ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 21, 2011

Mabomu yaunganisha familia Gongo la Mboto

Image
Jacob Nyajiego (mwenye suti nyeusi) akipita kutoa heshima za mwisho mbele ya majeneza yaliyohifadhi miili ya marehemu mke wake, Rozi Nyajiego (34) na watoto wake wawili, Clementina Nyajiego (4) na Stella Nyajiego (miezi 3) waliokufa kwa kuangukiwa na ukuta wa nyumba wakati wa milipuko ya mabomu. Ibada ya kuwaaga ilifanyika nyumbani kwake Mzambarauni, Gongo la Mboto Dar es Salaam. Miili ya marehemu hao ilisafirishwa kwenda Rorya, mkoani Mara kwa maziko. (Picha na Fadhili Akida).

INGAWA milipuko ya makombora iliyotokea katika Kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kikosi 511 iliyopo Gongo la Mboto, jijini Dar Salaam ilileta simanzi na hasara kubwa, lakini pia imeunganisha ndugu, jamaa na majirani na kuimarisha upendo katika familia.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wakazi wa eneo hilo, walisema mshituko uliotokana na makombora hayo ulisababisha majirani kufahamiana na wengine kusaidiana ili kuokoa maisha.

“Nimekaa eneo hili kwa zaidi ya miaka miwili, lakini sikuwahi kuzungumza na jirani yangu, lakini ile siku ya mabomu tulijikuta tunaitana na kushauriana jinsi ya kuokoa familia zetu,” alisema mkazi wa Gongo la Mboto, Zainab Hamis akizungumzia tukio hilo la Februari 15, usiku.

Naye Grace Masaule alisema alikuwa hajakaa na mume wake kujadiliana masuala ya kifamilia kwa muda mrefu, lakini siku hiyo mume wake alimueleza juu ya akaunti za benki na maeneo aliyowekeza kibiashara.

Kwa mujibu wa Masaule, siku hiyo yeye na mumewe waliwekeana ahadi ya kutunza vyema watoto endapo mmoja wao atapoteza maisha kutokana na milipuko hiyo.

“Wakati wa mabomu, mume wangu alikuwa anakunywa pombe baa ya jirani, lakini alirejea nyumbani, tukajadili kwa haraka, akanipa fedha na tukagawana watoto na kukimbilia kila mtu na njia yake ili tusife kwa pamoja…kwa kweli alinionesha upendo wa kipekee,” alieleza Grace.

Pia watoto mbalimbali waliohojiwa na gazeti hili, walisema mabomu yamewawezesha kupata fursa za kukaa na ndugu zao wakubwa pamoja na wazazi wao.

“Mimi sikuwahi kukaa pamoja na dada zangu wakubwa, pia sikuwahi kuwaona baba na mama wakiwa pamoja, lakini kuanzia siku ile ya mabomu upendo umeongezeka...yaani hapa ndio nimeamini wazazi wangu wanapendana pia wanatupenda,” alisema Amani Mshauri mwenye umri wa miaka 11.

Naye Mfaume Fadhili (59) mkazi wa Gombo la Mboto alisema pamoja na simanzi kubwa, amefarijika kubaini kuwa watoto wake wanampenda na kumthamini kwa kuwa kila mmoja alimpigia simu kumjulia hali licha ya kwamba alishindwa kuwasaidia walipokuwa wadogo.

Katika hatua nyingine, maiti za watu watatu wa familia moja waliokufa kutokana na kuangukiwa ukuta uliosababishwa na milipuko ya mabomu hayo, wameagwa Februari 20. Maiti hizo ni za familia ya Jacob Nyagiego aliyepoteza mkewe, Rose Nyagiego (34) na watoto wawili Clementina (3) na Stella mwenye umri wa miezi minne na mpwawe Neema ambao kwa pamoja wanasafirishwa kwenda Kijiji cha Manila, Kata ya Rorya kwa ajili ya maziko.

Taratibu za kuaga zilifanyika jana saa 6:30 mchana nyumbani kwa Jacob, Gongo la Mboto Mzambarauni ambako eneo hilo kulipangwa majeneza matatu ya wanandugu hao na kuhudhuriwa na watu mbalimbali.

Akitoa mahubiri yake kabla ya kuaga, Kiongozi wa Parokia ya Ukonga ya Kanisa Katoliki, Paroko Stephano Nyelawila alisema katika janga hilo lililowakumba wakazi wa Gongo la Mboto na maeneo jirani, si kila jambo la kumsingizia Mungu, bali viongozi wameshindwa kuwajibika ipasavyo.

Hata hivyo, alisema kutokea kwa vifo kusiwe ndio chanzo cha kuvuruga amani iliyopo nchini na kuwasihi waumini kuishi kwa kumtegemea Mungu kila mara.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema sio kwamba walioathirika ni wakazi wa Gongo la Mboto peke yake, lakini pia yapo maeneo mengine kama Kimara ambako kuna mabomu manane hadi sasa.

Kamanda Kenyela alisema mabomu hayo yako ardhini hayajatolewa ambapo wananchi walioko karibu wamekimbia makazi yao na kuiomba Serikali wataalamu wa kukusanya mabomu pia watembelee maeneo hayo kwa kuwa wanahitaji msaada.

Aliyataja maeneo ambayo mabomu bado yapo kuwa ni pamoja na eneo la Msuguri, Kibamba Hospitali, Kimara Temboni na Kimara Suka na kuongeza kuwa hayakuathiri binadamu.

Alisema waathirika waliokimbilia Manispaa ya Kinondoni kwa ajili ya kupatiwa hifadhi ni 1,500.

Wakati huo huo, majeruhi waliokuwa wamelazwa katika hospitali za Amana, Temeke na Muhimbili kutokana na kujeruhiwa katika mlipuko wa mabomu katika kambi hiyo ya JWTZ, Gongo la Mboto, hali zao zimeendelea kuimarika na kuruhusiwa ambapo majeruhi 50 pekee ndiyo wamebaki katika hospitali hizo.

Katika majeruhi hao 50, 27 bado wamelazwa katika Hospitali ya Amana wanawake wakiwa ni 21, wanaume watatu na watoto watatu ambapo awali hospitali hiyo ilipokea majeruhi 242.

Aidha, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Kitengo cha Mifupa (MOI), wamebaki majeruhi 27, wakiwamo wawili walio katika uangalizi maalumu (ICU), wakati Hospitali ya Temeke imebaki na majeruhi wawili.

Katika hatua nyingine, wabunge wa CUF wamewatembelea majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Amana na Temeke ili kuwajulia hali na kuwapa pole sanjari na kuwatembelea waathirika waliopo jirani ya kambi hiyo na ndani ya kambi ili kujionea maghala yaliyotokana na mlipuko huo.

Aidha, Watanzania zaidi ya 60 wenye asili ya Kiasia jana walichangia damu salama kwa ajili ya kuwasaidia majeruhi walioathirika na mlipuko wa mabomu katika Kambi ya JWTZ Gongo la Mboto.

Wananchi hao wa Jumuiya ya Singasing, Shinaithnasheri, Hindu wakiongozwa na Dk. Kulbir Gupta na Fazleabbas Dhiran walitoa damu hiyo jana na kuiwasilisha katika kituo cha damu salama kwa ajili ya kuwasaidia watu waliojeruhiwa.

Pia jumla ya Sh 11,687,000 zimechangwa jana na watu waliohudhuria maadhimisho ya kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) kwa ajili ya watu walioathirika na mabomu ya Gongo la Mboto.

Katika maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Istiqaama nchini na kufanyika jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal alikuwa mgeni rasmi.

CHANZO:HABARI LEO

No comments: