ZAIDI ya abiria 150 waliokuwa wakisafiri kwa boti kutoka Kijiji cha Ikola, Wilaya ya Mpanda mkoani Rukwa kuja mkoani Kigoma, wamenusurika kufa maji baada ya boti yao kukumbwa na dhoruba.
Akisimulia mkasa huo muda mfupi baada ya kufika katika bandari ndogo ya Ujiji mjini Kigoma, abiria katika boti hiyo, Juma Mswahili alisema dhoruba hiyo iliwakumba baada ya boti hiyo inayojulikana kama ‘Pamba nyepesi’ kuzimika injini yake na kuanza kusukwa sukwa na mawimbi.
Mswahili alisema licha ya kuzimika injini, pia hali ilikuwa mbaya kutokana na boti kuzidisha abiria kuliko uwezo kwani wakati kwa hali ya kawaida ilipaswa kubeba abiria 50, lakini wakati ikipata matatizo hayo, ilikuwa imebeba abiria zaidi ya 150 na mizigo mbalimbali yenye uzito mkubwa.
Abiria huyo alisema hali ilikuwa mbaya kuanzia maeneo ya Lubengela hadi Kijiji cha Herembe ambapo ili kujiokoa, walilazimika kutupa mizigo ziwani Tanganyika ili kupunguza uzito hadi walipookolewa.
“Tulianza kupigwa mawimbi katika maeneo ya Lubengela hali ilikuwa mbaya, tulikata tamaa, tulijua tunakufa, ikabidi tuanze kutupa mizigo na bidhaa mbalimbali zilizokuwa zimebebwa ikiwemo mchele, maharage, samaki na dagaa,” alisema na kubainisha kuwa yeye amelazimika kutosa ziwani gunia nne za dagaa.
Abiria mwingine aliyesafiri katika boti hiyo, Maria Stanslaus alisema bila ya kutupa mizigo ziwani, boti ilikuwa inazama na pengine habari ingekuwa tofauti na wengi wangepoteza maisha.
“Tulianza kupiga simu, mie nilimpigia mume wangu yuko mjini ili awaambie Polisi waje kutuokoa, baada ya kuona kimya akapigiwa Mheshimiwa Serukamba (Peter, Mbunge wa Kigoma Mjini), naye akamwambia Mkuu wa Polisi wa Mkoa eti ndio tukaona kanakuja kaboti
kadogo kutuokoa ambako kasingeweza,’’ alilalamika Maria.
Kutokana na tatizo hilo, Polisi walipata wakati mgumu baada ya wananchi waliofurika katika bandari ndogo ya Kibirizi na Ujiji, kuanza kuhoji kuchelewa kwa jeshi hilo kuokoa watu hadi chama cha maboti kilipopeleka injini nyingine na kuwezesha abiria hao kuendelea na safari hadi mjini Kigoma.
Naye nahodha wa boti hiyo, Deo Boniface alidai wanalazimika kubeba abiria wengi na mizigo kutokana na mahitaji makubwa ya usafiri kwa wananchi wanaoishi katika vijiji vya mwambao wa Ziwa Tanganyika wanaotegemea boti hizo kwa usafiri baada ya meli za mv Mwongozo na Liemba kupunguza safari zake.
“Vijiji vya ziwani huko hakuna usafiri, kwa hiyo wakiona boti tu, watu wanajazana na ni ngumu sana kuwaacha, watu wanakaa wiki wanasubiri usafiri ambao haupo, ni kweli boti yangu ina leseni ya kubeba abiria 50, lakini nawaachaje watu?” alisema nahodha wa boti hiyo.
Alisema wingi wa abiria na mizigo katika ukanda huo, unatokana na kupunguzwa kwa safari za meli za Mv Liemba na Mv Mwongozo, ambazo sasa zinafanya safari mara moja kwa mwezi katika ziwa Tanganyika, Kigoma hadi Mpulungu nchini Zambia badala ya safari nne kwa mwezi za awali.
Naye Ofisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), Iroga Nashon alisema pamoja na uchunguzi wa awali kuonesha boti hiyo ilizidisha uzito, imegundulika kuwa haikuwa na vifaa vya uokoaji kwani ilikuwa na maboya 30 tu ya kujiokoa.
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment