atakapoleta maombi na wala si kwamba sisi ndio tunakwenda kumtafuta, mahakama haiwezi kwenda kutafuta kesi,” alisema Bongole. 

Hata hivyo akizungumza kwenye semina ya wabunge jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema serikali iko katika mchakato wa kuangalia namna itakavyoweza kutumia njia za kisheria kuondoa mzigo wa kuilipa mabilioni ya shilingi kampuni ya kufua umeme ya wa dharura ya Dowans.  

“Suala hili ni la kisheria kwa maana kwamba limetokana na kitu kinaitwa mkataba, jambo hilo limepelekwa mpaka kwenye chombo hicho cha kisheria chombo kile kimetoa maamuzi yake maamuzi yake yamerudiswa hapa nyumbani kwa ajili ya utekelezaji. 

Aliendelea,"kwa hiyo katika mazingira ya kawaida hatuna namna nyingine ya kusema hapana kimabavu bavu hivi, hebu tutazame kama vipo vyombo au watu wanaosema upo uwezekano wa kujiondoa katika hili basi tujaribu kushirikiana nao ili tuone kama wanaweza kutusaidia namna ya kutoka pale bila kuvunja sheria zinazotakiwa kuzingatiwa.”


CHANZO: MWANANCHI

No comments: